UTT AMIS YAWAFUNDA WANAFUNZI WA ELIMU YA JUU KUWEKA AKIBA


Ofisa Mafunzo, Masoko na Uhusiano wa UTT AMIS, Waziri Ramadhani, akigawa vipeperushi kwa wanafunzi wa Shule Kuu ya Uandishi wa Habari na Mawasiliano ya Umma (SJMC) iliyoko chini ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), wakati wa semina inayohusu umuhimu wa kuwekeza katika mifuko ya dhamana kwa wanafunzi wa elimu ya juu, wahadhiri na watumishi wengine kwa ujumla. (Picha na Asia Mbwana)

Mary Mafuru na Doreen Mafole

Taasisi ya UTT AMIS iliyochini ya Wizara ya Fedha kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Uandishi wa Habari (SJMC) na D3 Promotions and Communication Co. Ltd imeendesha semina kwa wanafunzi wa SJMC juu ya umuhimu wa kujiwekea akiba na kuwekeza katika masoko ya mitaji.

Semina hiyo iliyofanyika leo katika Shule Kuu ya Uandishi wa Habari na Mawasiliano ya umma (SJMC) na kuhudhuriwa na wanafunzi wa mwaka wa kwanza, pili na tatu wanaosomea fani za Uandishi wa Habari, Mawasiliano ya Umma na Uhusiano wa Umma.

Akizungumza katika semina hiyo Afisa Mafunzo, Masoko na Uhusiano wa UTT AMIS, Waziri Ramadhani, amesema kuwa semina hiyo inalenga kuwajengea wanafunzi nidhamu ya fedha na umuhimu wa kuweka akiba kwa ajili ya kuwawezesha kufikia malengo yao ya kiuchumi.

“Watu wengi huwekeza fedha zao katika mabenki kwa sababu za kiusalama na si kwa faida.  Na kama kuna faida basi inakuwa ni kiasi kidogo sana.  Lakini uwekezaji katika UTT inamuhakikishia mteja wake usalama na faida ambayo inakuwa ni kubwa kulingana na kile alkichokiwekeza.  UTT AMIS inakupa fursa ya kuwekeza kwa akiba ambayo inakuwa,” amesema Ramadhani.

Amesema kuwa kuwekeza kupitia UTT AMIS kuna faida kubwa ikiwemo ikiwemo dhamana ya uwekezaji kuwa kwa UTT na mtu anayewekeza kwa kipande anaweza kuchukua fedha yake wakati wowote.

Amewashauri wanafunzi kufungua akaunti za vikundi kupitia mfuko wa umoja ama ya mtu mmoja mmoja.

“Wanaowekeza UTT wanakatwa asilimia moja pale mteja anapoamua kuuza vipande ambayo inaingia kwenye gharama za uongozi,” amesema Ramadhani.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa D3 Promotions Mbwana Mnose amesema “Tumeamua kuitisha semina hii kwa dhumuni la kutoa elimu juu ya umuhimu wa kuwekeza katika mfuko huu ili kuwapa ujasiri wanafunzi kujiandaa kuwa na mitaji yao baada ya masomo.  Hii haifanyiki kwa chuo hiki peke yake bali elimu hii itakuwa ikitolewa kwa wanafunzi wa vyuo mbalimbali hapa nchini ambavyo tutakuwa tunavitembelea kutoa elimu hii,”

Mhadhiri wa Chuo cha SJMC, Edgar Ngelela, amesema kuwa wanafunzi wanatakiwa kuwa na maono ya baadae ya kuwawezesha kuona fursa za kujipatia kipato tofauti na kutegemea kuajiriwa.

“Mifuko kama hii ndiyo inayowawezesha vijana wenye nia ya kupiga hatua kiuchumi kuwa na mahala pa kuanzia.  Hatuwafundishi ili mkihitimu muwe na mawazo ya kwenda kuajiriwa bali mbuni mbinu za kijiingizia kipato,” amesema Ngelela.

Nae Muhammed Likusi, ambaye ni moja kati wanafunzi waliohudhuria semina hiyo, amesema kuwa amenufaika vya kutosha kutokana na semina hiyo ambapo amefahamu maana ya UTT AMIS kazi zake na faida zake hususani katika uwekezaji na ameshauri kuwa ni vyema wanafunzi kuichukua elimu hiyo waliopatiwa na kuizingatia kwa mantiki ya kuwekeza kwa malengo yenye faida.


UTT AMIS YAWAFUNDA WANAFUNZI WA ELIMU YA JUU KUWEKA AKIBA UTT AMIS YAWAFUNDA WANAFUNZI WA ELIMU YA JUU KUWEKA AKIBA Reviewed by Unknown on 19:43 Rating: 5

No comments:

Theme images by merrymoonmary. Powered by Blogger.