WADAU WATAKIWA KUWEKEZA KATIKA RIADHA
Na Mtapa Wilson
Serikali
imesema kuwa uwekezaji mkubwa wa wadau katika tasnia ya michezo utasaidia kukuza
na kuboresha hali ya michezo nchini, jambo ambalo linaweza kurudisha heshima na
utukufu wa michezo mbalimbali katika Taifa letu ikiwemo mchezo wa riadha.
Akizungumza
mbele ya waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam, wakati wa hafla ya
kumpongeza mshindi wa mbio za Standard Chartered Mumbai Marathon, zilizofanyika
nchini India, January 15 mwaka huu, Alphonce Simbu kutoka Tanzania, Waziri wa
Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye, alisema kuwa kwa muda mrefu
sana Taifa limekuwa nyuma katika medani za michezo ya kitaifa na kimataifa
kutokana na uwekezaji duni wa wadau katika michezo.
“Mafanikio
ya Alphonce Simbu, kwa msaada wa Kampuni ya Multichoice Tanzania ni mfano mzuri
kwamba kumbe tukiwekeza inawezekana. Kwa
muda mrefu Tanzania tumekuwa na maneno mengi sana na tabia ya kunyoosheana
vidole sana. Lakini kumbe ni uamuzi wa
kuwekeza tu.
Multichoice
Tanzania imewekeza kwa Simbu kwa muda usiozidi hata mwaka mmoja na matokeo yake
tumeyaona. Kupitia hadhara hii
ninawaomba wadau wa sekta binafsi kushirikiana serikali kuwekeza katika
michezo, ambayo imekuwa na mvuto kwa watu, ili kutengeneza fursa ya kutangaza
vivutio vyetu vya utalii lakini pia kuendeleza michezo nchini,” alisema Waziri
Nape.
Kwa upande
wake Simbu alisema kuwa amefarijika sana kuona mwitikio mkubwa wa Watanzania
baada ya kuibuka mshindi mashindano hayo ya mbio, ambayo yalishirikisha
wanariadha mbalimbali kutoka Mataifa yenye uzoefu na sifa za kujinyakulia
ushindi katika mashindano ya kimataifa kama vile Kenya na Ethiopia.
“……mtaona
kwenye 10 bora, kulikuwa na Wakenya 7, Waethiopia 2 na Mtanzania nilikuwa peke
yang tu. Hii inaleta ugumu sana kwenye mashindano
tofauti na mkiwa wengi kwakuwa mnaweza kusaidiana mbinu ilimradi mwishoni
ashinde mtu wa timu yenu.
Lakini pia
nimefarika sana kuona watu wengi sana wakifuatilia maendeleo yangu ikiwemo
serikali yangu ambayo ilinitumia pongezi dakika chache baada ya ushindi wangu
kupitia Waziri wa Michezo. Hii
inaonyesha dhahiri kuwa hata yeye mwenyewe Waziri alikuwa akifuatilia kwa
karibu sana mashindano hayo,” alisema Simbu.
Nae Kaimu
Mkurugenzi wa Multichoice Tanzania, Ronald Shelukindo, alisema kuwa Multichoice
Tanzania itaendelea kumdhamini Simbu, na kwamba wanatarajia kuwa atafanya vyema
kwenye michuano ijayo ya London Marathon, Aprili, mwaka huu na ile ya Dunia
itakayofanyika Agosti, mwaka huu.
“Tunaendelea
kumdhamini Simbu kwa kushirikiana na Meneja wake na kocha wake pamoja na Mwalimu
wake ili kuhakikisha kuwa anajinoa vizuri kwa ajili ya mashindano yanayomkabili
mbeleni.
Tunataka
Simbu awe chachu na hamasa kwa vijana wanochipukia katika mchezo wa riadha
nchini. Tunamuunga mkono ili aendelee
kushinda na chipukizi wengine waone kweli inawezekana mtu kushinda na wala siyo
kubahatisha,” alisema.
WADAU WATAKIWA KUWEKEZA KATIKA RIADHA
Reviewed by Unknown
on
10:32
Rating:
No comments: