MIKOA NANE YAFAIDIKA NA MIRADI YA VISIMA VYA KISASA
Na Mwandishi wetu, Dodoma
Ili
kukabiliana na tatizo la uhaba wa maji katika maeneo mbalimbali nchini hususani
vijijini, hali inayosababisha usumbufu kwa watoto wa kike kutembelea umbali
mrefu kutafuta maji, kampuni ya bia ya Serengeti (SBL) imechimba visima 16 vya
kisasa katika mikoa nane ili kuiwezesha jamii kupata maji safi na salama.
Msaada huo
wa visima vya maji unakadiriwa kuwanufaisha takribani Watanzania milioni mbili
katika maeneo hayo kwa kupata maji ya uhakika ikiwa ni sehemu ya mchango wa
kijamii (social corporate responsibility) wa kampuni hiyo.
Akizungumza na
waandishi wa habari leo mjini Dodoma, Mkurugenzi wa Uhusiano wa SBL, John
Wanyancha, alisema kwamba msaada huo umejikita katika kupunguza uhaba wa maji
katika maeneo ambayo kwa muda mrefu yamekuwa yakitaabika kutokana na uhaba
huduma hiyo muhimu.
“SBL ina
sera iliyojikita katika ustawi wa jamii yetu ambapo maji ni moja ya maeneo
ambayo ni kipaumbele chetu na sera yetu imefafanua pia malengo yake ya kutoa
msaada kwa jamii,” alisema.
Aidha Wanyancha
alisema kuwa kwa kutoa huduma ya maji ya uhakika katika jamii inawawezesha
wananchi kupata fursa zaidi ya kutumia muda mwingi kujikita katika shughuli za
uzalishaji badala ya kupoteza muda kutafuta maji katika umbali mrefu.
Mikoa ambayo
SBL imechimba visima hivyo ni Iringa, Dar es Salaam, Pwani, Kilimanjaro,
Mwanza, Ruvuma, Tanga na Dodoma.
Mpango
wa hisani ya kusaidia jamii wa SBL kupitia program yake ya Maji kwa Uhai, kwa mwaka 2017 umelenga kuanzisha miradi ya maji zaidi katika
maeneo ya Ngare Nairobi wilaya ya Siha (Kilimanjaro), Chang’ombe B wilayani Temeke (Dar es
Salaam), Karatu na Likamba mkoani Arusha ambapo watu zaidi ya 300,000 watanufaika
na miradi hiyo.
MIKOA NANE YAFAIDIKA NA MIRADI YA VISIMA VYA KISASA
Reviewed by Unknown
on
15:11
Rating:
No comments: