JINSI HOSPITALI YA BUGANDO ILIVYOUBEBA MZIGO WA BODABODA

Hospitali ya Rufaa ya Bugando iliyopo jijini Mwanza.

Na Mtapa Wilson
Hospitali ya rufaa ya Bugando iliyopo jijini Mwanza imekuwa ikipata hasara takribani shilingi milioni tano mpaka milioni 12 kila wiki ikiwa ni misamaha ya gharama za matibabu ya majeruhi wa ajali za barabarani hususani bodaboda.

Hali hiyo inatokana na ukweli kuwa waendesha bodaboda wengi wanaopata ajali za bodaboda hawana bima ya matibabu wala fedha, hivyo kushindwa kumudu gharama za matibabu zinazohitajika.

Akizungumza katika mahojiano maalumu, Afisa Ustawi wa Jamii hospitali ya Bugando, Daudi Makumucha, alisema uelewa duni juu ya bima imekuwa ni changamoto miongoni mwa wananchi wengi, hali inayosabababisha majeruhi wengi wanaofikishwa hospitalini kutokuwa na bima.

“Kwakweli gharama kubwa za matibabu zinawatesa majeruhi wengi wanofikishwa hospitalini.  Unaweza kukuta majeruhi ndio alikuwa anategemewa na familia yake kama mzalishaji mkuu.”

“Majeruhi kama huyu analazimika kuuza mali zake ili aweza kumudu gharama za matibabu.  Mara nyingi gharama za matibabu wagonjwa wengi zinawaelemea sana, hali inayofanya ndugu zao na hospitali kubeba gharama hizi.” Alisema Makumucha.

Alisema hali hiyo inailazimu hospitali kutoa msamaha wa matibabu kila wiki kwa wagonjwa ambao hawana uwezo wala ndugu wa kumudu kulipa gharama hizo.

“………kuna kamati ya msamaha ya hospitali ambayo inaundwa na Mwenyekiti ambaye ni Mkurugenzi wa fedha wa hospitali na Katibu wake ni Afisa Ustawi Mkuu wa jamii wa hospitali.  Kupitia kamati hii kila wiki siku ya alhamis tunajadili mafaili ya wagonjwa mbalimbali na kutoa msamaha wa matibabu.”

“Leo peke yake Julai 13, 2017 tumejadili mafaili ya wagonjwa kumi na kupitisha msamaha wa madeni ambayo ni gharama za matibabu kiasi kinachofikia shilingi milioni tano ambapo kuna mgonjwa mmoja kutoka wodi ya mifupa ambaye alipata ajali na alikuwa anadaiwa takribani shilingi 2,474,800” alisema.

Afisa huyo aliongeza kuwa mbali na majeruhi wanaokosa bima au fedha za matibabu, wapo pia majeruhi ambao hufikishwa hospitalini hapo wakiwa wamepoteza kumbukumbu hivyo inakuwa vigumu kuchukua taarifa zake kama vile jina lake, mahali anapoishi na ndugu zake.

Kwa mujibu wa Makumucha majeruhi hao mara nyingi huwa wanapata majeraha makubwa na inawachukua muda mrefu kukaa hospitali hususani katika kitengo cha uangalizi maalum (ICU) takribani wiki moja mpaka wiki mbili akiwa kapoteza fahamu kabisa na anakuja kuzinduka wiki ya tatu ndipo anapelekwa wodini.

Katika kipindi chote hicho majeruhi anakuwa amehudumiwa bila kujua ndugu zake pengine hata jina lake.  Lakini pia majeruhi akizinduka inaanza changamoto za kutafuta ndugu zake kwa kufanya nao mawasiliano mbalimbali ikiwemo kupitia simu na kutangaza kupitia vyombo mbalimbali vya habari.

Aidha Makumucha alisema wapo majeruhi wanaofikishwa Bugando ambao wanakuwa na ndugu lakini ndugu hao hawataki kufika hospitalini hatimae wanatelekezwa wodini kutokana na hali mbaya ya kiuchumi. 

“Majeruhi anaweza kuwapa taarifa zake mpaka mawasiliano ya ndugu zake kama ni sehemu ya karibu tutafika na kama ni mbali tutafanya mawasiliano lakini bado ndugu hawafiki na sisi kama hospitali tunaamua kuwatibu mpaka wanapona na kuamua kuwasafirisha kabisa mpaka kwao,” alisema.

Majeruhi ambao wanakuwa wametekelezwa hospitalini na ndugu zao wapo ambao huamua kutoroka kwakuwa wanakuwa wameshatibiwa na kupona.  Na mara nyingi wanakuwa hawajapachikiwa vyuma katika oparesheni zao na wanajua hata akitoroka hawezi kurudi tena. 

Akielezea utorokaji wa wagonjwa Makumucha alifafanua kwamba, “unaweza kukuta katika wagonjwa 10 wanaotoka hospitali kuna wagonjwa watatu wanaotoroka kukwepa gharama za matibabu ya hospitali,”

Alisema misamaha ya matibabu kwa majeruhi wa ajali barabarani imekuwa ikiitia hasara Bugando kila wiki kati ya shilingi milioni tano mpaka 12, ambapo kwa mwezi inapoteza kati ya shilingi milioni 20 na 48.

Hii ina maana kwa mwaka mzima Bugando inapoteza kati ya takribani shilingi milioni 240 mpaka milioni 570 kutokana na msamaha wa madeni ya matibabu kwa majeruhi wa ajali za bodaboda peke yake.

Hata hivyo kuna wagonjwa baadhi wenye unafuu wa kipato kama vile wakulima wanaojiweza na wafanyabiashara ambao anagalau humudu kulipa wao wenyewe gharama za hospitali licha ya kutokuwa na bima za afya.

Wagonjwa hulipa gharama za hospitali tu ili waweze kuruhusiwa kutoka.  Lakini linapokuja suala la kuhudhuria kliniki kwa muda wa miezi kadhaa wanashindwa kumudu na wanaamua kukatisha kliniki zao na kutafuta huduma ya tiba mbadala.

Ufafanuzi wa daktari bingwa wa mifupa
Kwa upande wake daktari bingwa wa mifupa katika hospitali ya Bugando, Dk. Isidor Ngayomela, alisema kuwa wanapokea majeruhi wa mifupa watatu mpaka wanne kila siku kutokana na ajali za barabarani. 

Katika idadi hiyo wapo angalau mmoja au wawili wanaohitaji huduma ya kutibiwa na kurudi nyumbani na wengine wanahitaji kulazwa ingawa wanakuwa tayari wameshapatiwa matibabu ya dharura na kulazwa wanapofikishwa hospitalini kutegemeana na jinsi mgonjwa alivyoumia.

“Kiutaratibu kila unapoumia mfupa mmoja kitaalamu tunaita ‘region’ unahitaji huduma ya oparesheni moja kamili.  Hii ni tofauti na huduma ya oparesheni kwa idara zingine.”

“Kwahiyo kama umeumia ‘region’ moja ya mfupa hiyo ni oparesheni moja inayojitegemea pamoja na gharama zake.  Mgonjwa kama kaumia mifupa mitatu inamlazimu alipe mara tatu.  Katika hospitali yetu ya Bugando oparesheni moja inagharimu shilingi 320,000” alisema.

Akieleza zaidi Dk. Ngayomela alisema kutokana na changamoto ya gharama hizo za matibabu Bugando imeamua kupunguza gharama kwa kuhesabu gharama za matibabu kwa mgonjwa mmoja badala ya kuhesabu gharama za matibabu kwa kila sehemu ya mfupa iliyofanyiwa oparesheni (region).

Alisema hospitali imekuwa ikipata hasara kutokana na huduma za kutibu ambazo zinagharimu rasilimali kubwa ya wataalamu, muda, vifaa tiba wakati wa kufanya oparesheni, ambapo inahitajika kupachika vyuma na kufunga eneo la jeraha kwa mfupa mmoja na endapo kama kaumia mara tatu inahitaji kufanya zoezi hilo hilo kwa kila sehemu.

Daktari bingwa huyo wa mifupa alieleza zaidi wakati wa oparesheni ya mgonjwa mmoja wa mifupa pekee inahitajika jopo la wataalamu angalau sita watakaoweza kusaidiana ili kukamilisha opareshenin hiyo.

“…..ni lazima awepo daktari bingwa mmoja wa mifupa, daktari msaidizi mmoja, muuguzi wa vifaa (Instruments Nurse) kwa ajili ya kusogeza vifaa kwa daktari bingwa, wahudumu wawili wa usingizi kwa ajili ya mgonjwa na muuguzi mmoja wa pembeni (Circulating Nurse),” alieleza mtaalamu huyo wa mifupa.

Kadhalika Dk. Ngayomela alisema uzembe wa madereva wengi wa bodaboda umesababisha idadi kubwa ya wagonjwa wa mifupa wanaofikishwa hospitalini kutokana na ajali wanazokumbana nazo kila siku katika shughuli zao.

Kwa mujibu wa Dk. Ngayomela, majeruhi wengi wa ajali za bodaboda huvunjika mifupa na wanahitaji kuwekewa vyuma mathalani mtu aliyevunjika mfupa na umetoka nje inatakiwa asafishwe na kuwekewa chuma nje kitaalamu kinachojulikana kama ‘External fixator’ ambacho wagonjwa hukiita antena kwa ajili ya usalama wa kidonda na mfupa wake.

Gharama za vifaa tiba vya mfupa uliovunjika.
Akizungumzia changamoto ya gharama za vifaa tiba kwa majeruhi aliyevunjika mfupa, Dk. Ngayomela alisema kuna majeruhi wanaovunjika mifupa mirefu ya miguu na mikono, ambao wanahitaji kuwekewa vyuma kwajili ya kushikilia mifupa kwa ndani, ambavyo vina gharama kubwa inayozidi hata gharama ya oparesheni moja ya mfupa ‘region’.

“Mfano pini kwa ajili ya kushikilia katika mifupa ya vidole vya miguu au mkono ni shilingi 30,000 mpaka 40,000.  Kuna seti moja ya vyuma vinavyoshikilia mfupa mmoja uliovunjika kwa nje yaani ‘External fixator full sets’ inagharimu takribani shilingi 200,000.”

“Kuna vyuma vingine vya kuweka ndani ambavyo tunapokea kwa msaada kutoka wahisani wa nje ambavyo vinagharimu zaidi ya 500,000 ambapo oparesheni moja ya mfupa ni shilingi 320,000.  Nadhani unaweza kuona ni gharama kiasi gani?” alisema.

Aidha Dk. Ngayomela alisema vyuma vya kuweka mgongoni (back rods and screws) kwa ajili ya kushikilia eneo lililovunjika ili mgonjwa aweze kukaa na kutembea mapema vina bei zaidi. 

“Kama mgonjwa amevunjika sehemu moja (one level) inahitaji kuweka ‘screws’ nne na ‘rods’ mbili, ambapo ‘screw’ moja inauzwa dola 700 na ‘rods’ moja inauzwa dola 300., ambapo inakuwa na jumla ya dola 3,400.”

“Hii ni gharama ya vyuma peke yake bila oparesheni kwa eneo moja (one level) na kama itakuwa ni ‘level’ zaidi ya moja basi itahitaji vyuma vingi zaidi.  Endapo kama mgonjwa atakuwa hakuwekewa vyuma itamlazimu alale kitandani kwa muda usiopungua mwezi mmoja na nusu bila kutikisika,” alisema.

Kwa mujibu wa Dk. Ngayomela mgonjwa huyo baadaye ataangaliwa kitaalamu kwa kumulikwa mionzi ‘X-Ray’ ili kuona kama mfupa umeunga ndipo anaruhusiwa kunyanyuka taratibu kisha kufungwa mkanda mgumu ambao mgonjwa huvaa mgongoni kwa ajili ya kushikilia eneo lililoumia mpaka pale atakapoimarika zaidi.

Alisema vyuma anavyopachikwa mgonjwa humfanya aweze kuinuka kitandani ndani ya muda mfupi kama vile wiki moja mpaka mbili.  Bila vyuma hivyo mgonjwa anaweza kulazwa kitandani kwa muda mrefu zaidi.

Dk. Ngayomela alisema mgonjwa anaweza kukaa takribani mwezi mmoja na nusu hospitalini jambo ambalo linaleta msongamano wa wagonjwa na kusababisha upungufu wa vitanda kwani wagonjwa wengi hukaa kitandani kwa muda mrefu zaidi ukilinganisha na wale wanaoingia.

Hospitali ya Bugando ina madaktari bingwa wa mifupa watano, ambao hutoa huduma hospitalini hapo pamoja na hospitali zingine za kanda ya ziwa yenye watu takribani milioni 16 kupitia mpango wake wa kutembelea hospitali za mikoa na wilaya nyingine (Outreach programs).

Mpango huo umesaidia watu walioko mbali na Bugando kama vile Mara, Shinyanga, Kigoma na Singida, ambao hawana uwezo wa kifedha kuweza angalau kufika Bugando.

Pia umesaidia kupunguza msongamano wa wagonjwa na kupunguza lundo la gharama za matibabu ambazo mara nyingi zimekuwa zikisamehewa na Bugando kutokana na wagonjwa wengi kushindwa kumudu kulipa.

Aidha mpango huo umesaidia majeruhi wengi wa ajali za barabarani walioumia mifupa kupatiwa huduma za kitaalamu zinazohusu mifupa huko huko katika hospitali za mikoa na wilaya, badala ya kutegemea kupelekwa Bugando peke yake.

Kutokana na changamoto ya gharama za matibabu kuwa kubwa, elimu ya bima ni muhimu kutolewa ili wananchi wengi wajiunge na mifuko mbalimbali ya bima itakayowasaidia kujilinda dhidi ya majanga ya ajali kwa kupatiwa matibabu kwa unafuu zaidi.

Makoye Kayanda ni Mwenyekiti wa Umoja wa waendesha bodaboda Mkoa wa Mwanza alisema changamoto ya ukosefu wa bima ipo miongoni mwa bodaboda lakini bado wanaendelea kuitoa elimu na baadhi yao wanajiunga lakini changamoto kubwa imekuwa utekelezaji wa kusuasua wa malipo ya bima kwa bodaboda pale wanapopata ajali.

“Kuna urasimu unafanywa na kampuni za bima wakati wa kutathimini endapo bodaboda imepata ajali ili mteja aweze kulipwa.  Mara nyingi kumekuwa na ‘nenda rudi’, ambapo mteja anacheleweshewa malipo yake na pengine kutokulipwa kabisa, jambo linalowakatisha tamaa waendesha bodaboda wengi kuona kama bima haiwasaidii chochote zaidi ya ukaguzi barabarani tu,” alisema Kayanda.

Kamanda wa polisi kikosi cha usalama barabarani mkoa wa Mwanza, SSP Robert Hussein alisema kipindi cha miaka mitano iliyopita kumekuwepo na ajali za barabarani zipatazo 1540, kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo kutokana na kuzingatia sheria ya usalama barabarani kama vile mwendo kasi na unywaji na uendeshaji miongoni mwa madereva.

Akifafanua zaidi taarifa hiyo alinasema mwaka 2012 kulikuwa na ajali asilimia 34.5, 2013 asilimia 21.5, 2014 asilimia 17.7, 2015 asilimia 13.3 na 2016 asilimia 12.6.
Alisema asilimia 51 ya ajali hizo zilikuwa ni ajali za vifo, asilimia 40 zilikuwa ni ajali za majeruhi na asilimia 9 zilikuwa ni ajali za kawaida.

Kauli ya Wizara ya Afya
Msemaji wa Wizara ya Afya, Nsanchris Mwamwaja amesema suala la misamaha ya wagonjwa hospitalini lipo kila hospitali siyo Bugando peke yake hata hospitali ya Taifa ya Muhimbili au hospitali ya rufaa ya Mbeya na hospitali zingine za mikoa na wilaya nao wana tatizo kama hilo.

Mwamwaja anasema wapo wagonjwa wanaosamehewa gharama za matibabu kutokana na changamoto mbalimbali ikiwemo umasikini, hali inayofanya washindwe kumudu gharama za matibabu. 

Lakini anaongeza kuwa wapo wachache wenye bima na wale wenye uwezo wa kifedha ambao hulipa moja kwa moja katika hospitali.

Kadhalika Mwamwaja anasema serikali imeshaanza mpango wa kutoa huduma kupitia mfuko wa afya ya jamii (Health community fund), ambapo kila kaya inatakiwa kujiunga kwa ajili ya kupatiwa huduma ya matibabu. 

“Julai 31 mwaka huu tulizindua bima ya mtoto maarufu kama Toto Afya kadi kwajili ya kumlinda mtoto.  Tumeanza na hii lakini lengo la serikali ni kuhakikisha baadae kila mwananchi anakuwa na bima ya afya,” anasema.

Kwa mujibu wa Mwamwaja, bima inasaidia kuokoa gharama kubwa zinazotelekezwa kwa hospitali na serikali kwa ujumla, kwakuwa mgonjwa anakuwa alishachangia zamani huduma ya matibabu kupitia bima yake. 

Lakini mgonjwa anapokuwa hana bima wala fedha taslimu ya kulipia matibabu inakuwa ni changamoto kwa hospitali ikiwemo kubeba mzigo wa gharama hizo za matibabu.
JINSI HOSPITALI YA BUGANDO ILIVYOUBEBA MZIGO WA BODABODA JINSI HOSPITALI YA BUGANDO ILIVYOUBEBA MZIGO WA BODABODA Reviewed by Unknown on 13:22 Rating: 5

No comments:

Theme images by merrymoonmary. Powered by Blogger.