ASKARI WA USALAMA BARABARANI KIGOMA, HII INAWAHUSU
Mkuu wa Kikosi cha Usalama barabarani nchini, Kamanda Fortunatus Musilimu. |
Na Mtapa Wilson
Mazoea
hujenga kawaida. Hivi ndivyo unavyoweza
kusema ukisafiri katika barabara ya kutoka Kigoma mjini kwenda Manyovu, mpakani
mwa Tanzania na Burundi.
Utaona gari
ndogo aina ya Noah na taksi nyingi aina ya ‘Toyota Pro box’ maarufu kama
‘mchomoko’ zikibeba abiria na mizigo huku zikisafiri umbali wa kilomita zaidi
ya 60.
Pata picha
gari yenye uwezo wa kubeba abiria watano inabeba abiria 10 mpaka 12. Wakati mwingine gari inayobeba abiria nane
inabeba abiria 15 mpaka 20 huku ikichanganya na mizigo ya mikungu ya ndizi na
nanasi.
Tatizo kubwa
ni abiria wengi kutokufunga mikanda ya usalama wanapokuwa ndani ya usafiri huu
mashuhuri huko Manyovu kutokana na kujazana wengi ndani ya gari mithili ya
nyanya kwenye tenga.
Katika
uchunguzi wa mwandishi aliyesafiri kwa usafiri wa ‘mchomoko’ mara kadhaa
barabara ya Manyovu alishuhudia ‘mchomoko’ namba T428 DEE wenye uwezo wa kubeba
abiria 5 ukiwa umebeba abiria 10, ambao hawakufunga mkanda, wakiwa wamejezana
pamoja na mizigo ya matunda mbalimbali.
Aidha
mwandishi aliona ‘mchomoko’ namba T479 ALR umejaza abiria bila kufunga mikanda
huku wengine wakikaa nyuma ya buti pamoja na mafurushi ya nanasi na mikungu ya
ndizi.
Imeelezwa
kuwa uchanganyaji wa abiria na mizigo katika magari ya abiria imekuwa ni hali
ya kawaida kwasababu wakazi wengi wa Manyovu, ambao ni wafanyabiashara
hutegemea zaidi usafiri wa ‘mchomoko’ kwajili ya kusafirishia bidhaa zao kwenda
mnadani kama vile Kalinzi na Kigoma mjini kwa madai ya kuwa ni usafiri nafuu
ukilinganisha na magari rasmi yanayobeba mzigo.
Sheria ya
usalama barabarani ya mwaka 1973 kifungu cha 39 inakataza dereva wa chombo cha
moto kubeba mzigo wenye uzito mkubwa ukilinganisha na uwezo wa gari. Pia inamkataza dereva kubeba idadi kubwa ya
abiria ukilinganisha na uwezo wa gari husika.
Aidha sheria
hiyo inaelekeza kwa dereva atakayekiuka kulipa faini isiyopungua kati ya
shilingi 20,000 na 50,000 au kifungo kisichopungua miaka mitatu ama adhabu zote
mbili kwa mpigo.
Kuna wakati
mwandishi alipanda gari aina ya Toyota Noah namba T663 DDF ambapo dereva
alibeba abiria takribani 20 kwa kuwabananisha bila kufunga mikanda.
Dereva wa
gari hilo, Rashid Mussa (30), alisema wanalazimika kubeba abiria wengi
kwasababu ya kutengeneza faida kubwa.
Alisema
kubeba abiria kulingana na uwezo wa gari unatia hasara kwakuwa wanasafiri
umbali mrefu na nauli inayolipwa na abiria ni kiduchu mno.
“Kama
unavyoona gari ni nyingi. Hapa tulipo
tunapakia kwa foleni. Ili upate faida ni lazima ubebe abiria wengi zaidi. Vinginevyo utakuwa unafanya kazi bure,”
alisema.
Deogratius
Ramadhan ni mmiliki na dereva wa ‘mchomoko’ namba T219 ATS alisema mbali na
faida inayopatikana kwa kujaza abiria lakini ukweli ni kwamba, abiria walio
wengi wanakabiliwa na umasikini mkubwa, hivyo huomba msaada wa nauli pungufu,
hali inayowalazimu kuwabeba wengi kwa kufidia gharama hiyo.
“Mie Manyovu
ndio nimezaliwa na kukulia. Unakuta nipo kazini anakuja jirani kabisa anajua
nauli 5,000 lakini yeye anataka umbebe kwa 2,000 au 3,000. Siwezi kumuacha kwa ujamaa tulionao. Hapo sasa inanibidi nibebe abiria zaidi ili
kufidia wanaolipa kidogo,” alisema.
Pamoja na
changamoto ya abiria na mizigo kujazwa kupita kiasi katika ‘michomoko’ hiyo,
hakuna sehemu hata moja ambayo mwandishi alishuhudia ukaguzi wa askari
ukifanyika na hatua zikichukuliwa.
Barabara ya
Manyovu ina vizuizi takribani vinne ambavyo vinakaliwa na askari. Lakini mwandishi aliweza kupita akiwa ndani
ya ‘michomoko’ iliyojaza abiria wengi na mizigo kupita uwezo wake lakini
iliruhusiwa kupita bila bughuza yoyote.
Akiwa ndani
ya usafiri huo, mwandishi alipita katika vizuizi vya askari maeneo ya Mwandiga
kwa Zitto, Kalinzi, Kasagamba na Kiremba ingawa abiria wote walikuwa
hawakufunga mikanda.
kwa mujibu
wa Sumatra magari madogo ya abiria kama vile Noah yanaruhusiwa kusafiri umbali
usiozidi kilomita 50, lakini hali ni tofauti katika eneo la Manyovu,
ambapo Noah na taksi ‘mchomoko’
zinasafiri umbali zaidi ya kilomita 60 huku abiria wake wakiwa hawajafunga
mkanda.
Chiku Shaban
(37) ni abiria mkazi wa Manyovu mpakani alisema wapo abiria wanaofahamu umuhimu
wa kufunga mikanda ndani ya gari lakini wanashindwa kutokana na kujazana kwa
abiria na mizigo ndani ya gari kupita kiasi.
“Unaweza
kupanda gari lenye uwezo wa kubeba abiria wanne na dereva wa tano. Lakini unakuta mnajazwa mpaka 12. Sasa hapo abiria wote mtafungaje hiyo
mikanda?” aliuliza.
Barabara ya
Manyovu ina Noah saba na ‘michomoko’ zaidi ya 120, ambayo hubeba abiria na
mwandishi alishuhudia mara zote alizopanda usafiri huo, abiria wakiwa
hawajafunga mikanda.
Katika
uchunguzi wake, Septemba 20, mwaka huu 2017, mwandishi alipata ajali kwenye
mchomoko namba T137 DEX katika barabara ya Manyovu akitokea Kigoma mjini
kuelekea mpakani katika eneo la Kiremba baada ya taili ya mbele kushoto
kupasuka.
Gari
iliyumba mara kadhaa njia nzima huku abiria (akiwemo mwandishi) waliokuwa ndani
ya gari hilo wakigongana kwa mtikisiko mkubwa kutokana na kutokufunga mikanda
ya usalama.
Rhoda Nashon
(60) ni mmoja wa abiria mkazi wa Munanila aliyenusurika katika ajali hiyo
alisema imekuwa ni kawaida kwa madereva kujaza abiria wengi, hali inayofanya
wanashindwa mpaka kufunga mkanda na kujiweka katika hatari pale ajali
inapotokea.
“Huku kwetu
hata kama gari imejaa lakini bado dereva anapakia. Hata abiria wenyewe wanaona gari limejaa bado
wanaingia,” alisema.
Mkuu wa Mkoa
wa Kigoma, ambaye ni Mwenyekiti wa kamati ya usalama barabarani, Brigedia
Jenerali Emmanuel Maganga, alikiri kuwepo kwa tatizo hilo na kudai kuwa
wanadhibiti hali hiyo ingawa madereva na abiria wameendelea kufanya hivyo kwa
mazoea.
“Tumewahi
kulijadili hilo na kuchukua hatua za kuzuia lakini ikaonekana wananchi
wameshazoea huo usafiri. Kwa sasa
tumelifumbia macho kidogo wakati tukiendelea na kuandaa mkakati wa kuondoa
kabisa tatizo hilo,” alisema.
Afisa leseni
na udhibiti usafiri wa barabarani kutoka Mamlaka ya Usafiri wa Majini na Nchi
kavu (Sumatra) Mkoa wa Kigoma, Amaniel Sekulu, naye alikiri kupokea taarifa
hizo lakini akasema ‘michomoko’ imesajiliwa na Manispaa ya Kigoma Ujiji kama
taksi kwa ajili ya huduma za mjini tu lakini inakiuka sheria kwa kusafirisha
abiria.
“Mabasi yote
yanakaguliwa asubuhi kabla hayajaondoka stendi.
Tunakagua masuala mbalimbali ikiwemo idadi ya abiria na mikanda.
Tukimbaini dereva kakiuka sheria tunampiga faini. Lakini hiyo ‘michomoko’ iko chini ya
manispaa, na na huko ndiko wanapata leseni,” anasema.
Mwanasheria
wa Manispaa ya Kigoma Ujiji, Emmanuel Mkwe alikana‘michomoko’ hiyo kuwa chini
ya manispaa yake kwakuwa walishawafukuza zamani na kuhamia halmashuri ya wilaya
ya Kigoma Vijijini, baada ya kushindwa kufuata utaratibu ikiwemo kupaki katika
kituo kimoja kwa ajili ya kukodiwa, na siyo kubeba abiria kama inavyofanya
sasa.
Afisa
biashara wa halmashauri ya Kigoma Vijijini, Boniphace Buberwa alikiri usafiri
huo kuhamia katika halmashauri yake tangu mwaka 2014, lakini akasema hawakutoa
leseni kutokana na kukosekana kwa sheria ndogo, ambapo walianza kwanza mchakato
wa kutunga sheria hizo na zitakapokamilika ndio wataanza kutoa leseni.
“Sasa tupo
katika mchakato wa kupitisha mapendekezo ya sheria. Hao unaowaona sasa wanafanya kazi bubu
kwakuwa hawana utaratibu ndio maana wanabeba abiria hovyo,” alisema.
Kamanda wa
Polisi Mkoa wa Kigoma, Ferdinand Mtui, alisema jeshi limekuwa likifanya ukaguzi
wa magari yote katika vizuizi mbalimbali ingawa kuna baadhi ya askari siyo
waadilifu ambao huruhusu ‘michomoko’ hiyo kuendelea na safari ijapokuwa
imevunja sheria ikiwemo kubeba abiria wengi pasina kufunga mkanda.
“Ni kweli
kuna uhuma za rushwa zinazoelekezwa kwa askari wetu. Tunazipokea.
Lakini wajue kabisa kuna mbinu zetu tutakazozitumia kuwabaini na
kuwachukulia hatua zaidi,” alisema.
Pamoja na
maelezo hayo, Kamanda Mtui, hakuweza kumweleza mwandishi ni idadi ya askari
wangapi ambao wamebainika si waadilifu na hatua zilizochukuliwa dhidi yao ili
kuongeza ufanisi wa askari wengine wanaosimamia usalama barabarani ikiwemo
abiria kufunga mkanda.
Kutokana na
changamoto ya ‘michomoko’ inaripotiwa kuwa mwaka 2016 kulitokea ajali 10 za
‘michomoko’ na kusababisha vifo vya watu saba na kujeruhi mtu mmoja.
Hiyo
inaonyesha madhara ya usafiri wa ‘mchomoko’ kwa kusababisha idadi kubwa ya vifo
mkoani Kigoma ukilinganisha na wilaya ya Kinondoni ambapo kulitokea ajali za
taksi 54 bila kusababisha kifo isipokuwa zilijeruhi watu 18.
Kwa mujibu
wa shirika la Afya Duniani (W.H.O), kufunga mkanda kwa abiria wa kiti cha mbele
husaidia kwa asilimia 50 uwezekano wa kupata majeraha makubwa pale ajali
inapotokea na humsaidia abiria aliyekaa kiti cha nyuma kwa asilimia 75.
Sheria ya
usalama barabarani nchini inamtaka dereva na abiria wote kufunga mkanda katika
magari ya abiria kama vile mabasi, lakini pia inamtaka dereva na abiria wa kiti
cha mbele peke yake kufunga mkanda katika magari madogo binafsi.
Hivyo basi,
kuna haja ya kufanya marekebisho katika sheria yetu ili kulazimisha watu wote
kufunga mkanda kwa ajili ya kupunguza madhara ya ajali katika gari ndogo kama
vile Noah na ‘michomoko’ ambayo maeneo mengi yaliyoko pembezoni mwa mjini
inafanya kazi ya kubeba abiria.
Hii inawezekana kwakuwa kuna nchi barani Afrika kama vile
Afrika Kusini, Botswana, Namibia, Zambia na hata Malawi, ambazo zina sheria
inayolazimisha abiria aliyekaa kiti cha mbele, nyuma pamoja na dereva kufunga
mkanda wanapokuwa wamepanda gari.
ASKARI WA USALAMA BARABARANI KIGOMA, HII INAWAHUSU
Reviewed by Unknown
on
15:15
Rating:
No comments: