TAMWA: MTOTO WA KIKE APEWE ELIMU SIYO KUOZESHWA

Ofisa Kitengo cha Jinsia TAMWA, Godfrida Jola.

Na Mwandishi wetu

Chama cha Waandishi wa habari Wanawake (TAMWA), kimeitaka jamii kuachana na mila potofu zinazomgandamiza mtoto wa kike ikiwemo kumnyima haki yake ya msingi ya kupata elimu kwa kisingizio kuwa mwanamke hapaswi kupata elimu badala yake anapaswa kuolewa kwa shinikizo la wazazi au walezi wao wakiwa katika umri mdogo.

Hayo yamesemwa leo na Ofisa Kitengo cha Jinsia kutoka TAMWA, Godfrida Jola wakati wa mahojiano maalumu na mtandao huu jijini Dar es Salaam na kubainisha kuwa kuna changamoto mbalimbali zinazowakabili watoto wa kike nchini ikiwemo sheria ya ndoa ya mwaka 1971.

Jola amesema kuwa sheria hiyo ya mwaka 1971 haimlindi mtoto kwani inatoa mwanya kwa wazazi au walezi kuwaozesha watoto wao wakiwa na umri wa miaka 15, jambo ambalo inawawia vigumu kupambana na ukatili huo wa kijinsia unaomnyima haki mtoto wa kike.

“Kuna baadhi ya jamii zimekuwa zikiwaozesha watoto wakiwa bado wadogo kabla hata ya kufikia umri wa miaka 18, umri ambao unatambulika kama umri wa kiutu uzima.  Lakini kupitia sheria ya ndoa ya mwaka 1971, watoto wengi wamekuwa wakiozeshwa katika maeneo mbalimbali.  Hii ni changamoto kubwa sana.  Sisi kama TAMWA tunaendelea kuipigia kelele,” amesema Jola.

Jola ameongeza kuwa kuna jamii ambazo zinakabiliwa na umasikini wa kupindukia, hali inayofanya kumtumia mtoto wa kike kama sehemu ya kujipatia utajiri au mali pindi wanapomuozesha.

“Kuna wazazi wanaozesha watoto wao kwa kuona ufahari kuwa watapata mali kama vile ngo’ombe.  Kwa hali hiyo basi, unakuta mzazi anaozesha mwanae bila kuona tatizo.  Suala hili linakuwa gumu kwetu pale tunapoelimisha mtoto anapawa kupata elimu kutokana na kasumba hii ya mtoto wa kike kutumika kama sehemu ya mtaji,”

Aidha Jola ameonya jamii zote zenye mtazamo hasi juu ya ustawi wa mtoto wa kike ikiwemo kutokupatiwa elimu, ambapo kuna baadhi ya maeneo nchini mtoto wa kike anapaswa kupata elimu ya msingi tu, jambo linaloleta changamoto ya usawa wa kijinsia katika masuala ya haki za kijamii kama vile elimu nchini.

“Mwaka 2012 nilifanya utafiti katika Wilaya ya Bariadi, Mkoani Shinyanga ambapo nilifanikiwa kukutana na Afisa elimu ambae alinithibitishia jinsi watoto wa kike wanvyotishwa na wazazi pamoja na walezi wao wakati wanapoenda kufanya mitihani ili wafanye vibaya kwa makusudi kwa lengo la kwenda kuozeshwa watakapoku wameshindwa kufaulu mitihani yao,” amesema

Kwa mujibu wa ripoti ya utafiti uliofanywa na Shirika la Watoto Duniani (UNICEF) mwaka 2015/2016 inasema kuwa takribani asilimia 33 ya watoto wadogo wa kike nchini Tanzania wanaolewa.  Kati ya ndoa 5 zilizopo nchini.  Ndoa 3 kati yake ni ndoa za watoto wadogo.

Sheria ya makosa ya jinai ya mwaka 1998 inaeleza kuwa endapo mtu atashiriki ngono au kuishi na mtoto mwenye umri chini ya miaka 18, hilo ni kosa la ubakaji. Sheria hiyo inatoa hukumu ya miaka 30 jela kwa mtu aliyefanya kosa la ukatili huo kwa mtoto mwenye umri chini ya miaka 18.  Lakini pia sheria inatoa hukumu ya kifungo cha maisha jela endapo mtuhumiwa atabainika kutenda kosa hili la ukatili kwa mtoto mwenye umri chini ya miaka 10.

Takwimu za kitaifa za makosa ya unyanyasaji wa kijinsia kwa mwaka 2012 zinaonyesha kuwa wanawake 5,745 walibakwa.  Kati yao wanawake wenye umri wa miaka 19 na kuendelea walikuwa 5,389 na watoto wenye umri chini ya miaka 18 walikuwa 356.
TAMWA: MTOTO WA KIKE APEWE ELIMU SIYO KUOZESHWA TAMWA: MTOTO WA KIKE APEWE ELIMU SIYO KUOZESHWA Reviewed by Unknown on 19:23 Rating: 5

No comments:

Theme images by merrymoonmary. Powered by Blogger.