WATUMIAJI WA PIKIPIKI CHUKUENI HII KUTOKA DODOMA


Na Mtapa Wilson, Dodoma

Inawezekana.  Dereva wa bodaboda kuvaa kofia ngumu anapoendesha.  Ama abiria kuvaa kofia ngumu anapopanda bodaboda.  Inawezekana tena bila shuruti.  Kupitia sheria ndogondogo wanazojiwekea wanaweza kabisa kuhimizana kuvaa kofia ngumu miongoni mwa madereva na abiria wa bodaboda.

Sheria ya usalama barabarani ya mwaka 1973 kifungu 39 kifungu kidogo cha 12 inamtaka dereva wa chombo cha moto chenye magurudumu mawili au matatu kama vile bodaboda kuvaa kofia ngumu wakati wote anapokuwa amepanda chombo hicho.

Sheria hiyo inatoa msisitizo zaidi kwa dereva kuvaa kofia ngumu peke yake huku ikikaa kimya kuhusu abiria anayebebwa.

Baadhi ya maeneo nchini kama vile Dodoma mjini, bodaboda wamejiwekea sheria ndogondogo zinazowahimiza miongoni mwao na abiria wao kuvaa kofia ngumu bila shuruti ya askari wa usalama barabarani. 

“Tuna utaratibu wetu wa kupiga faini ya shilingi 5,000 kwa dereva bodaboda anayeendesha bila kuvaa kofia ngumu au kubeba abiria ambaye hajavaa kofia ngumu.  Hii ni faini tuliyojipangia katika kituo chetu kwa anayekiuka utaratibu.

Faini hiyo huitoa pale anapokosea mara ya kwanza, lakini akifululiza zaidi ya mara tatu tunamkamata na kumpeleka polisi akaandikiwe faini ya serikali ambayo ni shilingi 30,000.”

Hiyo ni kauli ya Mwenyekiti wa bodaboda, kituo cha Jamatini, Mkoa wa Dodoma, Jumanne Seif (42),  akifafanua juu ya sheria ndogo ndogo walizojiwekea, ambazo zinamlazimisha dereva na abiria kuvaa kofia ngumu wanapotumia usafiri wa a bodaboda kwa ajili ya usalama wao.

Dodoma mjini ni eneo pekee nchini, ambalo bodaboda wake wamefanikiwa kwa kiasi kikubwa kujiwekea sheria ndogo ndogo katika vituo vyao wanavyopaki ili kuhimizana wao kwa wao kuvaa kofia ngumu wanapoendesha ama wanapobeba abiria.

Hilo lilijidhihirisha baada ya mwandishi kutembelea vituo takribani 10 vya Shabiby terminal, Cape town, Puma, Jamatini, NK, Maisha Club, Nyerere Square, General hospital, Sarafina na Stendi kuu vyenye bodaboda takribani 209 na kujionea kila dereva akiwa na kofia ngumu mbili, ikiwa moja ni kwa ajili ya dereva na nyingine ya abiria.

Aidha mwandishi aliona bodaboda wengi wakiwa wamevaa kofia ngumu wanapoendesha pamoja na abiria waliowabeba ikiwa ni utii wa sheria ndogo ndogo walizojiwekea katika vituo vyao pamoja na sheria mama ya usalama barabarani ya mwaka 1973.

Mwenyekiti wa kituo cha Jamatini, Seif, alisema uvaaji wa kofia ngumu ni usalama wa abiria mwenyewe na dereva anayeendesha bodaboda na kusisitiza kuwa bodaboda imetengenezwa katika mfumo ambao ni lazima mtu anayepanda avae kofia ngumu kwa ajili ya usalama wake.

“Abiria akikataa kuvaa kofia ngumu katika kituo changu hatuwezi kumbeba.  Tunamwacha aende akatafute bodaboda sehemu nyingine,” anaeleza Mwenyekiti huyo wa bodaboda.

Michael Mathias (34), ni dereva wa bodaboda namba MC 818 AAJ, kituo cha NK, Dodoma alisema yeye binafsi anavaa kofia ngumu kwasababu pikipiki ni chombo cha matairi mawili na hakina bodi, hivyo ajali inapotokea mtu anaweza kuumia kichwa ambacho kimsingi hakina spea kama ilivyo kwa miguu au mikono.

“Kwa upande wangu natekeleza hilo kwasababu naelewa madhara ya kutokuvaa lakini wapo baadhi wasiokuwa waelewa hawavai.  Na tuna ugomvi mkubwa na abiria wasiovaa kofia ngumu.” Anasema Mathias.

Aidha Daniel Nshunju (27) ambaye ni dereva bodaboda namba MC 292 BFF kituo cha Shabiby bus terminal, Mkoani Dodoma anasema kila bodaboda inayopaki katika kituo chao ina kofia ngumu mbili, lakini kuna baadhi ya abiria hawataki kuvaa kwa madai ya kuwa ni chafu.

Nshunju alisema ikitokea hivyo hawezi kumbeba abiria huyo hata kama atamlipa fedha nyingi kiasi gani kutokana na usimamizi mkali wa askari, ambao huvaa kiraia na kufuatilia bodaboda wasiotii sheria ikiwemo kutokuvaa kofia ngumu.

Ufuatiliaji na udhibiti wa askari kwa dereva na abiria asiyevaa kofia ngumu ni utekelezaji wa sheria ya usalama barabarani nchini ya mwaka 1973.

Sheria hiyo inaakisi muongo mmoja wa utekelezaji wa usalama barabarani kimataifa ili kupunguza vifo vitokanavyo na ajali kwa asilimia 50 ifikapo 2020.

 “Abiria asiyetaka kuvaa kofia ngumu hatumbebi na tunamuona kama mtu asiyejali usalama wake mwenyewe wala kutii sheria kwani hata ukikamatwa hakuna anachokusaidia.  Siwezi kumbeba mtu asiyevaa kofia ngumu kwasababu ni majanga,” anasema Nshunju.

Wakati bodaboda wa eneo la Dodoma mjini wakionekana kutii sheria ya kuvaa kofia ngumu pamoja na abiria wanaowabeba, hali ni tofauti katika jiji la Da r es Salaam, ambapo bodaboda wengi pamoja na abiria si watiifu kwani wengi wao hawavai kofia ngumu.

Mwandishi alizunguka kwa takribani siku 21 mwaka huu, katika wilaya tano za Ilala, Kigamboni, Kinondoni, Temeke na Ubungo kwenye vituo 10 kila wilaya vyenye jumla ya bodaboda takribani 1,136, ambapo alishuhudia mara kadhaa bodaboda wakiendesha bila kuvaa kofia ngumu na kubeba abiria bila kuwavalisha kofia ngumu.

Baraka Ruben (37) ni dereva wa bodaboda kituo cha GBP Posta mpya wilaya ya Ilala, alisema abiria wengi wanadai kofia nyingi za bodaboda ni chafu, jambo linalofanya wanakataa kuvaa, lakini hata hivyo wanalazimika kuwabeba wakiwa wamezishikilia mkononi.

Uchafu unaotajwa na abiria wengi hususani wanawake ni kwamba, kofia ngumu zinavaliwa na abiria wengi, suala linalosababisha kuchafuka na jasho pamoja na mafuta wanayopaka.

Aidha inaelezwa kuwa ni nadra sana kukuta kofia ngumu ya abiria ni safi ingawaje wapo madereva baadhi wanaosafisha kofia ngumu za abiria.  Lakini inakuwa ngumu kuziamini kutokana na kutumiwa na watu wengi.

Chimila Nassor (30) ni dereva wa bodaboda, kituo cha Mwalimu Nyerere Ferry wilaya ya Kigamboni alisema wapo baadhi ya bodaboda wenye kofia mbili lakini changamoto kubwa ni baadhi ya abiria hususani wanawake hawapendi kuvaa kwasababu ya kuhofia kuvuruga mitindo yao ya nywele.

“Ukisema uwe unakataa abiria wasiokubali kuvaa kofia ngumu unaweza kukataa abiria hata sita kwa siku kwa sababu wako wengi sana wasiopenda kuvaa kofia ngumu, matokeo yake unakuwa unaharibu siku yako, inabidi uende nao vivyo hivyo. 

Katika kituo chao wanahimiza sana kuvaa kofia ngumu lakini inashindikana kutokana na hali ngumu ya biashara kwakuwa bodaboda wengi wanakaa muda mrefu bila kupata abiria na pale anapokuja anaweza kukataa kuvaa kofia ngumu, jambo ambalo inawawia vigumu kumwacha.

Amiri Mnugwa (50) ni dereva bodaboda, kituo cha Makumbusho stendi, wilaya ya Kinondoni, katika kituo chao hawaachi abiria kwakuwa kakataa tu kuvaa kofia ngumu wala hakuna utaratibu wa kumlazimisha dereva avae kofia ngumu ndio aendeshe.

“Kama abiria au dereva hataki kuvaa kofia ngumu huwa tunamwambia kama ana shilingi 30,000 ya kulipa faini apande lakini kama hana aache,” anasema dereva huyo wa bodaboda.

Abdallah Mohamed (45) ni bodaboda, kituo cha Majaribio, wilaya ya Temeke, anasema kuna baadhi ya abiria wanaokataa kofia ngumu kwasababu wanahofia kuambukizwa magonjwa ya ngozi kwa madai kofi zinatumika na watu wengi.

Mohamed anaeleza zaidi kuwa anapopata abiria wa aina hiyo humshawishi avae kofia, lakini akikataa humwacha. 

Changamoto kubwa kwamba kuna dereva mwingine anaweza kumbeba vivyo hivyo ingawa anakuwa anakiuka taratibu na akiambiwa hudai akikamatwa atajua cha kueleza mwenyewe.

Jacob Elia (30) ni dereva bodaboda, kituo cha Mawasiliano stendi, wilaya Ubungo, anasema katika kituo chao wana taratibu za kuzuia kubeba abiria zaidi ya mmoja lakini suala la kofia ngumu hawalitilii mkazo sana.

“Suala la kulazimisha mtu kuvaa kofia ngumu iwe dereva au abiria hatuna kabisa.  Tunachokataa hapa ni kubeba ‘mshikaki’ tu,” anasema Elia.

Elizabeth Mihambo ni abiria wa bodaboda anasema madereva wa bodaboda wana kofia ngumu ya abiria moja tu, ambayo hubeba kila abiria anayepanda.  Hivyo anahofia kuathirika na magonjwa mengine ya ngozi kwa kuchangia kofia ngumu na watu wengi.

Naye Rose Erasto, anakiri kujua madhara yanayoweza kumpata endapo akipata ajali akiwa hajavaa kofia ngumu.  Lakini anadai kofia ngumu huvuruga mtindo wa nywele alizotengeneza wakati akijiandaa kutoka kwa ajili ya matembezi yake binafsi.

Kamanda wa polisi kanda maalum ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa, alisema wamefanya oparesheni maalum katika mikoa mitatu ya kipolisi yaani Ilala, Kinondoni na Temeke, ambapo walikamata bodaboda takribani 1,379 kwa makosa mbalimbali ya barabarani. 

Kamanda Mambosasa akaeleza pia madereva 97 walifikishwa mahakamani kwa kosa la kutokuvaa kofia ngumu na kubeba  abiria zaidi ya mmoja maarufu kama ‘mshikaki’.

Kutokana na umuhimu wa kuvaa kofia ngumu kwa madereva na abiria wa bodaboda, kuna baadhi ya maeneo nchini kama vile Dodoma mjini, ambayo madereva hao wanahimizana kuvaa kofia ngumu kwa usalama wao na abiria.

Hali hiyo inaashiria kuwa bodaboda wanaweza kuwa mawakala wazuri wa utekelezaji wa sheria ya usalama barabarani ikiwemo uvaaji wa kofia ngumu miongoni mwa abiria wakaidi.

Takwimu za jeshi la polisi kikosi cha usalama barabarani zinaonyesha kuwa mwaka 2015 kulitokea ajali za bodaboda zipatazo 2,749 ukilinganisha na ajali 4,304 zilizotokea mwaka 2014 ikiwa ni pungufu ya ajali 1,555, ambayo ni sawa na asilimia 36.

Aidha ajali hizo zilisabababisha vifo vipatavyo 971 mwaka 2015 ukilinganisha na vifo 957 vilivyotokea mwaka 2014 ikiwa ni ongezeko la vifo 14 sawa na asilimia 2.

Idadi ya majeruhi katika ajali hizo walikuwa 2,491 mwaka 2015 ukilinganisha na majeruhi 4,016 walioripotiwa mwaka 2014, ikiwa ni pungufu ya majeruhi 1,525 sawa na asilimia 38.

Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (W.H.O) mwaka 2015, vifo vingi vya bodaboda hutokana na majeraha makubwa kichwani na kusisitiza kuwa uvaaji wa kofia ngumu unasaidia kwa asilimia 40 kuepuka kifo na huokoa kwa asilimia 70 uwezekano wa  kuumia vibaya kichwani pale ajali inapotokea.
WATUMIAJI WA PIKIPIKI CHUKUENI HII KUTOKA DODOMA WATUMIAJI WA PIKIPIKI CHUKUENI HII KUTOKA DODOMA Reviewed by Unknown on 15:35 Rating: 5

No comments:

Theme images by merrymoonmary. Powered by Blogger.