MWANANYAMALA INAVYOLIA NA UHABA WA MADAKTARI WA MIFUPA
Na Mtapa Wilson
Hospitali ya Mwananyamala inakabiliwa na upungufu wa madaktari
bingwa wa mifupa, jambo ambalo limekuwa likisababisha usumbufu kwa wagonjwa wa
mifupa ikiwemo majeruhi wa ajali za barabarani, ambao wamekuwa wakifikishwa
hospitalini hapo wakihitaji huduma ya matibabu ya mifupa.
Mganga mkuu wa hospitali hiyo, Nkungu Daniel, alisema kuwa
hospitali yake imekuwa ikipokea wagonjwa wengi wa mifupa hususani majeruhi wa
ajali mbalimbali za barabarani kuanzia watatu mpaka watano katika siku za
kawaida na majeruhi watano mpaka 10 katika siku zenye mlundikano wa watu kama
vile sikukuu, lakini changamoto kubwa imekuwa ni kukosekana kwa wataalamu wa
mifupa wanaoweza kuwahudumia wagonjwa hao.
Alisema Mwanyanala imekuwa ikitoa huduma kwa majeruhi wa ajali
za barabarani ambao wanakuwa hawajajeruhiwa vibaya sana katika mifupa ya miili
yao kwa kuwapima na mashine za X-rays, kuwashona na kuwapatia dawa muhimu,
ambazo zinawasaidia kupunguza maumivu na kutibu sehemu zilizoathirika na
majeraha ya ajali.
“Kwa sasa tuna uwezo wa kutibu majeraha madogo madogo tu ya
majeruhi wa ajali za barabarani kama vile michubuko, kuteguka na kuhama
mifupa. Lakini bado hatujawa na uwezo wa kutibu majeraha makubwa kama vile
majeraha ya kichwa na kuvunjika mifupa kutokana na kukosa wataalamu wa mifupa
katika hospitali yetu,” alisema Dk. Daniel.
Kadhalika Dk. Daniel alisema kuwa hospitali yake pia inakabiliwa
na upungufu wa mashine za vipimo vya wagonjwa wa mifupa hususani majeruhi wa
ajali katika sehemu za vichwa, jambo ambalo linawalazimu kupeleka wagonjwa
wenye majeraha makubwa kichwani katika Taasisi ya Mifupa ya Muhimbili (MOI),
ambapo wanaweza kupata vipimo na tiba bora zaidi.
“Kwakweli sasa hivi tuna vipimo vya X-rays peke yake, ambacho ni
kipimo cha kuangalia majeraha ya kawaida tu ndani mwili wa majeruhi lakini
haiwezi kupima majeraha yaliyoko kichwani. Hii ni changamoto kubwa kwetu
kwakuwa tunalazimika kuwaelekeza wagonjwa kutafuta vipimo vya city scan nje ya
hospitali yetu kisha ndio tuwatibu,” aliongeza Dk. Daniel.
Aidha Dk. Daniel alisema kuwa mbali na changamoto ya ukosefu wa
wataalamu wa mifupa na vifaa tiba kama vile vipimo vya city scan, bado
kumekuwepo na changamoto ya kukosekana kwa wahuduma wa afya wakati wa usiku
kutokana na ukweli kwamba kuna ajali nyingi zinatokea usiku na wagonjwa
wanapofikishwa hospitalini hapo wanakuta wahudumu wakiwa wachache.
Kwa upande wao majeruhi waliofikishwa katika hospitali hiyo
wameiomba serikali kuboresha zaidi huduma za afya katika hospitali za umma
hususani kuajili wataalamu wa kutosha kwa ajaili ya kuhudumia wagonjwa wa
mifupa.
Mathias Lucas, ni dereva wa bodaboda ambye ni muathirika wa
ajali wa ajali za barabarani alisema kuwa kwa sasa hospitali inajitahidi kutoa
huduma kwa majeruhi wa kawaida wa ajali lakini imekuwa ni ngumu sana kutoa
huduma kwa watu waliojeruhiwa vibaya kutokana kukosa wataalaamu.
Hivyo ameiomba serikali kuongeza wataalamu watakaosaidia kutatua
changamoto hiyo hospitalini hapo.
Changamoto hiyo ya upungufu wa madaktari pamoja na vifaa tiba
katika hospitali ya Mwananyamala imekuwepo pia katika hospitali ya Bugando
jijini Mwanza ambayo ina madaktari bingwa
wa mifupa watano pekee.
Madaktari hao hutoa
huduma hospitalini hapo pamoja na hospitali zingine za kanda ya ziwa yenye watu
takribani milioni 16 kupitia mpango wake wa kutembelea hospitali za mikoa na
wilaya nyingine (Outreach programs).
Hali kama hiyo inaikabili
hospitali ya wilaya ya Karatu jijini Arusha, ambayo ina uwezo wa kuhudumia
majeruhi watatu tu katika kitengo chake cha dharura, jambo linawalazimu
kusitisha huduma katika vitengo vingine vya hospitali ili kuongeza nguvu katika
kitengo cha dharura.
Mathalani hali hii iliweza
kujitokeza pale ajali mbaya ya basi aina ya costa, mali ya shule ya Lucky
Vincent ya Jijini Arusha ilipoacha njia na kutumbukia katika mto Merera ulipo
kwenye milima ya Rhotia na kuuwa wanafunzi takribani 32, walimu wawili na
dereva wao mmoja.
Kwa mujibu wa Daktari kiongozi
wa hospitali hiyo, Asanteli Makyao ni kwamba hospitali ya wilaya ya Karatu ina
uhaba wa vifaa katika kitengo cha dharura kinachoshughulikia matukio ya ajali,
huku ikiwa na watumishi wachache wa afya.
Hospitali ya wilaya ya Karatu
ina watumishi wa afya 146 tu wakati inahitaji watumishi angalau watumishi 245
ili iweze kukidhi ombwe watumishi iliyonao katika kutoa huduma za dharura
ikiwemo ajali.
Vilevile hospitali ya wilaya ya
Karatu inakabiliwa na ukosefu wa vifaa muhimu katika kitengo cha dharura.
Hivyo, hospitali hiyo haiwezi kutibu mtu aliyevunjika mfupa mkubwa wa mguu,
aliyeumia kichwani au uti wa mgongo, jambo linaloilazimu kuwapa rufaa ya kwenda
hospitali ya mkoa wa Arusha ya Mount Meru majeruhi wote wa ajali walioumia
kiasi hicho.
Daktari bingwa wa upasuaji
katika hospitali ya Mount Meru, Iddy Zubery anasema kitengo cha dharura katika
hospitali hiyo kina uwezo wa kupokea majeruhi angalau 10 na kuwapa huduma kwa
wakati mmoja.
Hata hivyo, Dk. Zubery nasema
kumekuwepo na changamoto kadhaa kama vile ukosefu wa mashine za kusaidia kupumua, hali
inayosababisha baadhi ya majeruhi wa ajli kupewa rufaa ya kwenda hospitali ya
KCMC Moshi mkoani Kilimanjaro.
Muuguzi katika huduma za dharura hospitali ya Mount Meru,
Simphorosa Silalye anasema mara nyingi majeruhi wa ajali za barabarani hupata matatizo
katika mfumo wa kupumua. Hivyo huihitaji
mashine za kisasa kwa ajili ya kuwasaidia kupumua tofauti na sasa ambapo bado
kuna vifaa duni vya kusaidia kupumua vinatumika kama vile ‘Bag valve’.
Kwa mujibu wa ripoti ya Shirika la Afya Duniani (W.H.O) mwaka
2015, asilimia 50 ya vifo vyote vinavyotokana na ajali za barabarani
huwakumba watembea kwa miguu, waendesha baiskeli na bodaboda, ambapo vifo vya
watembea kwa miguu ni asilimia 22, waendesha kwa miguu asilimia 5 na waendesha
bodaboda ni asilimia 23.
MWANANYAMALA INAVYOLIA NA UHABA WA MADAKTARI WA MIFUPA
Reviewed by Unknown
on
04:58
Rating:
No comments: