HOTUBA YA RAIS DONALD TRUMP ILIYOTAFSIRIWA KISWAHILI, ALIITOA BAADA YA KUAPISHWA RASMI KUWA RAIS WA MAREKANI
Rais wa 45 wa Marekani, Donald Trump, mara baada ya kuapishwa Januari 20, mwaka huu. |
Imetafsiriwa
na Julius Mtatiro
TRUMP: Jaji Mkuu Roberts, Rais Carter, Rais Clinton, Rais Bush, Rais
Obama, Wamarekani wenzangu na watu wote duniani,
asanteni sana. (MAKOFI)
Sisi, Wananchi wa Marekani, tunaungana katika juhudi za pamoja
kitaifa kujenga nchi yetu na kutunza ahadi zake kwa watu wetu wote. (MAKOFI)
Pamoja, tutaamua hatima ya Marekani na dunia kwa ajili ya watu wote
(na tutafanya hivyo) kwa miaka mingi ijayo. Tutakutana na changamoto,
tutakutana na vikwazo, lakini tutahakikisha kazi inafanyika.
Kila miaka minne, tunakusanyika hapa kubadilishana madaraka kwa njia
ya amani, na tunamshukuru sana Rais Obama na mke wa Rais Bi. Michele Obama kwa
msaada wao mkubwa muda wote tulipokuwa tunafanya mchakato huo. Wamekuwa watu
muhimu. Asanteni sana. (MAKOFI)
Pamoja na hayo, sherehe ya leo, ina maana kubwa, hatuko hapa kwa
ajili tu ya kuhamisha madaraka kutoka utawala mmoja kwenda mwingine au kutoka
chama kimoja kwenda chama kingine, lakini tuko hapa kuhamisha madaraka kutoka
Washington D.C na kuyakabidhi kwenu, watu. (MAKOFI).
Kwa muda mrefu, kikundi kidogo kwenye mji mkuu wa nchi yetu kimekuwa
kikivuna matunda ya serikali wakati watu wakibeba gharama. Washington
iliendelea kuneemeka lakini watu hawakupata mgao wa utajiri wake. Wanasiasa
walifaidika lakini kazi ziliondoka na viwanda vikafungwa. Mfumo wa Waanzilishi
(The Establishments) ulijilinda na siyo kuwalinda wananchi wa nchi yetu.
Ushindi (wa Waanzilishi) haukuwa ushindi wenu. Mafanikio yao hayakuwahi kuwa
mafanikio yenu. Na wakati walikuwa wakisheherekea kwenye mji mkuu wa nchi yetu,
familia zinazohangaika nchi nzima hazikuwa na cha kusheherekea. (MAKOFI)
Mabadiliko yote hayo yanaanzia hapa na yanaanza sasa hivi kwa sababu
wakati huu ni wakati wenu na ni wakati unaomilikiwa na nyinyi. (MAKOFI)
TRUMP: Wakati huu unamilikiwa na kila mmoja aliyekusanyika hapa leo
na kila mmoja anayetufuatilia akiwa sehemu yoyote hapa Marekani. Hii ni siku
yenu. Hii ni sherehe yenu. Na hii, Marekani, ni nchi yenu. (MAKOFI).
Cha msingi siyo chama gani kinaongoza serikali yetu, cha msingi ni
ikiwa serikali yetu inadhibitiwa na nyinyi, watu. (MAKOFI).
Tarehe 20 Januari 2017 itakumbukwa kama siku ambayo watu (Wa
Marekani) walikuwa watawala wa taifa hili tena. (MAKOFI).
Wanaume na Wanawake wa nchi yetu hawatasahaulika tena. (MAKOFI).
Kila mmoja anawasikiliza hivi sasa. Mmekuja kwa wingi mno kwa makumi
na mamilioni kuwa sehemu ya vuguvugu, mfano ambao dunia haikuwahi kuuona kabla.
(MAKOFI).
Katikati ya vuguvugu hili kuna ahadi muhimu, kwamba taifa lipo kwa
ajili ya kuwatumikia raia wake. Wamarekani wanahitaji shule bora kwa ajili ya
watoto wao, maji salama kwa ajili ya familia zao, kazi nzuri kwa ajili yao.
Haya ni mahitaji halali na ya msingi ya watu sahihi na jamii sahihi.
Lakini sehemu kubwa ya watu wetu, wanakumbana na halisia tofauti:
akina mama na watoto wameshikiliwa na umasikini ndani ya miji yetu; viwanda
vilivyochakaa vimetapakaa kama makaburi kila kona ya nchi yetu; elimu yetu
inatolewa kwa wenye pesa, jambo linaloacha wanafunzi wetu wadogo na wazuri
wakinyimwa maarifa; na uhalifu na makundi ya kihalifu na madawa ya kulevya
ambavyo vimeshachukua maisha ya watu wengi na kuiondolea nchi yetu nguvu kazi
muhimu. Mabalaa hayo kwa Wamarekani yanasimamishwa mahali hapa na yanasimama
sasa hivi. (MAKOFI)
Sisi ni taifa moja na maumivu yao ni maumivu yetu. Ndoto zao ni
ndoto zetu. Na mafanikio yao yatakuwa mafanikio yetu. Tunashirikishana moyo
mmoja, nyumba moja na matarajio ya aina moja. Kiapo cha Urais nilichokula leo
ni kiapo cha utii kwa Wamarekani wote. (MAKOFI).
Kwa miongo mingi, tumekuwa tukitajirisha viwanda vya nje ya Marekani
kwa gharama za viwanda vya Marekani; tumekuwa tukitoa ruzuku na kuyapa majeshi
ya nchi nyingine, wakati tukiruhusu hali mbaya na ya kusikitisha kwa majeshi
yetu. Tumekuwa tukilinda mipaka ya nchi nyingine na tukikataa kulinda mipaka
yetu wenyewe. (MAKOFI).
Tumekuwa tukitumia trilioni na trilioni za dola za Marekani nje ya
nchi yetu wakati miundombinu ya Marekani ikiwa imeanguka, kuharibika na kuoza.
Tumekuwa tukizifanya nchi nyingine kuwa tajiri, wakati utajiri, uimara na
kujiamini kwa nchi yetu kukipungua kwa kila namna.
Kimoja baada ya kingine, viwanda vikafungwa na vikaiacha ardhi yetu,
bila hata kufikiria kuhusu mamilioni na mamilioni ya Wamarekani ambao walikuwa
wanapotezewa kazi. Utajiri wa watu wa kati umeondolewa kutoka kwenye familia
zao na kisha ukagawanywa katika nchi zote duniani. Lakini hayo yamepita. Na
sasa, tunaangalia mbele tu. (MAKOFI).
TRUMP: Tumekusanyika hapa leo kutoa AMRI MPYA itakayosikika katika
kila mji, katika kila mji mkuu wa nchi za Dunia yote, na katika kila sehemu
yenye madaraka. Kuanzia leo kwenda mbele, dira mpya ndiyo itaongoza taifa letu.
Kuanzia leo kwenda mbele, itakuwa ni Marekani kwanza, Marekani kwanza.
(MAKOFI).
Kila maamuzi kuhusu biashara, kuhusu kodi, kuhusu uhamiaji, kuhusu
mambo ya nje yatafanywa kuwanufaisha wafanyakazi wa Marekani na familia za
Marekani. Lazima tulinde mipaka yetu dhidi ya mipango ya nchi nyingine
kutengeneza bidhaa zetu, kuiba makampuni yetu na kuharibu kazi zetu. (MAKOFI).
Kujilinda kutapelekea tupate uimara na mafanikio makubwa.
Nitawapigania kwa kila pumzi iliyomo kwenye mwili wangu. Na kamwe
sitaawangusha. (MAKOFI).
Marekani itaanza kushinda tena, kushinda kuliko ilivyowahi kutokea.
(MAKOFI).
Tutarudisha kazi zetu. Tutarudisha mipaka yetu. Tutarudisha utajiri
wetu. Tutarudisha ndoto zetu. (MAKOFI).
Tutajenga njia mpya, na njia kuu na madaraja na viwanja vya ndege na
mitaro na reli kila mahali katika nchi yetu kuu. Tutawatoa watu wetu kwenye
matatizo na kuwarudisha wafanye kazi, kuijenga upya nchi yetu kwa mikono ya
Wamarekani na Wafanyakazi wa Marekani. (MAKOFI).
Tutafuata kanuni mbili za kawaida; nunua Mmarekani na ajiri
Mmarekani (Nunua bidhaa ya Marekani na toa ajira kwa Raia wa Marekani).
(MAKOFI).
Tutatafuta marafiki na kuonesha nia njema kwa mataifa ya dunia,
lakini tutafanya hivyo kwa kuelewa kwamba ni haki ya kila taifa kuweka mbele
maslahi yake.
Hatutatafuta kuanzisha aina yetu ya maisha kwa taifa lolote, lakini
badala yake kufanya maisha yetu yangare na kuwa mfano. Tutangara ili kila taifa
lifuate mfano wetu. (MAKOFI).
Tutarejesha marafiki wa zamani na kukaribisha wapya na kuunganisha
dunia iliyostaarabika dhidi ya Ugaidi wa Uislamu wa siasa kali, ambao
tutauondoa katika uso wa dunia. (MAKOFI).
Katika kitovu cha siasa zetu kutakuwa na utii mkubwa kwa Marekani,
na kupitia heshima kwa nchi yetu tutavumbua heshima kwa kila mmoja. Unapofungua
moyo wako kwa ajili ya uzalendo, hakutakuwa na nafasi ya kuhujumiwa. (MAKOFI).
Biblia inatueleza namna ilivyo jambo jema pale watu wa Mungu
wanapoishi pamoja katika muunganiko/muungano. Lazima tuseme yaliyomo katika
fikra zetu kwa uwazi, tujadiliane mambo ambayo hatukubaliani kwa uaminifu,
lakini muda wote tukilinda umoja wetu. Wakati Marekani inapoungana, hakuna
awezaye kuisimamisha. (MAKOFI).
Hakupaswi kuwa na woga. Tunalindwa na siku zote tutalindwa.
Tutalindwa na wanaume na wanawake wasio na mfano ambao wako kwenye majeshi yetu
na vyombo vya dola. Na muhimu kuliko yote, tutalindwa na Mungu. (MAKOFI).
TRUMP: Mwisho, lazima tufikiri mbali na kuota ndoto kubwa zaidi.
Marekani, tunafahamu kwamba taifa linaishi ikiwa tu linapambana kupata matokeo
bora. Hatutaendelea kukubali wanasiasa ambao wanaongea bila vitendo, muda wote
wanalalamika, lakini hawajawahi kufanya chochote ili kubadilisha kile
wanachokilalamikia. (MAKOFI)
Muda wa mazungumzo hewa umekwisha. Sasa imefika saa ya vitendo.
(MAKOFI).
Usiruhusu mtu yeyote akwambie kwamba haiwezi kufanyika. Hakuna
changamoto inayoweza kuendana na jitihada na ari ya Marekani. Hatutashindwa.
Nchi yetu itavuka na kushamiri tena.
Tunasimama wakati wa kuzaliwa kwa milennia mpya, tukiwa tayari
kufungua majaribu ya anga, kuifanya dunia kuwa huru dhidi ya majanga ya
magonjwa, na kujenga nishati, viwanda na teknolojia kwa ajili ya kesho. Tunu
mpya za taifa zitakuwa ndani yetu, zitainua maono yetu na kuponya migawanyiko
yetu.
Ni muda wa kukumbuka busara za zamani ambazo wanajeshi wetu hawawezi
kusahau, kwamba hata kama sisi ni weusi au kijivu au weupe, sote tunavuja damu
moja nyekundu ya wazalendo. (MAKOFI).
Sote tunafurahia uhuru wa kipekee na sote tunaipiga saluti, bendera
moja kuu ya Marekani. (MAKOFI).
Na ikiwa mtoto amezaliwa katika eneo la Mjini la Detroit au maeneo
yenye upepo mwingi huko Nebraska, wote wanaangalia anga moja ya usiku, wote
wana ndoto moja, na wote wamepewa pumzi ya maisha na Muumbaji mmoja. (MAKOFI).
Kwa hiyo, kwa Wamarekani wote katika kila mji karibu na mbali, mdogo
na mkubwa, mlima kwa mlima, bahari kwa bahari, sikilizeni maneno haya.
Hamtadharauliwa tena. (MAKOFI).
Sauti zenu, matumaini yenu na ndoto zenu, zitaeleza ukuu wa Marekani
yetu. Na ujasiri wenu na uzuri wenu na mapenzi yenu vitatuongoza siku zote
katika njia tunayopita. (MAKOFI).
Pamoja, tutaifanya Marekani kuwa imara tena. Tutaifanya Marekani
kuwa tajiri tena. Tutaifanya Marekani kujivuna tena. Tutaifanya Marekani kuwa
salama tena. Na ndiyo, pamoja tutaifanya Marekani kuwa Kuu tena. (MAKOFI).
Asanteni sana. Mungu awabariki. Na Mungu aibariki Marekani.
(MAKOFI).
Hotuba hii ya
Rais wa 45 wa Marekani Donald Trump, ambayo aliitoa mara baada ya kuapishwa
rasmi kuwa Rais, Januari 20, 2017. Imetafsiriwa na Julius Mtatiro, ambaye ni Mwenyekiti Taifa wa muda wa Chama cha Wananchi CUF, Mwanasheria
na Mchambuzi wa Masuala ya Siasa na Jamii.
Anapatikana kwa barua pepe: juliusmtatiro@yahoo.com, Whatsup: +255 787
536759.
HOTUBA YA RAIS DONALD TRUMP ILIYOTAFSIRIWA KISWAHILI, ALIITOA BAADA YA KUAPISHWA RASMI KUWA RAIS WA MAREKANI
Reviewed by Unknown
on
09:11
Rating:
No comments: