MFAHAMU SIR GEORGE KAHAMA, Mpigania uhuru Tanganyika na Waziri wa kwanza wa Mambo ya Ndani
Clement George Kahama maarufu kama Sir George Kahama. |
Na Mwandishi wetu
Taifa limempoteza moja ya viongozi wake mashuhuri na mwanaharakati wa uhuru wa Tanganyika wakati huo (Tanzania kwa sasa), Clement George Kahama maarufu kama Sir George Kahama, ambaye alifariki dunia jana baada ya kuugua na kulazwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH).
Sir George alikuwa Waziri wa Mambo ya Ndani wa kwanza kabisa baada ya Tanganyika kupata uhuru wake mwaka 1961 kuanzia mwaka 1961 mpaka mwaka 1962, kabla nafasi hiyo kuchukuliwa na Oscar Kambona, ambaye alihudumu kuanzia mwaka 1962 mpaka 1963.
Sir George ni mtumishi wa umma aliyekuwa mtendaji mkuu na mwanasiasa aliyekuwa mahiri na makini, katika utendaji kazi kuanzia nyakati za Tanganyika kudai uhuru mnamo miaka ya 1950, hadi kujitawala mwaka 1961, na baada ya uhuru mpaka alipostaafu utumishi wake kwa umma.
Sir George alipelekwa Uingereza na Chama cha Ushirika wa zao la Kahawa cha jimbo lililoitwa Ziwa Magharibi wakati ule, likiwa na wilaya za Bukoba, Karagwe, Biharamulo na Ngara, na sasa ni mkoa wa Kagera, ili kusomea taaluma ya ushirika na masoko kwa ajili ya maendeleo ya chama kile.
Katika kutimiza dhana yao ya kuzima harakati za Nyerere za kudai uhuru, na kwa vile hakuwa peke yake katika harakati zile, wakoloni walimpatia masurufu yasiyokidhi mahitaji yake akiwa masomoni, kusudi akose uwezo wa kuwasiliana na waasisi wenzake kwa kuwatumia nyaraka kwa njia ya posta.
Alipokwisha taabika kwa muda mrefu akisaidiwa na baadhi ya wanachuo wenzake kutoka Tanganyika waliokuwa katika vyuo mbalimbali vya Uingereza, ndipo alipodokezwa ya kuwa yupo mwenzao aitwaye Clement George Kahama katika chuo kingine kuwa, alikuwa na uwezo kifedha kutokana na kusomeshwa na chama cha ushirika wa zao la kahawa.
Mwalimu Nyerere alifurahi akawa na matumaini ya kusaidiwa, kwanza kwa sababu alikwishaona ushirikiano wa Watanganyika wengine, akajua hata Sir George atamsaidia.
Lakini kwa mujibu wa Sir George, tumaini la Nyerere lilizidishwa na ukweli kwamba, wote wawili ni watani wa jadi.
Tangu walipokutana mpaka waliporejea nyumbani baada ya kuhitimu masomo, gharama zote za kutuma nyaraka za kisiasa kuja kwa waasisi wa harakati za kudai uhuru, zilitolewa na Sir George, kiasi kwamba, hata wenye kujadili ni jinsi gani alipachikwa cheo cha Sir, wanadhani Nyerere kiutani huenda ndiye alimwita vile kutokana na mazingira ya msaada huo.
Sir George Kahama atakumbukwa kama mwanasiasa aliyelitumikia Taifa letu katika nyadhifa mbalimbali zikiwemo za ubunge, uwaziri na ubalozi toka enzi za Mwaimul Nyerere.
Kubwa zaidi, atakumbukwa kama mmoja wa jopo la watu wanne walioenda nchini Uingereza na Umoja wa Mataifa (UN) kupeleka ujumbe wa Watanganyika juu ya utayari wao wa kujitawala kama Taifa huru. Mungu ailaze roho ya Sir George Kahama mahala pema peponi. Amen!
MFAHAMU SIR GEORGE KAHAMA, Mpigania uhuru Tanganyika na Waziri wa kwanza wa Mambo ya Ndani
Reviewed by Unknown
on
12:09
Rating:
No comments: