SERIKALI ONDOA CHANGAMOTO KATIKA MFUMO WA ELIMU NCHINI
Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi, Prof. Joyce Ndalichako. |
Na Mtapa Wilson
Kwa hapa
tulipofikia, serikali inapaswa kupitia upya sera ya elimu nchini na kuisimamia
ili kuhakikisha mfumo wa elimu hauyumbishwi kutokana na kiwango cha utashi wa
mawaziri wanaokabidhiwa sekta hiyo muhimu kuelekea katika uchumi wa viwanda.
Tangu uhuru
wa nchi yetu, mfumo wa elimu umekuwa unaamuliwa na matakwa ya Waziri wa elimu
aliyeko madarakani, hali inayosababisha udhaifu mkubwa katika mfumo wa elimu,
ambao huigharimu Taifa kwa kiasi kikubwa.
Takribani
miongo mitano sasa, sekta ya elimu nchini imekuwa ikifanyiwa mabadiliko badala
ya mapinduzi, ambayo yatasaidia kufikia dira ya maendeleo ya Taifa letu ikiwamo
uchumi wa viwanda na pato la kati ifikapo 2025.
Tukirejea
huko nyuma, Wizara ya Elimu imeongozwa na Mawaziri zaidi ya Watano, ambao kila
mmoja alikuja na namna anavyoona inafaa kuwa.
Hali hii haihitaji kuvumiliwa tena kwani umefika wakati wa kuweka
muafaka wa kitaifa katika mfumo wa elimu nchini, ambao utafuatwa na Mawaziri
wote wanaochaguliwa kuongoza Wizara hiyo.
Baadhi ya mabadiliko
yaliyoshuhudiwa yakitokea katika mfumo wa elimu nchini yamekuwa hayana mchango
wenye tija katika mageuzi ya elimu badala yake yanarudisha nyuma jitihada za
serikali kutaka kuboresha elimu nchini.
Tumeshuhudia
mabadiliko kadha wa kadha mathalani, mdaraja ya ufaulu, mara daraja la tano,
mara mfumo wa GPA, mara wanafunzi wa kidato cha nne kujiunga na chuo kikuu,
hali inayopingana na miongozo ya udahili wa wanafunzi katika ngazi ya elimu ya
juu nchini.
Upitiaji
upya wa sera pamoja na kuweka sheria mpya ya elimu utasaidia kuboresha kiwango
cha elimu nchini, jambo ambalo linaweza kufanikisha hata kuleta maendeleo ya
Taifa kwa kutekeleza dira ya uchumi wa kipato cha kati na viwanda.
Kumekuwapo
na changamoto kubwa ya sheria za elimu nchini ambazo zimekuwa hazirandani na
sera ya elimu, hali inayosababisha kubadilika kwa sera za elimu kutokana na
viongozi wanaoingia kuongoza na kutoka katika sekta ya elimu nchini kwa nyakati
tofauti.
Endapo
kutakuwa na sera ya elimu inayorandana na sheria ya elimu itasaidia kutekeleza
dira ya maendeleo ya elimu nchini bila kujali kiongozi au mtu yeyote ambaye
anaingia kuongoza sekta ya elimu bila kuathiri lengo la sera iliyopo.
Taifa letu
limechukua muda mrefu sana bila kupitia upya sera na sheria ya elimu
nchini. Sheria ya elimu iliyopo sasa
iliandikwa upya mwaka 1978 na kufanyiwa marekebisho mwaka 1995.
Mwaka huo
huo ndio kuliundwa sera ya elimu ambayo ilikuwa inafuata sheria ya elimu ya
mwaka 1978. Lakini tangu mwaka huo, sheria ya elimu haijapitiwa tena ili kuweka
mipaka ya mabadiliko ya elimu, ambayo inazingatia dira ya maendeleo ya Taifa
ikiwemo kukua kwa uchumi.
Watumishi wa
sekta ya elimu nchini pia wanapaswa kuzingatia hati idhini ya elimu inayotolewa
na serikali, ambayo huwaongoza viongozi, wakuu wa idara, na wakurugenzi na
watumishi wa Wizara ya elimu katika kutekeleza sera ya elimu.
Uzingatiaji
huo utasaidia kuhakikisha kunakuwepo na fursa ya utoaji wa elimu bora katika
ngazi zote za elimu yaani kuanzia elimu ya awali hadi Chuo Kikuu.
Licha ya
udhaifu mkubwa uliopo katika mfumo wa elimu lakini bado kuna changamoto kubwa
ya wanafunzi wa elimu ya juu kumudu kupata elimu hiyo kwakuwa hakuna kanuni
wala kipimo maalumu cha utambuzi wa uwezo wa wanafunzi kujigharamia elimu yao
ya juu, jambo ambalo linafanya wanafunzi wengi kukosa mikopo ya elimu
inayotolewa na serikali kupitia Bodi ya Mikopo (HESLB).
Kutokana na
kukosekana kwa kanuni na kipimo maalumu cha kutoa mikopo kwa wanafunzi wa vyuo
vikuu nchini, kinachofanyika sasa ni ubashiri ambao kwa kiasi kikubwa ‘unawanyonga’
wanafunzi wengi ni watoto wa masikini na yatima ambao hawana mbele wala nyuma
ambao hata kusoma shule za sekondari walifanikiwa kwa kupitisha mabakuli ya
kuomba kwa ndugu jamaa na marafiki.
Mfumo giza
uliopo Bodi ya Mikopo unatoa mianya ya rushwa katika upatikanaji wa mikopo,
hali ambayo pia inachangia madhara makubwa ya kuendelea kuwa na tabaka la
wasomi (wanomudu kujisomesha) na wajinga (wanaoshindwa kumudu kujisomesha) kwa
kukosa haki yao ya msingi ya kupata elimu.
Serikali ina
wajibu wa kubeba jukumu la kuwasomesha bure wanafunzi wote kuanzia shule ya
msingi hadi vyuo vikuu ili kutengeneza Taifa la wasomi wasio na matabaka kati
ya walionacho na wasionacho.
Nchi yetu
sio masikini kiasi cha kushindwa kudhamini elimu ya wananchi wake. Serikali ina uwezo wa kutenga rasilimali
yeyote ambayo mapato yake yote yataelekezwa katika kudhamini elimu nchini.
Haiwezekani
leo mwanafunzi anayesoma bure kuanzia chekechea mpaka kidato cha nne, awe na
uwezo kujigharamia ada ya Chuo Kikuu, ambayo ni wastani Shilingi milioni 1.5
kwa vyuo vya serikali. Na ukiangalia
katika vyuo vya binafsi ada inazidi hapo.
SERIKALI ONDOA CHANGAMOTO KATIKA MFUMO WA ELIMU NCHINI
Reviewed by Unknown
on
11:27
Rating:
No comments: