LEMA AMSHUKIA RAIS MAGUFULI KUWAITA WASALITI WALIOTAKA KUMUONA MAHABUSU

Mbunge wa Arusha Mjini (Chadema), Godbless Lema.

Na Godbless Lema

Nimetoka Magereza hivi karibuni ambako nilikuwa huko kwa zaidi ya miezi minne kwa kunyimwa masharti ya dhamana kwa dhamana iliyokuwa wazi.

Mheshimiwa Rais, nimeona kwenye vyombo vya habari leo kuwa kwamba wale Wabunge waliokuwa wanataka kunisalimia nilipokuwa magereza kuwa ni wasaliti wa chama cha CCM,

Mheshimiwa Rais wengi walinisalimia, Wachungaji , Masheikh, Wabunge na Viongozi mbalimbali, sidhani kama hatua hii ilikuwa ni usaliti isipokuwa upendo ambao ni muhimu kwa binadamu yoyote haswa wakati wa matatizo.

Mheshimiwa Rais, nimeogopa sana kwa kauli hii yako! Je, Taifa linakwenda wapi? Hivi kweli sisi Wabunge ni maadui? Kama viongozi tutafikiri utengano ni moja ya njia ya kuimarisha vyama vyetu, basi bila shaka tutakuwa tunalitendea Taifa ubaya.

Dhambi hii ikikomaa basi ni hakika kwamba lugha za udini, ukanda na ukabila hazitaacha kukomaa, ni muhimu sasa tukajenga utamaduni wa kuimiza mshikamano wa kitaifa bila kujali itikadi kama kweli tunawapenda masikini na wanyonge wa nchi hii.

Nawaomba Wabunge wenzangu walionijali wakati niko magereza wasijisikie vibaya kwani walifanya jambo jema na muhimu kwa wakati muhimu sana katika maisha yangu, ninatarajia kuwa Spika wa Bunge atatoa kauli juu ya kauli yako.

Mheshimiwa Rais wakati wa Msiba wa Christina Lissu, dada yake na Mheshimiwa Tundu Lissu, nilikuona katika msiba ule wewe na Mama yetu Mke wako.  Je, mheshimiwa Rais na wewe ulikuwa unasaliti chama chako?

Mheshimiwa Rais neno la Mungu linasema, “wapendeni maadui zenu, waombeeni wanaowaonea, wabarikini wanaowatesa” kwani kufanya hivi ni kuishi kwa thawabu za Mwenyezi Mungu.

Mungu akubariki sana, natumaini Mheshimiwa Rais sitakamatwa leo kwa ujumbe huu mfupi.

LEMA AMSHUKIA RAIS MAGUFULI KUWAITA WASALITI WALIOTAKA KUMUONA MAHABUSU LEMA AMSHUKIA RAIS MAGUFULI KUWAITA WASALITI WALIOTAKA KUMUONA MAHABUSU Reviewed by Unknown on 17:41 Rating: 5

No comments:

Theme images by merrymoonmary. Powered by Blogger.