MISAADA YA WAATHRIKA WA MVUA MWAKATA KUJENGA MIUNDOMBINU YA SERIKALI
Na Mtapa Wilson, Kahama
Serikali
imechukua vifaa vya ujenzi vilivyokuwa vimekusanywa kwa ajili ya ujenzi wa
nyumba za waathirika wa vijiji vitatu vya Kata ya Mwakata wilayani Kahama,
mkoani Shinyanga, ambavyo viliathiriwa vibaya na mvua kubwa ya mawe mwanzoni
mwa Machi 2015, na kusababisha vifo vya watu 47 na wengine 112 kujeruhiwa.
Serikali imesema
vifaa hivyo vya ujenzi vitaelekezwa kwenye ujenzi wa miundombinu ya serikali
pamoja na miradi mbalimbali ya maendeleo ya serikali katika vijiji vitatu vya
Magunhumwa, Mwakata yenyewe na kijiji cha Numbi.
Vifaa vya
ujenzi vilivyochukuliwa na serikali kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa kile
ilichokiita miundombinu ya serikali kama vile ujenzi wa shule, nyumba za
walimu, ukarabati wa vyumba vya madarasa, na ujenzi wa ofisi za serikali za
vijiji ni jumla ya tofali za saruji 33,365 na mabati 1,346.
Kwa mujibu wa
Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Fadhili Nkurlu ni kwamba hatua hiyo imekuja kufuatia
kauli ya Rais wa Tanzania, Dk. John Magufuli, aliyoitoa Julai 31, mwaka jana
akiwa kata ya Isaka, Mkoa wa Shinyanga kuwa serikali haitalipa fidia kwa
wananchi waliopatwa na maafa ya mvua iliyobomoa nyumba zao badala yake
itajielekeza kutatua tatizo kubwa la uhaba wa maji.
“Serikali haiwezi
ikajenga Mwakata kama alivyosema Mheshimiwa Rais. Tofali hizi tunazitoa kwa serikali za vijiji
ili izielekeze katika ujenzi wa miundombinu ya serikali pamoja na miradi
mingine ya maendeleo,” amesema Mkuu wa Wilaya huyo.
Akizungumza na Pipa la Habari, Mwenyekiti wa Kijiji cha Magunhumwa, Salum Mohammed, amesema
kuwa wananchi wake, ambao kimsingi ndio waathirika wa maafa yaliyotokea
wamesikitishwa sana hatua hiyo kwakuwa waliamini kuwa serikali inaweza angalau
kuwagawia vifaa hivyo vya ujenzi ili waanze ujenzi wao wenyewe kwa ajili ya
makazi yao.
“Kwakweli wananchi
wamepokea taarifa hii kwa masikitiko. Lakini
haina namna kwakuwa serikali ndiyo imeshasema.
Wananchi wamelalamika sana kwasababu tayari kuna nyumba tatu ambazo
zilikuwa zimeshajengwa na Kampuni ya Madini ya ACACIA na nyumba mbili ambazo
zilijengwa na serikali kama mfano na kugawiwa kwa wananchi. Hivyo, wananchi waliosalia waliamini kabisa
nyumba zingine zitajengwa, ikizingatiwa vifaa vya ujenzi kama saruji na mabati vilikuwa vimekwishakutolewa na wahisani mbalimbali,” amesema.
Machi 12,
2015, Rais wa Tanzania, Dk. Jakaya Kikwete (wakati huo), alitembelea Mwakata na
kuahidi kuwa serikali itahahakikisha makazi ya waathirika yanarejea katika hali
ya kawaida kwa kuwajengea nyumba, ambapo aliahidi kuwa serikali itatoa shilingi
bilioni 2 na aliagiza Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) kujenga nyumba hizo bila
kupitia mkandarasi yeyote kama ulivyo ujenzi wa serikali na kwakuwa ujenzi wa
jeshi unaisha kwa wakati mfupi na hakuna uchakachuaji.
MISAADA YA WAATHRIKA WA MVUA MWAKATA KUJENGA MIUNDOMBINU YA SERIKALI
Reviewed by Unknown
on
07:49
Rating:
No comments: