RAIS YAHYA JAMMEH WA GAMBIA AKUBALI KUACHIA MADARAKA

Aliyekuwa Rais wa Gambia, El Hadji Yahya Jammeh.
Banjul-Gambia

Hatimae mzizi wa fitna umekatwa nchini Gambia.  Hii ni mara baada ya kiongozi mkuu wa nchi hiyo aliyekaa madarakani kwa takribani miaka 22, Yahya Jammeh kusema kuwa ataondoka madarakani.

Awali Jammeh alikubali kushindwa na mpinzani wake Adama Barrow, katika uchaguzi mkuu uliofanyika nchini humo Desemba mosi mwaka jana, lakini baadae aligeuka na kung’ang’ania kusalia madarakani kwa madai kuwa, uchaguzi huo ulikuwa batili kwakuwa uligubikwa na kasoro kadhaa.

Akitangaza uamuzi wake huo wa kuachia madaraka kupitia kituo cha runinga, Jammeh amesema kuwa hakuna haja ya tone hata moja la damu kumwagika.

Uamuzi huo umekuja ikiwa ni siku moja tu baada ya kufanya mazungumzo na viongozi wakuu wa nchi za Guinea, Alpha Conde na Mauritania, Mohamed Ould Abde Aziz waliofika nchini Gambia kwa ajili ya kumshawishi Jammeh aachie madaraka kwa amani.

“Nimeamua leo nikiwa na dhamiri njema kuachia uongozi wa Taifa hili kubwa nikiwa na shukrani zisizo na kikomo kwa raia wa Gambia.  Namuahidi Allah na Taifa lote kwamba masuala ambayo yanatukabili kwa sasa yatatatuliwa kwa njia ya amani,” amesema Jammeh.

CHANZO: BBC SWAHILI
RAIS YAHYA JAMMEH WA GAMBIA AKUBALI KUACHIA MADARAKA RAIS YAHYA JAMMEH WA GAMBIA AKUBALI KUACHIA MADARAKA Reviewed by Unknown on 06:36 Rating: 5

No comments:

Theme images by merrymoonmary. Powered by Blogger.