MBINU ZA CHADEMA ZITAITIKISA CCM YA JPM? AMA MABADILIKO YA CCM YATAKIJENGA CHAMA?

Mwenyekiti wa CCM Taifa, Dk. John Magufuli.


Na Dotto Bulendu

Baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2005, ambapo Jakaya Kikwete alishinda kwa kishindo vyama vya upinzani hususani Chadema viliamua kufanya tafsiri ya namna ya kujijenga.

Mkakati walioibuka nao Chadema ilikuwa ni ‘Party campaign and agenda’ pia waliibuka na mikakati mingi ikiwemo Chadema Msingi kwa kukipeleka chama chini kwa wananchi.

Chadema walikuja na agenda ya ufisadi, hii iliwajenga sana baada ya kuihubiri bungeni, mitaani mpaka kwenye vyombo vya habari, viongozi wa kitaifa mpaka kwenye matawi waliimba ufisadi, wakaibuka na ‘list of shame’, hii iliwajenga sana!

Mwaka 2010 wakimsimamisha Dk. Slaa walimtikisa Kikwete, chini ya ajenda ya ufisadi, baada ya uchaguzi wa mwaka 2010, Chadema waliamua kujiuza kwa kutumia ‘Party campaign’ na ‘party strategy’.

Walikuja na kampeni nyingi, wakazindua harakati za vuguvugu la mabadiliko (Movement for change-M4C) na oparesheni zingine kama Sangara, wakaja na mkakati wa Chadema ni Msingi kwa kukiimarisha chama chini, mbinu hizi mbili ziliwajenga.

Walikuja na kampeni za kujenga ‘Party Credibility’ and ‘Popularity’, walifanya mikutano isiyo na ukomo, Chadema walifikia hatua ya mpaka mwenyekiti wa mtaa aliweza kuitisha mkutano na kupata watu, sababu ajenda kuu ilikuwa ufisadi na wananchi walikuwa wanataka kusikia kuhusu ufisadi!

Chadema walifanya maandamano kwa kila jambo, walitokea kwenye vyombo vya habari, kwenye kila mjadala, ajenda ilikuwa ufisadi, katika kuwafanya watu wakifie chama, walianzisha kampeni za kukichangia chama kwenye mikutano na mpaka kupitia simu za mkononi!

Chadema walikuwa na ajenda kuu ya chama, harakati za chama na mipango ya chama, hii iliwabeba ikawajengea ‘Credibility, Popularity na trust’

Chadema walijiingiza kwa kundi la vijana, walipata nguvu kubwa vyuo vikuu, waliimarisha Bavicha na umoja wa vijana vyuoni ikawa na nguvu kubwa, wabunge na viongozi wenye mvuto wakawa hawakauki vyuo vikuu kushiriki mijadala!

Baada ya uchaguzi mkuu wa 2010 waliibuka na kuifufua kampeni ya katiba mpya, waliwahubiria wanachama na mashabiki wao kuwa kushindwa kwao 2010 kumesababishwa na ubovu wa katiba, Slaa akaanza kampeni ya Katiba mpya, watu wakaamini katiba ina matatizo!

Upepo wa Chadema baada ya kuitikisa CCM mwaka 2010, uliwastua CCM wakafanya mabadiliko ndani ya chama, wakatengeneza timu ya tathmini, nakumbuka ilikuwa chini na Wilson Mkama ambaye baadae akaja kuwa katibu mkuu, kuna timu nyingine ilikuwa chini ya Mihanjo!

CCM walikuja na mkakati wa kujibu mapigo uliolenga kuhakikisha kwanza wanabomoa ‘credibility’ ya Chadema, Chadema walipita kwenye kipindi kigumu cha kuitwa chama cha wachaga, wakristo kabla ya kuitwa chama kinachofanya matendo ya kigaidi!

‘Counter attack’ hii iliwapa wakati mgumu chadema kuhakikisha ‘credibility’ na ‘popularity’ yao haibomoki, nakumbuka Mwigulu akiwa Naibu katibu mkuu alizunguka kwenye vyombo vya habari na kusema ana ushahidi wa CD ya Chadema wakipanga mauaji! lilikuwa kombora gumu kwa Chadema, baadhi ya viongozi wake wakakamatwa!

Mbali na ‘kucounter attack’, CCM walikuja na kampeni ya kuzunguka kuwafuata chadema mitaani, Katibu mkuu Abdulrahman Kinana na Katibu mwenezi, Nape Nnauye, walizunguka nchi nzima na wao kuishambulia serikali, walihakikisha wanaitenganisha Serikali na Chama!

CCM walihubiri kuwa makosa ya serikali si makosa ya Chama, waliibuka na kampeni ya kuvua gamba ikiwa ni kujibu mapigo ya kampeni ya ufisadi serikalini, wakaja na kampeni ya Mawaziri mizigo ikiwa ni mapigo ya serikali dhaifu iliyohubiriwa sana na upinzani hususani Chadema!

CCM waliishambulia serikali hadharani, waliwashambulia baadhi ya mawaziri na hata kuwaambia wabunge wake wasiwe watu wa kukubali kila kitu!

CCM waliamua kukileta chama chini na hii ni baada ya utafiti wa Luhanjo, wakaanzisha mabaraza ya vijana wa vyuo vikuu, nafasi za uongozi na wajumbe wanye nafasi za kwenye kushiriki mkutano mkuu zikatanuliwa mpaka chini, wajumbe wakaongezeka mpaka 380, nia ilikuwa ni kujenga dhana ya hiki ni chama chetu (sense of ownership).

Idadi ya wana CCM wenye nafasi ya kushiriki vikao vya maamuzi ikaongezeka, huku mitaani ikawa si ajabu kukutana na MNEC na mnakunywa nae kahawa! WaNEC hawa wakawa wanaishi na watu, wakawa wanakisemea chama mpaka vijiweni tena kwa Mamlaka kuwa ‘Mimi MNEC’.

Jana CCM imefanya mabadiliko makubwa sana ya idadi ya wajumbe wenye nafasi ya kuingia kwenye vikao vya maamuzi, wajumbe karibu 200 wameondoshwa!

CCM wamesema mabadiliko hayo yamelenga kuongeza ufanisi ndani ya chama, na kupunguza majungu, nakumbuka wakati idadi ya wana CCM wenye nafasi ya kuingia kwenye vikao vya chama inaongezwa, sababu ilikuwa ni kukipeleka chama kwa wanachama, kwa sababu chama ni watu!

Je, mabadiliko haya yaliyopitishwa na wana CCM yatakijenga chama ama kukidhoofisha?

Nakumbuka wakati wa Rais Kikwete ndani ya chama kulikuwa na upinzani mkali sana, kuna tetesi kuwa kuna kundi ndani ya chama liliwahi kutaka kuja na ajenda ya kumpokonya Kikwete nafasi ya Uenyekiti abaki na Urais, Kikwete hakuwafurusha chamani bali alizuia upepo huo kidiplomasia!

Je, mbinu ya sasa ya chama ya kuwafurusha wanaohisiwa kukisaliti ama kwenda kinyume na chama itakijenga ama kukibomoa chama? Ndani ya chama Kikwete atakumbukwa kwa kuwavumilia aliowaongoza, hata walipoimba mbele yake kuwa wanaimani na Lowasa aliwatazama tu huku akitabasamu!

Je, mabadiliko ndani ya CCM yatakijenga chama? Je, mbinu za sasa za kambi ya upinzania zitaitikisa CCM ya Magufuli!
MBINU ZA CHADEMA ZITAITIKISA CCM YA JPM? AMA MABADILIKO YA CCM YATAKIJENGA CHAMA? MBINU ZA CHADEMA ZITAITIKISA CCM YA JPM? AMA MABADILIKO YA CCM YATAKIJENGA CHAMA? Reviewed by Unknown on 17:31 Rating: 5

No comments:

Theme images by merrymoonmary. Powered by Blogger.