RIPOTI KAMILI UVAMIZI WA CLOUDS MEDIA
Tulianza kufanya juhudi za kumpata Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, ambapo kuanzia Machi 20 tulianza kwa utaratibu wa kumpigia simu ili kumsihi kuwa imeundwa kamati, tungependa kukusanya taarifa kutoka kwa wadau mbalimbali akiwemo yeye hakupokea simu.
Tukaamua kumpelekea ujumbe, hakuujibu. Tukaamua kumtafuta kupitia wasaidizi wake, ambapo tukawapata. Wasaidizi wake walitutaka twende pale ofisini kwake na tukafanya hivyo.
Tulifika ofisini kwa Mkuu wa Mkoa Machi 21, saa 11.10 asubuhi na tulikaa mpaka saa 12.30 mchana, tukielezwa kwamba alikuwa na mgeni ofisini kwake, ambaye alikuwa ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Mheshimiwa George Simbachawene.
Sasa ilivyofika saa 12.30 mchana, tukaambiwa kuwa Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa anatuita ofisini kwake, na tukaelezwa tupande kupitia ngazi za kule mbele. Kamati ilipokwenda kupanda ngazi kumbe Mkuu wa Mkoa akapita mlango wa nyuma, akatoka nje, akapanda gari na kuondoka.
Kwahiyo kilichotokea, kamati ilitaka kuondoka lakini mhudumu wa ofisi aliijia kamati na kuiambia kuwa Katibu wa Mkuu wa Mkoa amesema tumsubiri amekwenda pale Machinga Complex kwa muda mfupi na angerudi.
Kamati iliendelea kukaa pale ofisi za Mkuu wa Mkoa mpaka saa tisa kamili, ambapo baadaye mhudumu yule yule alirejea na kutuambia kwamba amepata shughuli nyingine, kwahiyo hatoweza kurejea ofisini kuonana na kamati.
Mkuu wa Mkoa, Paul Makonda, aliwatisha wafanyakazi wa Clouds waliokuwa studio usiku huo kwamba angewafunga jela miezi sita, alipopiga simu kwa Wakuu wa Kituo cha Clouds mbele ya wafanyakazi na kuwahoji sababu za kutokurusha hewani kwa habari yake (Tunaita habari yake kwa sababu alisema ile habari yangu, ambayo imekuja hapa kwanini haikuruka?).
Kwahiyo Mkuu wa Mkoa pia, ilielezwa kuwa alitoa vitisho kuwa angeweza kuwakagua Watangazaji wa kipindi kama wanahusika na dawa za kulevya au kuwabana wadhamini wa kipindi hicho na pengine kuwaingiza katika orodha ya kuuza dawa za kulevya iwapo wangeendelea na msimamo wa kutokurusha kipindi. Hii ni kwa mujibu wa taarifa za uchunguzi tulizozipata kule.
Ikizingatiwa kuwa vijana wengi pale ni wadogo, vilio vilitawala. Kamati imebaini kuwa kutokana na taharuki hiyo ya vitisho vya Mkuu wa Mkoa, hata kipindi cha Shilawadu siku hiyo hakikufungwa, kiliishia hewani. Kwa walioangalia waliona ghafla baada ya zile picha zilizokuwa zinaonyeshwa iliingia taarifa ya habari.
Kamati imebaini kuwa kwa takribani saa moja, ambayo Mkuu wa Mkoa, alikishikilia kituo cha Clouds, alitoa vitisho kwa wafanyakazi waliokuwa zamu.
Alisisitiza kuwa kwa yale yaliyotokea usiku huo yabaki ndani ya ofisi hizo na iwapo yangetolewa nje wangemtambua kuwa yeye ni nani? Na hii ndio maana utaona tukio lilitokea ijumaa pamoja na kwamba Clouds ni kituo ambacho tunajua wana mitandao ya kijamii na vijana pia pale wapo, lakini lilikaa mpaka jumapili wakiogopa kushughulikiwa.
Kamati imebaini kwamba kulikuwepo na uvunjifu wa sheria na uingiliaji wa uhuru wa uhariri wa vyombo vya habari kwa kiwango cha juu kutokana na vitisho na amri alizozitoa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda.
Kifungu cha saba, kifungu kidogo cha kwanza (a), (b), na (c) cha Sheria ya Huduma za Habari ya mwaka 2016, iliyosainiwa na Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Magufuli, Novemba mwaka jana, na kuanza kutumika mwaka huu, kinatoa uhuru kwa vyombo vya habari na wanahabari, kukusanya, kuchakata, kuhariri na kusambaza taarifa na habari.
Kwa mujibu wa ibara ya 18 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, Mheshimiwa Mkuu Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, alipofika kituo cha Clouds alijipa jukumu la kiuhariri kwa kuhoji nani aliyezuia habari yake inayohusu kashfa ya Askofu Gwajima isitangazwe? Wakati hii ni kazi ambayo anapaswa kuifanya Mhariri.
Mbali na Sheria, alichokifanya Mheshimiwa Makonda ni kinyume na kifungu cha 23 cha Azimio la Dar es Salaam, juu ya uhuru wa uhariri na uwajibikaji la mwaka 2011 kinachosema kuwa;
"serikali inapaswa kuondokana na tabia ya kutumia ubabe unaozuia uhuru wa uhariri kama vile vitisho vya polisi, kufungwa jela kwa waandishi wa habari, kunyang'anya na kuharibu vitendea kazi vya habari.
Pale ambapo mawakala wa serikali watapatikana na shutuma za kutenda ukatili dhidi ya wanahabari, uchunguzi makini lazima ufanyike na wahusika washughulikiwe kwa uthabiti na uwazi,"
Pia Sheria ya Mawasiliano ya Kielektroniki na Huduma za Posta namba tatu ya mwaka 2010. Katika kifungu cha 104, kifungu cha pili (c), inazuia chombo chochote cha habari kurusha habari kurusha matangazo, ambayo yameegemea upande mmoja.
Hivyo, kitendo cha Mkuu wa Mkoa, kulazimisha habari ambayo haijahusisha pande zote irushwe, alikuwa akishinikiza kukiukwa kwa sheria za nchi.
Ni kweli kwamba ilikuwa ni kawaida yake kwenda pale Clouds TV. Yeye alikuwa ni mgeni mwenyeji. Kwahiyo ndiyo maana hata walinzi hawakumshaangaa alipofika anaendesha gari mwenyewe. Mfano; Machi 14, mwaka huu, alikaa katika ofisi za Clouds mpaka saa 04.00 alfajiri akishirikiana na baadhi ya wahariri kuandaa taarifa ya mwaka mmoja ya utawala wake akiwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam.
Kilichowashangaza wengi kwa siku hii ya ijumaa, Machi 17, alikuwa hajawahi kufika pale na askari wenye bunduki, waliovaa sare, lakini pia kwa ukali ambao hawakuutarajia.
Wote iliwashangaza mpaka walinzi waliokuwepo pale ndani kwamba alifika na silaha. Na imeelezwa kwamba tangu kuzinduliwa kwa kituo hicho miaka 17 iliyopita hawajahi kushuhudia askari wakiingia studio na bunduki na mgeni yeyote. Hairuhusiwi kuingia studio wakati matangazo yakiendelea bila ridhaa lakini yeye aliingia.
Hakuna aliyepigwa kwa kitako cha bunduki wala kupigwa mtama. Isipokuwa wale waliolia, walilia kwasababu ya vitisho walivyokuwa wanapewa kwamba wajiandae kwenda jela miezi sita bila kupitia mahakamani.
MAONI YA KAMATI ILIYOCHUNGUZA UVAMIZI CLOUDS MEDIA
1. Kamati imebaini kuwa vitendo vya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, vina viashiria vya uvunjifu wa sheria mbalimbali za nchi hususani zinazohusiana na utangazaji na huduma za habari.
2. Kamati imebaini dalili za Mkuu wa Mkoa, kutotambua ukubwa madaraka aliyonayo na kujikuta akiyatumia vibaya katika mazingira yasiyostahili.
3. Kamati imebaini kuwa uongozi wa Clouds unastahili pongezi kwa kusimamia misingi, sheria na maadili ya uandishi wa habari kwa kukataa kuchapisha habari isiyokuwa na mizania (unbalanced story).
MAPENDEKEZO MANNE YA KAMATI ILIYOCHUNGUZA UVAMIZI WA CLOUDS MEDIA
1. Kamati imeomba kwamba Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, awaombe radhi wafanyakazi wa kampuni ya Clouds Media Group na vyombo vya habari kwa ujumla nchini kwa tukio hili la ukiukaji wa usalama na maadili ya uandishi wa habari.
2. Mheshimiwa Waziri Nape Nnauye, katika kulinda masilahi ya tasnia ya habari, ambayo anaiongoza, awasilishe rasmi malalamiko ya tasnia ya habari dhidi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, kwa mamlaka yake ya uteuzi ya Mkuu huyo wa Mkoa, kuomba mamlaka ya uteuzi imchukulie hatua zinazopaswa.
3. Vyombo vya dola vianzishe uchunguzi wa ndani dhidi ya askari walioingia na bunduki katika kituo cha Clouds kwa nia ya kudhibiti matukio ya aina hii siku za usoni kwani ipo hatari ya kujengeka mazoea ya kuvamia vituo vya utangazaji na inaweza kusababisha matatizo makubwa ya kiusalama nchini.
4. Kampuni ya Clouds Media Group ipitie upya miongozo, kanuni, sheria na taratibu zinazoongoza shughuli za utangazaji na kuangalia njia bora ya kuwa na udhibiti wa watu wasiohusika kuzoea kuingia mara kwa mara kufanya kazi za uhariri bila kuwa wanataaluma wa habari au wahusika katika chumba cha habari.
RIPOTI KAMILI UVAMIZI WA CLOUDS MEDIA
Reviewed by Unknown
on
17:53
Rating:
No comments: