SPIKA WA BUNGE ATANGAZA KUJIUZULU KWA WAZIRI WA MAGUFULI
Na Mwandishi Wetu, Dodoma
Ikiwa
ni siku moja tu imepita tangu Rais John Magufuli kuwaapisha Mabalozi sita
watakaoiwakilisha Tanzania katika nchi mbalimbali, Spika wa Bunge la Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Job Ndugai, ametangaza kupokea barua ya kujiuzulu Ubunge,
Dk. Abdallah Possi.
Kwa mujibu
wa taarifa kwa umma iliyotolewa leo na Kitengo cha Habari, Elimu na
Mawasiliano, Ofisi ya Bunge inasema kwamba Dk. Possi aliwasilisha barua yake ya
kujiuzulu kwa Spika Ndugai jana Januari 20, mwaka huu, mara baada ya kuteuliwa
kuwa Balozi, ambapo atapangiwa baadae nchi ambayo atakwenda kuiwakilisha.
“Spika
Ndugai anapenda kuwataarifu Wabunge wote na wananchi kwa ujumla kuwa jana
tarehe 20 Januari, 2017, amepokea barua ya kujiuzulu Ubunge iliyowasilishwa
kwake na Dk. Abdallah Possi, aliyeteuliwa kuwa Balozi katika kituo
atakachopangiwa hapo baadae,” ilisema taarifa hiyo.
Taarifa
hiyo iliongeza kuwa kufuatia barua hiyo ya kujiuzulu ubunge wa Dk. Possi,
iliyozingatia masharti ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977,
ibara ya 67 (1) (g) ikisomwa pamoja na ibara ya 149 (1) (d), Spika Ndugai amemwandikia
barua Rais Magufuli kuwa hivi sasa Wabunge wa kuteuliwa na Rais waliopo Bungeni
ni saba na hivyo nafasi zilizo wazi ni tatu baada ya Dk. Possi kujiuzulu.
Wabunge
waliokwisha kuteuliwa mpaka sasa ni Naibu Spika, Dk. Tulia Ackson, Waziri wa
Elimu, Prof. Joyce Ndalichako, Waziri wa Fedha, Dk Philip Mpango, Naibu Waziri
wa Fedha, Dk. Ashantu Kijaji, Waziri wa Ujenzi, Prof. Makame Mbarawa, Mhadhiri
wa Sheria kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) Prof. Palamagamba Kabudi
na aliyekuwa Mkuu wa Msafara wa Kampeni za Chama cha Mapinduzi (CCM) wakati wa
uchaguzi mkuu mwaka 2015, El Hadji Abdallah Bulembo.
Dk. Possi aliteuliwa na Rais Magufuli kuwa Mbunge, ambapo baadae aliteuliwa tena kuwa Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Walemavu.
SPIKA WA BUNGE ATANGAZA KUJIUZULU KWA WAZIRI WA MAGUFULI
Reviewed by Unknown
on
14:26
Rating:
No comments: