MTATIRO AMJIBU LIPUMBA KUHUSU TAMKO LA KUTEUA KATIBU MKUU MPYA NA KUWAFUKUZA WAKURUGENZI WA CUF ZANZIBAR
Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi CUF, Julius Mtatiro. |
Na Julius Mtatiro
Nimeulizwa na watu wengi sana kuhusu tamko la jana la
Lipumba la kuwavua ukurugenzi wakurugenzi wote wa CUF Zanzibar na kumteua Magdalena
Sakaya kuwa Katibu Mkuu.
Nachoweza kuwaeleza ni kuwa; “kichaa akiiba nguo zako,
usikimbizane naye ukiwa hujajisitiri, kavae nguo kwanza”. Wenye akili na
waelewe!
Ukweli ni kuwa Katibu Mkuu wa CUF anachaguliwa na
mkutano mkuu wa CUF, kamwe hawezi kuteuliwa na Mwenyekiti wa CUF (hata kama
Lipumba angelikuwa ndiye mwenyekiti wa CUF kama ilivyokuwa zamani).
Pili, wakurugenzi wa CUF wanateuliwa na Mwenyekiti wa
CUF kwa kushauriana na Makamu Mwenyekiti wa CUF. Mwenyekiti wa CUF alijiuzulu
tokea mwaka 2015 na Mkutano Mkuu wa taifa uliidhinisha kujiuzulu kwake tarehe
21 Agosti 2016, kwa hiyo CUF haina Mwenyekiti kwa sasa. Yupo mhuni mmoja tu
amekalia ofisi na anaishi ofisini kwa kulindwa na dola.
Makamu Mwenyekiti wa CUF alijiuzulu na kujiunga
Chadema kwa maslahi ya kitaifa kwenye uchaguzi mkuu na hajachaguliwa mtu
mwingine kushika wadhifa huo.
Kama kuna mtu anasimama hadharani na kufukuza
wakurugenzi wa CUF Bara au Zanzibar hivi sasa, basi mtu huyo si Mwenyekiti wa
CUF, labda ni msukule wa mwenyekiti wa CUF.
Itoshe tu kusema kuwa Lipumba anatumiwa vibaya sana na kama kuna
wanasiasa wanatumika basi kwa sasa yeye ana PhD ya eneo hilo.
Lakini nataka kuwahakikishia watanzania kuwa katika
CUF tuko imara sana, Kamati ya Utendaji ya Taifa inayotambulika ndani ya chama
na iliyothibitishwa na Baraza Kuu ipo na inakutana kila mara, kwa hiyo kikatiba
huwezi kuwa na Kamati nyingine ya utendaji ya taifa isipokuwa ile
iliyothibitishwa na Baraza Kuu ambalo wajumbe wake huchaguliwa na Mkutano Mkuu.
Baraza Kuu la Uongozi la Taifa la CUF lipo na
linakutana kama kawaida. Bodi ya Wadhamini ya CUF ipo na imefanya maamuzi mengi
hivi karibuni, ikiwa ni pamoja na kuzifunga akaunti zote za CUF ili zisiendelee
kutumiwa na bwana yule kutorosha fedha za chama na kugawana na genge lake na kadhalika.
Kama nilivyowahi kusema huko nyuma na narudia tena
hapa, jeuri yote ya Lipumba ni CCM na serikali yake, hawa ndio wanamuweka
mjini, anatamba, anaita vyombo vya habari, anatangaza madudu yake na kadhalika.
Lakini kitaalamu tumeshamshinda vita ya ndani, bado
ameshikilia tawi moja tu, CCM na vyombo vya dola – nawahakikishia kuwa tawi
hilo litakatika na Lipumba ataanguka kama mzigo na genge la wahuni wake
litatawanyika kama kondoo wasio na mfugaji na CUF imara itasimama kuelekea
2020.
Kwa hiyo msitishwe na matamko ya Lipumba na watu wake,
ni kweli watatusumbua sana, lakini tutawashinda tu, na mahali tutakapowashindia
wanapajua na hawana pa kutokea. Hakuna uongo uliyowahi kuishinda kweli.
Hakuna wasaliti waliowahi kudumu kwa hiyo nawaomba
watanzania tuendelee kumpuuza kama wanachama wa CUF mkoani Tanga walivyompuuza
hivi karibuni alivyojaribu kufanya ziara mkoani humo. Tumkatae kama wabunge na
madiwani wa CUF walivyomkataa. Tumsuse kama wenyeviti wa mitaa wa CUF
walivyomsusa.
Tuendelee kumzodoa kama anavyozodolewa na familia
yake. Let us disown and continue to neglect him untill CCM registers him
officially (tumkatae na kumpuuza mpaka pale atakaposajiliwa na CCM).
MTATIRO AMJIBU LIPUMBA KUHUSU TAMKO LA KUTEUA KATIBU MKUU MPYA NA KUWAFUKUZA WAKURUGENZI WA CUF ZANZIBAR
Reviewed by Unknown
on
15:29
Rating:
No comments: