UCHUNGUZI: MADEREVA WA BODABODA MWANZA WENGI NI WALEVI
Na Mtapa Wilson, Mwanza
Wakati
ripoti ya Shirika la Afya Duniani (W.H.O) ikisema kuwa takribani watu milioni
1.2 wanapoteza maisha kila mwaka kutokana na ajali za barabarani, ambazo
kimsingi husababishwa na sababu mbalimbali ikiwemo tabia ya unywaji wa vileo na
uendeshaji miongoni mwa madereva.
Uchunguzi
uliofanywa na mwandishi wa taarifa hii katika jiji la Mwanza, katika kipindi
cha siku 14 yaaani kuanzia Julai 8 mpaka 22, mwaka huu, unaonyesha kuwa tabia
ya unywaji wa vilevi na uendeshaji imeendelea kuwa tatizo miongoni mwa madereva
wengi wa bodaboda.
Mwandishi
alijaribu kutembelea vituo mbalimbali takribani kumi vya waendesha bodaboda vilivyopo
katika ya jiji hilo na kufanya uchunguzi ambapo alibaini kuwa katika kila kituo
kimoja kuna waendesha bodaboda wawili, watatu, wanne mpaka watano wenye tabia
ya kunywa vileo na kuendesha bodaboda.
Aidha
uchunguzi unaonyesha kuwa madereva wa bodaboda wengi huendesha wakiwa
wamekunywa vileo hasa wakati wa usiku, ambapo hutumia vilevi vya aina mbalimbali.
Mara nyingi
waendesha bodaboda wa usiku wanakunywa pombe kali zaidi ya chupa moja. Wapo wengine wanaokunywa bia za kawaida
katika kumbi mbalimbali za starehe wakiwa wanaendelea kusubiria abiria
wanaotoka kustarehe wakati wa usiku waweze kiuwapeleka nyumbani.
Hali hiyo
ilijidhirisha pale mwandishi alipotembelea klabu kubwa maarufu jijini Mwanza na
kujionea waendesha bodaboda wakinywa pombe na wengine wakitumia ugoro huku
wakisubiri abiria wao.
Wakati
mwingine waendesha bodaboda hutumia mihadarati kama mbadala wa pombe kali
ambazo hutoa harufu pale wanapozitumia.
Mwandishi
alifanya mahojiano na baadhi ya waendesha bodaboda na viongozi wa vituo kumi
vya bodaboda mkoani Mwanzo, ambao ni wasimamizi wa sheria za vituo hivyo ikiwemo
marufuku ya kunywa vileo na kuendesha miongoni, ambapo walieleza bayana suala
la tabia ya unywaji na uendeshaji lilivyo.
Athuman
Rashid, ni mwenyekiti wa kamati tendaji ya umoja wa bodaboda wilaya ya
Nyamagana, alisema kuna vijana ambao wamekuwa wakinywa na kuendesha kutokana na
hulka zao wenyewe ijapokuwa elimu wamekuwa wakiitoa juu ya tabia hiyo ya
unywaji.
“Hapa kwetu
kulikuwa na vijana wengi waliokuwa wanaendesha huku wakiwa wamekunywa. Na kuna kijana mmoja ambaye yeye alikuwa ana
tabia ya kuendesha akiwa amekunywa tu yaani asipokunywa anakwambia hawezi
kuendesha.”
“Sasa
tulikuwa tunajiuliza sana kwanini yuko namna ile au ni tabia yake tu ambayo
amejizoeza? Tuliamua kumuonya baada ya
kupata ajali akawa amejirekebisha.
Nadhani sasa ameacha. Ila sisi kama viongozi tunajitahidi kutoa elimu
juu ya suala hili zima la ulevi ijapokuwa wapo wanaotusikia na kutuelewa na
wengine hawaelewi kabisa,” alisema.
Renatus
Francis ni mwendesha bodaboda kituo cha Masai darajani ambapo panatajwa kuwa
mashuhuri kwa uuzaji wa vilevi mbadala wa viroba mathalani ugoro, alisema wapo
waendesha bodaboda wawili, watatu wanaokunywa na kuendesha na wamewahi kupata
ajali walipokaguliwa mifukoni walikutwa na chupa zenye pombe.
“watu
wanatumia vilevi kama vile bia. Serikali
ilipiga marufuku pombe za viroba. Lakini
zimekuja pombe zingine zikiwa katika chupa ndogo ambazo kuna baadhi ya madereva
ambao ni wanywaji wanavitumia,” alisema.
Mwandishi
aliamua kuvinjari eneo hilo la Masai darajani ambalo ni maarufu kwa biashara ya
ugoro, ambapo alijionea vijana wengi waendesha bodaboda wakimbilia kununua
ugoro uliofungwa katika vifungashio vya karatasi na vikiuzwa kuanzia shilingi
500 mpaka 1000.
Maeneo
mengine maarufu kwa uuzaji wa ugoro jijini Mwanza aliyoyatembelea mwandishi na
kuona waendesha bodaboda wakipatiwa huduma hiyo ya ulevi huo ni Milongo kwa
Kayese, Ofisi za zamani za stendi ya mabasi ya Tanganyika, na Station karibu na Ofisi za Idara ya
Uhamiaji.
Sebastian
Leonald, ni dereva bodaboda kituo cha Bugando hospitalini, ambaye mwandishi
alimshuhudia kwa macho akitumia ugoro wakati akiwa kazini na alipomuuliza kama
anajua endapo sheria hairuhusu alisema kuwa hajui kama ugoro una madhara ndiyo
maana unauzwa hadharani na serikali inajua.
”Ugoro
sidhani kama unakatazwa kwasababu hata ukishuka hapo chini unauzwa tu na
wamasai kwa shilingi 500. Kwahiyo ugoro
siyo kiroba. Nafikiri kama ungekuwa na
madhara basi serikali ingekuwa imeshapiga marufuku,” alisema.
Ugoro ni
tumbaku iliyosagwa na kuwa unga. Watu
huitumia kwa kuvuta unga wake puani na wengine kubwia kwa kuweka katika mdomo
wa chini.
Katika ugoro kuna kemikali ambayo
kitaalamu inafahamika kama nikotini ambayo ni hatari kwa afya ya binadamu kwani
husababisha maradhi mbalimbali ikiwemo; maradhi ya moyo, saratani,upungufu wa
nguvu za kiume, mapafu na mengineyo mengi.
Kwa mujibu wa shirika la
Africa Tobacco-Free Initiative ambalo linajihusisha na shughuli ya kudhibiti
matumizi ya tumbaku nchini ikiwemo matumizi ya ugoro, tumbaku imekuwa ikiathiri
afya za wananchi ambapo takribani watanzania 6,800 hupoteza maisha kila mwaka
kutokana na maradhi yanayosababishwa na matumizi ya tumbaku kama vile kuvuta
sigara na ugoro.
Godfrey Samwel
ni mwendesha bodaboda kituo cha Mwanza hotel ambaye Julai 3, mwaka huu alipata
ajali wakati akijaribu kulipita gari lililokuwa mbele yake lakini ghafla
alikutana uso kwa uso na gari iliyokuwa inakuja kwa mbele yake. Alipojaribu kuikwepa alijikuta akiyumba na
kudondoka kutokana na mwendokasi aliokuwa nao, hali iliyomfanya kupata majeraha
makubwa sehemu za kichwani na kupoteza fahamu papo hapo.
Samwel alipelekwa
hospitali ya Mkoa wa Mwanza, Sekou Toure akiwa hajitambui ambapo alizinduka
baada ya siku mbili. Vipimo vya daktari vilivyoandikwa
katika karatasi yake ya matibabu vilionyesha wazi kuwa alikuwa akiendesha huku
akiwa amelewa, jambo ambalo liliweza kumsababishia ajali hiyo.
Kutokana na
majeraha aliyoyapata sehemu za kichwani imemfanya kupoteza kumbukumbu mara kwa
mara.
Wakati akizungumza
na mwandishi, Samwel alikiri kutumia pombe mara kadhaa ijapokuwa alisisitiza
kuwa siyo wakati wote lakini pia imekuwa ni tabia kwa waendesha bodaboda wengi
wanaokesha usiku wakifanya shughuli hiyo.
“Kwakweli
huwa nakunywa lakini siyo sana. Sasa mtu
unakunywa bia mbili unaweza kusema mimi mlevi.
Kuna watu wanakunywa hata bia saba.
Hao ndio walevi. Kwenye kituo
chetu walio wengi wanakunywa. Katika kituo chetu tuko zaidi ya 30 lakini
wasiotumia ni kama wawili tu,” Alisema Samwel.
Naye Makoye
Kayanda, mwenyekiti wa umoja wa waendesha bodaboda mkoa wa Mwanza alisema
serikali imedhibiti uuzaji wa viroba lakini bado kuna changamoto ya pombe mpya
zinazofungashwa katika chupa ndogo ambazo huuzwa na kutumiwa na baadhi ya bodaboda
walevi ijapokuwa viongozi wamekuwa wakifanya ukaguzi kugundua wanaoendesha
wakiwa wamekunywa.
“Kwanza
naomba nikiri wazi kuwa wapo baadhi ya waendesha bodaboda ambao wana tabia ya
kulewa. Tunaishukuru serikali sana kwa
kuzuia uuzaji wa pombe ya viroba kwani bodaboda wengi walikuwa wanatumia
sana. Mbaya zaidi kwenye vituo vya
bodaboda na daladala ndiko ambako kulikuwa na kibanda cha kuuza viroba.”
“Jambo
ambalo bado linatusumbua kwa sasa ni waendesha bodaboda wa usiku. Sisi kama viongozi tunafanya ukaguzi nyakati
za mchana wote mpaka usiku saa nne au saa tano usiku. Lakini tukiondoka tu, usiku wa manane ndio
bodaboda wengi hunywa pombe na kutumia vilevi vingine,” alisema.
Kamanda wa
kikosi cha usalama barabarani Mkoa wa Mwanza, SSP Robert Hussein alisema kuna
tabia ya unywaji na uendeshaji kwa waendesha bodaboda na jeshi linajitahidi
sana kudhibiti hali hiyo kwa kutumia vifaa ambavyo wanavyo askari kwa kufanya
ukaguzi na kugundua madereva wanaolewa na kuendesha.
“Changamoto
kubwa imekuwa ni ukamataji, ambapo bodaboda wengi wamekuwa wakikwepa kwa
makusudi na pengine kuweza hata kusababisha ajali nyingine kwa kumgonga askari
mkamataji au mtumiaji mwingine wa barabara,” alisema.
Wakili mkuu
mfawidhi katika ofisi ya Mwanasheria mkuu wa serikali mkoa wa Mwanza, Seth
Mkemwa, alisema kuwa sheria ya usalama barabarani imekuwepo kwa muda mrefu tangu
enzi za ukoloni ingawa imekuwa ikifanyiwa mabadiliko kadhaa. Lakini inabidi ipitiwe upya tena ili kuweka makali
katika adhabu ambazo zinapaswa kutolewa kwa mtu atakayetiwa hatiani ili asiweze
kurudia tena tofauti na ilivyo sasa.
“Kabla ya
kufanyiwa marekebisho sheria ya mwenendo wa makosa ya jinai ya mwaka 1985,
makosa yaliyokuwa yanasababisha vifo iwe barabarani au eneo lolote lile,
aliyesababisha kifo alikuwa anafunguliwa kesi ya mauaji na akipatikana na hatia
alikuwa anahukumiwa kama muuaji kwa kifungo maisha jera au hata kunyongwa
wakati mwingine.”
“Lakini leo
hata kama dereva ataua watu 30 kwa uzembe wake binafsi, akifikishwa mahakamani
na kutiwa hatiani basi sheria itamuhukumu kifungo kisichozidi miaka mitatu
tu. Huu ni udhaifu mkubwa na inafanya
madereva wengi kuendelea kufanya uzembe wanapokuwa barabarani,” alisema.
Meneja mkuu
wa kanda ya ziwa ofisi ya mkemia mkuu wa serikali, Bonaventure Masambu alisema
jeshi la polisi kwa sasa lina vifaa ambavyo linavitumia kupima kiwango cha pombe
kwa madereva wanaokunywa, hivyo hawapokei sampuli kwa ajili ya kupima pombe.
Alisema kuna
madereva wanaofikishwa kwa ajili ya kupimwa kiwango cha matumizi ya dawa zingine
za kulevya kama vile mirungi, bangi, cocaine na heroine ambapo wengi wao wanabainika
kutumia dawa hizo.
“Kwenye dawa zingine za kulevya tunaendelea
kupata kesi nyingi ambazo tunapima sampuli na kubaini wanaotumia dawa hizo. Miaka
miwili iliyopita watu takribani 7237 tuliwapima na kubaini kuwa watu asilimia
9.33 wanatumia mirungi, asilimia 76.27 wanatumia bangi, asilimia 0.08 wanatumia
cocaine, asilimia 14.07 wanatumia heroine, asilimia 0.18 wanatumia heroine na
bangi kwa pamoja , asilimia 0.04 wanatumia mirungi na heroine kwa pamoja, watu
0.03 wanatumia mirungi na bangi kwa pamoja,” alisema.
Akifafanua
zaidi madhara ya dawa za kulevya, Masambu, alieleza kuwa mtu akinywa pombe au
dawa za kulevya humfanya ashindwe kumudu kuendesha vizuri chombo cha moto na
wakati mwingine anaweza kusinzia. Hivyo
akiwa katika usukani anaweza kujikuta anapeleka gari pembeni, kugonga watembea
kwa miguu, magari mengine, nyumba, au hata nguzo.
“Kwa kawaida
pombe ikizidi sana mwilini inaweza kuathiri uwezo wa kufanya maamuzi kwa mtu
hasa pale anapokuwa akiendesha chombo cha moto.
Vilevi vingine kama vile bangi, heroin, mandrax vinamfanya mtu aweze
kuona vitu visivyokuwa halisi kitaalamu tunaita ‘illussions’. Mtu anaweza kuona simba kumbe ni mbwa. Mtu anaweza kuona shimo kubwa kumbe ni
kikorongo kidogo cha kawaida tu,” alieleza.
Sheria ya
kupambana na kudhibiti dawa za kulevya ya mwaka 2015 (The Drugs Control and
Enforcement) inatoa adhabu ya faini isiyopungua shilingi milioni 50 na
isiyozidi milioni 500 au kifungo kisichopungua miaka 7 na kisichozidi miaka 30
au vyote kwa pamoja kwa mtu atakayebainika kujihusisha na uzalishaji wa dawa za
kulevya mfano bangi au mirungi.
Ajali za
bodaboda zimekuwa zikigharimu maisha ya vijana wengi kwa kutokuzingatia sheria
ikiwemo kunywa vileo na kuendesha.
Hospitali ya rufaa Bugando inapokea majeruhi wa ajali watatu mpaka wanne
kwa siku ambao huhitaji matibabu ya dharura na muda mrefu.
Waendesha
bodaboda wengi wao hawana bima ya afya, hivyo wanapopata ajali hujikuta wakiuza
mali zao kwa ajili ya kujigharamia matibabu.
Wapo ambao hushindwa kabisa kumudu gharama za matibabu hatimae kupewa
msamaha na hospitali.
Mfano
hospitali ya Bugando inatoa msamaha wa madeni ya matibabu takribani milioni
tano mpaka 12 kila wiki kwa wagonjwa waliofikishwa hospitalini hapo kutokana na
ajali za bodaboda, ambao wanakuwa wameshindwa kulipa gharama za matibabu
zinazohitajika.
Afisa
uhusiano wa hospitali ya Bugando, Lucy Mogele, alisema kuwa majeruhi wa ajali aliyeumia
vibaya sana hususani bodaboda hulazwa kwa muda usipungua mwezi mmoja mpaka
miezi sita na pengine mwaka mzima, jambo ambalo huongeza gharama mbalimbali kwa
mgonjwa ikiwemo matibabu na huduma zingine.
“Gharama za
kutibu majeruhi aliyeumia sana ni kubwa kutokana na ukweli kuwa hukaa sana
hospitalini. Kwa muda wote huo hupatiwa huduma
za matibabu na huduma nyingine muhimu kwa mgonjwa kama vile chakula.”
“Mara nyingi
wagonjwa wanaotibiwa hapa hujikuta wanadaiwa kuanzia laki nane mpaka milioni
mbili. Hii pia inategemea na muda. Kuna wanaokaa mpaka mwaka hospitali. Hawa gharama hukua zaidi,” alisema Mogele.
Kwa mujibu
wa daktari bingwa wa mifupa hospitali ya Bugando, Dk. Isidor Ngayomela, alisema
kwamba, “kiutaratibu kila unapoumia mfupa mmoja kitaalamu tunaita ‘region’
unahitaji huduma ya oparesheni moja kamili.
Hii ni tofauti na huduma ya oparesheni kwa idara zingine.”
“Kwahiyo
kama umeumia ‘region’ moja ya mfupa hiyo ni oparesheni moja inayojitegemea
pamoja na gharama zake. Mgonjwa kama
kaumia mifupa mitatu inamlazimu alipe mara tatu. Katika hospitali yetu ya Bugando oparesheni moja
inagharimu shilingi 320,000” alisema Dk. Ngayomela.
Kwa upande
wa abiria wa bodaboda wao walisema kuwa usafiri wa bodaboda ni mzuri kwani
umekuwa ukiwawahisha katika shughuli zao lakini changamoto imekuwa ni uhakika
wa usalama wao. Suala hilo limekuwa
likichangiwa na uendeshaji wake, ambapo waeendesha bodaboda wamekuwa na mwendo
mkali huku wengine wakionekana wamekunywa.
Getrude
James, mkazi wa Makoroboi Mwanza alisema kuwa, “kuna watu wangu wa karibu ambao
walipata ajali za bodaboda. Mmoja
alipata ajali akavunjika mguu na kuwekewa vyuma. Mwingine yeye alivunjika meno. Ajali hizi zilitokana na mwendo mkali wa bodaboda. Kwahiyo mie naogopa sana kupanda mpaka leo,”
Fetrisha
Bigaye, mkazi wa Igogo Mwanza alisema changamoto ya mwendokasi kwa waendesha
bodaboda wengi imemfanya kutafuta bodaboda moja ambayo akiwa anashida ya kwenda
mahali inamchukua kumpeleka na kumrudisha.
“Usafiri wa
bodaboda ninautumia hasa ninapokuwa na kazi zangu za haraka nikiwa kama mama lishe. Isitoshe ni nafuu sana na unaweza kukuwahisha
mahali unapokwenda. Nina bodaboda wangu
maalumu wanaonipeleka na kunirudisha mahali ninapotaka.”
“Kuna siku
nimewahi kupanda bodaboda tofauti kwasababu hawakuwepo ndiyo siku ambayo
nilipata ajali na kuumia mguu, ambapo ilinigharimu kiasi cha shilingi 10,000 na
yeye wala hakunichangia kwa lolote,” alieleza Bigaye.
Sheria ya
usalama barabarani ya mwaka 1973 kama ilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2002
kifungu cha 44, inaeleza kuwa ni kosa la jinai kwa dereva yeyote kuendesha au
hata kujaribu kuendesha akiwa amekunywa au kutumia dawa za kulevya.
Taarifa iliyotolewa
na Ofisi ya Kamanda wa kikosi cha usalama barabarani mkoa wa Mwanza, Julai 19,
mwaka huu, inaeleza kuwa katika kipindi cha miaka mitano iliyopita kumekuwepo
na ajali za barabarani zipatazo 1,540, ambazo zinajumlisha bodaboda na magari
kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo unywaji na uendeshaji.
Ikifafanua
zaidi taarifa hiyo ilisema kuwa katika kipindi cha miaka mitano iliyopita yaani
kuanzia mwezi januari mpaka disemba 2012 mpaka 2016 kulitokea jumla ya ajali 1,540.
Takwimu za
taarifa hiyo zinaonyesha mwaka 2012 kulikuwa na ajali asilimia 34.5, 2013
asilimia 21.5, 2014 asilimia 17.7, 2015 asilimia 13.3 na 2016 asilimia 12.6,
asilimia 51 kati ya ajali hizo zilikuwa ni ajali za vifo, asilimia 40 ajali za majeruhi
na asilimia 9 zilikuwa ni ajali za kawaida.
Hata hivyo
jeshi la polisi kikosi cha usalama barabarani linafanya jitihada kubwa za
kusimamia sheria ya usalama barabarani kwa kutoa elimu kwa makundi yote ya
watumiaji wa barabara, kushirikiana na watunga sheria ili zitungwe sheria kali
zaidi zinazokwenda na wakati, kukamata wanaovunja sheria kwa kufanya doria na misako
pamoja na kupima ulevi miongoni mwa madereva katika maeneo mbalimbali ya jiji
la Mwanza.
Mwenyekiti
wa Taasisi ya mabalozi wa usalama barabarani nchini (RSA), John Seka, alisema nchi
nyingi zilizoendelea zimekuwa na kampeni maalumu pamoja na matangazo mengi ya
usalama barabarani, hali inayoleta mwamuko katika jamii.
Alisema hapa
nchini kuna tatizo la usimamizi wa jeshi la polisi kikosi cha usalama
barabarani, kwani bado halijaweza kujitosheleza kwa rasilimali kama vile vifaa vinavyopima
ulevi na askari wa kudhibiti tabia hiyo kwa mdereva katika maeneo mbalimbali ya
barabara.
“Usalama
barabarani bado una changamoto. Kuna
askari wachache wa usalama barabarani na wengi wao hawana vifaa
vinavyotosheleza katika ukaguzi na upimaji wa vileo kwa madereva,” alisema.
UCHUNGUZI: MADEREVA WA BODABODA MWANZA WENGI NI WALEVI
Reviewed by Unknown
on
15:57
Rating:
No comments: