FATMA MAGHIMBI, KIONGOZI WA KWANZA WA KAMBI RASMI YA UPINZANI NA MUASISI WA CUF ALIYEREJEA CCM
Na Mtapa Wilson
Unapozungumzia waasisi wa vyama vya upinzani nchini
huwezi kuacha kumtaja Fatma Maghimbi akiwa ni miongoni mwa wanawake wa kwanza
kuingia katika ulingo wa siasa hususani siasa za vyama vya upinzani nchini
ukiachilia mbali Elizabeth Kasembe na Ania Chaulembo.
Maghimbi aliingia katika siasa mwaka 1992 mara baada
ya kuwa amehudumu vyema katika nafasi yake ya ujumbe wa sekretarieti katika
tume ya maoni ya katiba chini ya aliyekuwa Jaji Mkuu wa Tanzania, Francis
Nyalali ambapo maoni asilimia 20 ya watanzania walipendekeza Tanzania kuwa na
mfumo wa vyama vingi na asilimia 80 ya watanzania walipendekeza Tanzania ibaki
katika mfumo wa chama kimoja.
Licha ya matokeo hayo ya maoni ya yaliyokusanya na
tume ya Nyalali, ili kuinua kutanua zaidi wigo wa maendelo ya kidemokrasia
nchini ilishauriwa ni bora Tanzania iingie katika mfumo wa vyama vingi
(Multipartism) ambao utaleta changamoto za kiuongozi badala mfumo wa chama
kimoja ambacho hakiruhusu mawazo mbadala katika kufikia maendeleo yenye tija
kwa wananchi wa kawaida.
Mara baada ya mfumo wa vyama vingi kuwa umeridhiwa
ndipo vyama vingi vya upinzani viliundwa ikiwemo chama cha wanchi Cuf ambacho
kilikuwa kikiongozwa na Mwenyekiti wake wakati huo James Mapalala kutoka
Tanzania bara na katibu wake akiwa ni Shaban Khamis Mloo kutoka Zanzibar,
wakati huo Maalim Seif Sharif Hamad akiwa Makamu Mwenyekiti wa Cuf.
Maghimbi alihamasika zaidi kujiunga na chama cha wananchi
mara baada ya kushawishiwa na katibu wa chama hicho ambae ni marehemu kwa sasa,
Shaban Mloo ambapo aliamua kuachana na kazi yake katika Chuo Kikuu cha Dar es
Salaam (UDSM).
Akiwa tayari ameshaingia katika siasa alikumbana na
changamoto mbalimbali ikiwemo kukumbana na pingamizi za mara kwa mara kutoka
kwa serikali na wananchi kwa ujumla ambao walikuwa na mtazamo hasi dhidi ya
vyama vya upinzani.
Muda mwingine Maghimbi aliratibu mikutano ya kisiasa
lakini mwisho wa siku kulikuwa na idadi ndogo ya wahudhuliaji jambo ambalo lilikuwa
linakatisha tamaa lakini kamwe halikumkatisha tamaa katika harakati zake za
mageuzi nchini.
Kutokana na harakati nyingi alizozifanya katika maeneo
mbalimbali nchini, mwaka 1995 ulifanyika uchaguzi wa kwanza chini ya mfumo wa
vyama vingi ambapo aligombea na kuibuka mshindi katika nafasi ya ubunge wa jimbo
la Chakechake lililopo mkoa wa Pemba Kusini baada ya kumbwaga aliyekuwa mgombea
wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Ramadhan Khamis Feruzi.
Kutokana na idadi kadhaa ya wabunge wa upinzani
kuingia bungeni baada ya uchaguzi wa mwaka 1995, chama cha wananchi Cuf
kilifanikiwa kuunda kambi rasmi ya upinzani bungeni ambapo Maghimbi alikuwa
Kiongozi Mkuu wa kambi hiyo jambo lililomfanya kuweka rekodi kubwa mbili. Kwanza, Maghimbi aliweka rekodi yakuwa
Kiongozi Mkuu wa kwanza wa kambi rasmi ya upinzani bungeni tangu kuanzishwa kwa
mfumo wa vyama vingi.
Rekodi ya pili aliyoweka Maghimbi ni kuwa mwanamke wa
kwanza kushika wadhifa mkubwa (Kiongozi Mkuu wa kambi rasmi ya upinzani
bungeni) tangu mfumo wa vyama vingi ulipoanza mwaka 1992.
Mara nyingi Maghimbi alionekana jasiri asiyetetereka
wakati wote wa kuwasilisha hotuba yake kama Kiongozi Mkuu wa Kambi rasmi ya
upinzani kwani hoja zake zilionekana kuwa na mashiko kutokana na utamaduni wa
kufanya tafiti mbalimbali kabla ya kuwasilisha hotuba yake bungeni.
Licha ya kuwa Maghimbi alikuwa mwanamke, uwezo wake wa
kujenga hoja katika hotuba zake ulifanya hotuba zake kuwagusa wengi kutokana na
taarifa muhimu ambazo alikuwa akizitoa kwa umakini wa hali ya juu.
Kuna wakati hali ya upinzani ilikuwa kali bungeni
kiasi cha wabunge wa chama tawala kuamua kumzomea wakati akiwasilisha hotuba
yake. Lakini bado alisimama kidete
kutetea kile alichokiamini kwa niaba ya kambi yake rasmi ya upinzani bungeni
ambayo ilikuwa inaundwa kwa kiasi kikubwa na chama cha wananchi Cuf.
Ilipofika katika uchaguzi wa mwaka 2000, Maghimbi
alianguka katika nafasi yake ubunge jimboni mwake kutokana na kile kilichoitwa
mbinu chafu za kisiasa za Chama cha Mapinduzi (CCM). Alikaa nje ya bunge kwa kipindi cha miaka
mitano ambapo mwaka 2005 alirejea tena kugombea kiti chake cha ubunge katika
jimbo lake la Chakechake na kuibuka mshindi tena kwa mara nyingine.
Safari hii aliporejea bungeni ateuliwa na kambi rasmi
ya upinzani kuwa Waziri kivuli wa Katiba, Sheria na Utawala bora (kwa wakati
huo) ambapo alisimamia hoja kuu tatu katika nafasi yake. Kwanza, alishinikiza serikali kufanya
mabadiliko ya katiba.
Pili, Maghimbi aliwasilisha hoja bungeni ambayo
ilikuwa ikiishinikiza serikali kufanya mabadiliko ya katiba yatakayoruhusu
kuwepo kwa mgombea binafsi.
Vivile hoja ya tatu ya Maghimbi ilikuwa ni uanzishaji
wa mahakama ya kadhi. Hii ilikuwa ni moja ya hoja ambazo alizinadi sana
wakati akiwa Waziri kivuli wa Katiba kwa kipindi hicho ili kutoa mwanya kwa
waumini wa dini ya kiislamu kudai haki zao katika misingi ya dini yao.
Mwaka 2010, ikiwa ni kipindi cha uchaguzi wa awamu ya
pili ya uongozi wa Rais Jakaya Mrisho Kikwete, Maghimbi alishindwa kutetea
nafasi yake ya ubunge katika hatua ya kura za maoni dhidi ya mgombea mwezie
ndani ya chama, Haji Mussa Kombo. Mwaka
huo huo aliondoka chama cha wananchi Cuf na kuchukua kadi ya Chama cha
Mapinduzi.
Wasifu
wa Fatma Maghimbi
Fatma Kitwana Msalem ni mzaliwa wa Chakechake, mkoa wa
Pembe kusini, visiwani Zanzibar.
Alizaliwa Desemba 10, 1946. Ni
mtoto wa mwisho kati ya watoto nane waliozaliwa na Mzee Kitwana Msalem. Alipata jina la Fatma Maghimbi baada ya
kuolewa na muwewe anayeitwa Mzee Mussa Maghimbi.
Alisoma elimu yake ya msingi katika shule ya msingi
Madungu iliyoko Chakechake kuanzia mwaka 1952 mpaka 1958. Akiwa darasa la sita alihamishiwa katika
shule ya kikatoliki iliyokuwa ikifahamika kama ‘St. Joseph Convent Primary
School’ iliyoko eneo la Wete ambapo alihitimu darasa la nane mwaka 1959.
Mwaka 1960, Maghimbi alijiunga na shule ya sekondari
Sayyida Maduka iliyoko Unguja, mkoa wa Mjini Magharibi na kuhitimu kidato cha
nne mwaka 1963. Wakati akiwa katika
harakati za kujiunga na masomo ya kidato cha tano na sita ndipo Mapinduzi ya
Zanzibar, hali iliyomfanya Maghimbi ashindwe kuendelea tena masomo yake.
Kutokana na mapinduzi ya Zanzibar ya 1964, ambayo yalisababisha
wazungu, wahindi na magoa waliokuwa wakifanyakazi katika ofisi za serikali
kuacha kazi. Huu ulikuwa mwanzo wa serikali
ya Mapinduzi kuchukua baadhi ya wananchi wa Zanzibar na kuja kuwasomesha bara
katika kozi maalumu za maofisini ili wakafanye kazi katika nafasi zilizokuwa
zimeachwa wazi.
Katika mpango huo, Maghimbi nae alichukuliwa kuja
kusoma kozi ya ukatibu mukhtasi (Secretarial Course) katika chuo cha ufundi Dar
es Salaam (D.I.T kwa sasa) ambapo baadae alirejea visiwani Zanzibar na kwenda
kuwa Katibu Mkuu wa Rais Abeid Amani Karume.
Hii nayo inamuweka katika rekodi ya kuwa Katibu Mkuu wa kwanza wa Rais
wa kwanza wa Zanzibar.
Baada ya kuhudumu kwa muda miaka mitatu, mwaka 1968
Maghimbi aliolewa bara na Mzee Mussa Maghimbi ambaye alikuwa ni Mwalimu katika
shule ya vipaji maalumu Kibaha iliyoko mkoa wa Pwani.
Hali hii ilimlazimu Maghimbi kuondoka Zanzibar kuja
kuishi bara na mumewe ambapo yeye alihudumu tena kama Katibu katika ofisi ya
Mganga mkuu wa kituo cha elimu Kibaha ambacho kilikuwa chini ya mradi
unaoendesha shule ya sekondari Kibaha, Kituo cha afya kibaha na Taasisi ya
kilimo Kibaha.
Mwaka 1971, Maghimbi alihama kutoka Kibaha mpaka Chuo
Kikuu cha Dar es Salaam ambapo aliajiriwa kama Katibu wa chuo. Alihudumu hapo
kwa takribani miaka kumi na tano ambapo alipata fursa ya kujiendeleza kielimu
kwa masomo ya kidato cha tano na sita kupitia mpango maalumu wa Chuo Kikuu
kuwandeleza wafanyakazi wake kielimu.
Kutokana na juhudi kubwa katika masomo yake ya
kujiendeleza aliweza kufaulu vizuri mitihani yake mwisho. Mwaka 1989 alijiunga na masomo ya juu kwa
ngazi ya chuo kikuu akisomea sheria mpaka alipohitimu mwaka 1992.
Ikiwa ni mpango wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam
kubadilishana maarifa kwa kusomesha wafanyakazi wake katika vyuo vingine
duniani, mwaka 1992, Maghimbi alipata ufadhili wa kwenda kusoma shahada ya
uzamili katika Chuo Kikuu cha Warwick kilichopo Birmingham nchini Uingereza
ambapo alihitimu mwaka 1993.
Aliporejea nchini aliendelea kufanya kazi Chuo Kikuu
cha Dar es Salaam (UDSM) akiwa kama Afisa utawala wa sheria ambapo baadae alijiunga
moja kwa moja na siasa za upinzani baada ya kuombwa na viongozi wa chama cha
wananchi Cuf wakti huo.
Maghimbi ana watoto watatu ambapo kati yao wawili ni
wakike na mmoja ni wa kiume. Mtoto wake
wa kwanza ni wa kiume ambae ni daktari wa binadamu, wa pili ni mtoto wa kike
ambae ni Meneja wa huduma kwa wateja katika mfuko wa pensheni wa PSPSF, na
mtoto wake wa mwisho ni Jaji wa Mahakama kuu kanda ya Arusha.
FATMA MAGHIMBI, KIONGOZI WA KWANZA WA KAMBI RASMI YA UPINZANI NA MUASISI WA CUF ALIYEREJEA CCM
Reviewed by Unknown
on
07:25
Rating:
No comments: