WAKONGWE WA SIASA WALIOWAHI KUFUKUZWA CCM

Aliyekuwa Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam, Ramadhan Madabida.

Na Dotto Bulendu

Vyama vya siasa kufukuza wanachama wake ama viongozi ni jambo la kawaida tu nchini na hata nje ya Tanzania!

Miaka hiyo akina Fortunatus Masha, Kasanga Tumbo, Oscar Kambona, James Mapalala na wengine wengi, walipishana na Mwalimu Nyerere wakafukuzwa TANU.

Akina Maalim Seif Sharif Hamad, Hamad Rashid Mohamed, Juma Duni Haji walifukuzwa ndani ya CCM baada ya kudaiwa kuufutini uchaguzi wa mwaka 1985, hawakuridhika na uamuzi wa CCM kumpitisha Abdul Wakili, kuwa mgombea wa nafasi ya Urais wa Zanzibar.

Horace Kolimba akiwa katibu mkuu wa CCM Taifa, ilikuwa kidogo atoswe, alihojiwa kwa kusema CCM imekosa dira, mtendaji mkuu wa chama aliwekwa kitimoto.

Upepo wa kufukuza wanachama na hata viongozi wakuu ulishavikumba mpaka vyama vya upinzani, NCCR baada ya kuwa chama chenye nguvu mwaka 1995, kilipita kwenye mtihani mkubwa na kusababisha akina Mabere Marando, Augustino Mrema, Masumbuko Lamwai, Benedicto Mtungurei kuachana na NCCR.

Zitto Kabwe akiwa mwanasiasa kijana mwenye nguvu ndani ya Chadema naye alikutana na kivumbi cha kufukuzwa baada ya kuvuliwa uongozi ndani ya chama chake kwa madai ya kwenda kinyume na chama chake tena akiwa kiongozi mkuu.

David Kafulila, mwanasiasa mwenye uwezo mkubwa wa kujenga ushawishi naye wakati akiwa kiongozi na mbunge ndani ya chama cha NCCR Mageuzi alikutana na dhoruba hii baada ya kufukuzwa kabla ya kusamehewa na kurejeshewa uanachama wake.

CUF walishapita kwenye kadhia hii, walimfukuza mpaka muasisi wa chama Mzee Mapalala,waliwatimua akina Hamad Rashid, Doyo Hassan, na sasa Habib Mnyaa naye kafurushwa.

Leo nasikia Lipumba nae amekuwa akitangaza kuwafukuza wakurugenzi ndani ya chama cha CUF! Nakumbuka wakati Mrema anamfukuza Mtungurei, alimtupia makombora mazito kuwa alimtoa barabarani kawa maarufu hamueshimu.

Fukuza fukuza hii ya akina Sophia Simba, Ramadhani Madabida na wengineo si jambo jipya kwenye vyama vya siasa nchini kikiwemo chama hiki kikongwe nchini (CCM).
Wapo ambao huamua kutoka wenyewe, wengine hukaa na kupambana humo humo mpaka wanatolewa.

Changamoto nayoiona kwenye vyama, wapo viongozi wasiopenda kukosolewa, wasiopenda kuona mwanachama ama kiongozi wa chini anapingana na mawazo ya kiongozi.

Wapo baadhi ya wanachama wanamisimamo yao, wapo tayari chama kife kama maslahi ama ndoto zao zimezimwa.

Wapo viongozi wanaamini wao ndiyo kila kitu, wanalotaka lazima lifuatwe.  Akitokea mwanachama akasema hili hapana, huitwa msaliti, hana nidhamu.

Wapo wanachama wakorofi, wasiojua itifaki, wasiojua falsafa na itikadi za vyama, wao kazi yao ni vurugu, kutukana na hawaheshimu hata viongozi wao.

Wapo watu kwenye vyama, hawana roho za kusamehe, ukipishana nae mfano kwenye uchaguzi ndani ya chama, atakugeuza adui, atahakikisha unateseka, unakosa amani na hata unafukuzwa.

Wapo watu kwenye vyama wanaamini kupewa uongozi maana yake kuwa unaakili kuliko wote ndani ya chama, unachosema yeye basi anadhani ndiyo sahihi.

Wapo watu ndani ya vyama, kwao busara na maslahi ya chama si kitu, jambo litafanyika kwenye vikao vya ndani, yeye kazi yake ni kusambaza nje hata taarifa za vikao vya ndani, hawa huwadhihaki viongozi wao mpaka mitandaoni bila kujali athari inayoweza kukikuta chama.

Wapo wengine wao chama hakina baya, yeye ni mtu wa kutetea mabaya, hata kama chama kinakwenda mrama.

Kuongoza taasisi hasa vyama vya siasa ni kazi ngumu sana, usipokuwa makini na maamuzi unayoyafanya, ukakosa busara, uvumilivu, moyo wa kusikia hata usiyoyapenda, utajikuta unaua taasisi yako.

Bahati mbaya siasa za Afrika leo siyo siasa za kiitikadi na falsafa, leo hakuna mijadala juu ya falsafa na itikadi za vyama, mijadala ndani ya vyama
imejikita zaidi kuzungumzia watu na siyo dira, itikadi na falsafa.

Vyama havijitambulishi kwa itikadi zao, vinajitambulisha aina ya watu vilivyo nao!
WAKONGWE WA SIASA WALIOWAHI KUFUKUZWA CCM WAKONGWE WA SIASA WALIOWAHI KUFUKUZWA CCM Reviewed by Unknown on 11:05 Rating: 5

No comments:

Theme images by merrymoonmary. Powered by Blogger.