ALPHONCE LUSAKO, MWANAFUNZI ALIYEFUKUZWA UDSM 'AFUNGUKA'


Alphonce Lusako (katikati) akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani).

Taarifa kwa  Vyombo vya Habari na Watanzania wote dhidi ya sakata endelevu la uonevu juu yangu katika kutimiza ndoto zangu kielimu

Kabla ya kueleza undani wa sakata langu la kufukuzwa kwa mara ya pili Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), ningependa Watanzania wajue kwamba ninaonewa.

Ni takribani miaka sita sasa, napambana kuitafuta haki yangu ya kusoma bila mafanikio.  Nimezunguka nchi hii nikiwaomba viongozi wenye mamlaka na elimu, wanipatie haki yangu ya kusoma bila ya mafanikio.

Kwa mara ya kwanza nilijiunga na UDSM mwaka 2009 na kudahiliwa kusoma Shahada ya Biashara katika Uhasibu (Bcom Account).  Lakini mwaka 2011, mimi na wanafunzi wenzangu kadhaa tulifukuzwa UDSM na kufutwa katika Mfumo wa Elimu nchini.

Sababu kuu ya kufukuzwa kwetu ilikuwa ni kuratibu mgomo wa wanafunzi UDSM uliolenga kupinga kurudishwa kwa wanafunzi wa mwaka wa kwanza waliokwisha kuwasili vyuo vikuu vya umma nchini, kurudishwa nyumbani kwa hoja ya kwamba bajeti haitoshi.
 
Wanafunzi wa UDSM tulihoji uwepo wa mikopo hewa ambayo ilikuwa inaliwa na baadhi ya watendaji wasio waaminifu.

Tuliiomba Serikali, mikopo hewa yote ielekezwe kuwadhamini baadhi ya wanafunzi.  Mnakumbuka, Waziri wa Elimu, Prof. Joyce Ndalichako, kuanzia August 17, 2016, alivitaka vyuo vikuu takribani 31 kati ya 81, kurejesha fedha walizozipokea ambazo ni za wanafunzi hewa. 

Haya yote ni matokeo ya kuhoji kwetu tangu mwaka 2011 (Rejeeni ripoti za Mkaguzi na Mdhibiti wa Fedha za Serikali (CAG) za miaka minne ya fedha ambayo imepita.

Tunamshukuru Mwenyezi Mungu!  Sisi tukatolewa mbuzi wa kafara lakini baada ya siku mbili tu Serikali kupitia Bodi ya Mikopo (HESLB) iliwadhamini mikopo wanafunzi wengi ndani ya vyuo vikuu vya umma nchini, kitakwimu, upande wa  UDSM, wanafunzi zaidi 144 walipewa mikopo.

Ifahamike kwamba, vuguvugu la migomo Vyuo Vikuu nchini, kwa kiasi kikubwa, ni zao la ubidhaishaji (uuzaji) wa sekta ya elimu, ambao ulianza miaka ya 1990 baada ya Serikali kuanzisha Sera ya Uchangiaji wa Elimu ya juu (Cost sharing Policy).  Hii ni sera pekee, iliyoleta matabaka makubwa sasa kati ya walionacho na wasionacho katika mfumo wa elimu nchini.

Kihistoria (Hatua Tulizozichukua)

Tulianza kufanya hatua za ndani ya Chuo.  Tukakata rufaa dhidi ya maamuzi ya kutufukuza na kutufuta katika mfumo wa elimu, kwa kuliomba Baraza la Chuo (UDSM) lirejee maamuzi husika yenye lengo la kupoka haki yetu ya kusoma katika vyuo vya umma nchini. Lakini Baraza la chuo lilikataa maombi yetu.

Tulishitakiwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, katika Mahakama ya Hakimu Mkazi kisutu (Criminal case No. 270 ya 2011), kwa makosa makuu mawili;
Mosi, kufanya mkusanyiko usio halali na pili ilikuwa ni kukaidi amri ya polisi iliyotutaka tutawanyike.

Agosti 30, 2012, tulishinda kesi hii kwa mahakama kutupilia mbali shitaka husika. Tuliporudi Chuoni, wanafunzi takribani 12 kati ya 51 tukabaguliwa bila sababu za msingi na hatukurudishwa.

Baadaye tukaanza njia za kidiplomasia tena.  Tulizunguka nchi hii kwa kila kiongozi mwenye mamlaka na sekta ya elimu, tukiomba huruma yao ya kuturudisha Chuoni tumalizie masomo yetu.

Tuliandika barua kwa Mkurugenzi wa Vyuo vikuu, Waziri wa Elimu, Dk. Shukuru Kawambwa (wakati huo), Waziri Mkuu mstaafu awamu ya nne, Mizengo Pinda, Waziri wa Mambo ya Ndani, Nahodha Vuai (wakati huo) ambaye tulimuomba atusaidie suala letu la kesi mahakamani.

Tuliomba Tume ya Utawala bora na haki za Binadamu iingilie kati, tuliomba Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia kamati maalumu iliyokuwa inaongozwa na Magreth Sitta, kuingilia kati.  Hatua zote hizi hazikuleta suluhisho.

Baada ya hatua zote hizo kushindikana, tuliona kutafuta haki yetu Mahakamani ndio njia pekee.  Tuliomba msaada katika taasisi zinazotoa msaada wa kisheria, Kituo cha Sheria na haki za binadamu (LHRC) na Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), tukapatiwa mawakili ambao wamepambana miaka yote kututea (takribani miaka 5) mahakamani ili tupate haki yetu ya kusoma bila mafanikio. 

Tulianza Mahakama ya Hakimu Mkazi kisutu, tukakata rufaa mahakama kuu, tukakata rufaa mahakama ya Rufaa (Court of Appeal of Tanzania).  Ilipofika mwaka 2016, nikaona niachane na masuala ya kesi kwani ni muda mrefu nipo mahakamani.  Nikatoa faili langu mahakamani.

Nikaamua kuingia katika diplomasia tena.  Tukamuandikia barua Rais wa Tanzania awamu ya tano, Dk John Magufuli, kuomba aingilie kati mgogoro huu ili tupate haki yetu ya kusoma nchini.

Tuliamini na bado ninaamini kwamba, mtu mwenye mamlaka makubwa kwenye nchi yoyote ile duniani, baada ya Mwenyezi Mungu ni Rais. Tukashukuru Mungu, Wasaidizi wa Rais katika masuala ya elimu na sheria walionyesha ushirikiano.

Tumekaa vikao mara kadhaa Ikulu, wakamshirikisha Mkurugenzi wa Vyuo vikuu, wakaishirikisha Wizara ya Elimu na Mkurugenzi Mtendaji wa Tume ya Vyuo vikuu (TCU), wakati huo akiwa ni Prof. Yunus Mgaya.

Februari 12, 2016, TCU waliwaandikia barua rasmi Chuo (UDSM) kwamba kwa mujibu wa sheria ya vyuo vikuu (Universities reguration 43 (1) GN 226 ya mwaka 2013, mwanafunzi aliyefukuzwa Chuo kwa masuala ya kinidhamu anaruhusiwa kuomba Chuo kwa mara nyingine tena baada ya miaka miwili kupita, katika chuo hicho hicho au vyuo vingine tangu kufukuzwa kwake (Barua imeambatanishwa), hivyo akakiomba Chuo kitupe ushirikiano.

Kutokana na ushauri husika, mwaka 2016 nikaomba udahili katika Vyuo vikuu vitatu ikiwemo UDSM.  TCU wakanichagua nisome UDSM, Shahada ya Uchumi (Economics) ambacho kilikuwa ni kipaumbele changu cha pili baada ya Sheria. 

Kwakuwa ndoto yangu ni kusoma shahada ya sheria, nikaanza hatua za kubadilisha kozi kuelekea Shahada ya Sheria, Utawala wa UDSM, ulinipa ushirikiano kwa kugonga mihuri ya kukubali kubadilisha kozi yangu, hadi Makamu Mkuu wa Chuo anayeratibu wanafunzi wa shahda ya kwanza (DVC Undergraduate UDSM), alithibitisha hamisho langu.

Hivyo, hakuna mhusika yeyote wa Utawala UDSM, ambaye alikuwa hajui kwamba, Alphonce Lusako, anasoma UDSM.  Miezi minne sasa imepita tangu nianze masomo yangu chuoni.

Katika hali ya sintofahamu  Januari 30, mwaka huu, nikiwa katika ratiba yangu ya mtihani nikapewa barua ya kusimamishwa uanafunzi wangu kwa kile kinachodaiwa kwamba nimedahiliwa kimakosa na hivyo kusimamishwa rasmi masomo katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM). Sio siri, nilishtushwa, niliumizwa, kibinadamu iliniwia vigumu sana.

Kikao na Mkurugenzi Mtendaji wa Tume ya Vyuo vikuu (TCU)

Kwakuwa nilikuwa katika ratiba ya mitihani yangu (UE), haraka iwezekanavyo, nikakikimbilia Tume ya Vyuo vikuu (TCU) kuonana na Mkurugenzi Mtendaji wa TCU, nikijaribu kuomba aingilie kati dhuluma hii ili nifanye mitihani yangu.

Niliandika barua rasmi kwa mujibu wa Sheria za vyuo vikuu (Universities Regulation) ili TCU inisaidie haraka iwezekanavyo niendelee na mitihani, kwani . Mkurugenzi akasema niache barua atakaa na wanasheria wake kisha nitapewa mrejesho.

Nimeshinda TCU siku zote tatu bila ya majibu ya barua yangu.  Nilipofanya marejeo ya Maamuzi ya Baraza la UDSM Desemba 13, 2011, yaliyoelekeza Tume ya Vyuo Vikuu (TCU) kutufuta katika Mfumo wa Elimu nchini.  Huenda haya yote yanayotokea sasa ni utekelezaji wa maazimio husika.

Watanzania, ifahamike kwamba ninaonewa, niliwahi kumuambia Makamu Mkuu wa UDSM, Prof. Rwekaza Mkandala, kwamba “Kumnyima mtoto wa masikini elimu, ni sawa na kumpiga risasi afe katika nchi yake.”  Hakuna dhambi kuu niliyoitenda nchi hii, nikastahili adhabu ya kupokwa haki yangu ya kusoma ndani ya nchi hii milele.

UDSM ni chuo kikuu cha umma, ni chuo kilichojengwa na kodi za watanzania, ni chuo kilichojengwa na jasho la kila mtanzania.  Hivyo kila mtanzania mwenye sifa kwa mujibu wa kanuni, taratibu na sheria, anapaswa kusoma katika chuo hiki bila kubaguliwa.

Kuongoza Vyuo Vikuu kwa misingi ya Sheria

Mpaka sasa ninamifano ya wanafunzi walioikimbia nchi hii na kuenda kusoma nje ya nchi kwa sababu ya ukiukwaji mkubwa wa Sheria ndani ya vyuo vikuu nchini.

Natamani kuona nchi hii inaongozwa kwa mujibu wa katiba na sheria za nchi hii.  Tukiendelea kuongoza vyuo vikuu , kwa visasi, chuki binafsi, neno la mtu likawa sheria, watawala wa vyuo vikuu wakawa juu ya sheria, tutaliingiza taifa hili katika gharama za machafuko.

Hitimisho

Nimetafakari sana na kujiuliza maswali mengi watanzania.  Ninachokishuhudia katika maisha yangu ni kwamba; hawapambani na binadamu anayeitwa Alphonce Lusako, wanapambana na elimu atakayoipata Alphonce.

Fimbo yao kuu, ni umasikini wangu na wazazi wangu.  Kibinadamu masuala haya ni magumu sana. Nimeona nimuache Mwenyezi Mungu apambane mwenyewe.

Aidha, niwashukuru viongozi wote wa dini walionipigia simu kutoka Mikoa mbalimbali, wakinifariji, nachelea kusema, waliombee Taifa kwani kuna vijana wengi katika vyuo vikuu hutendwa kama ninavyotendwa.

Niwashukuru wazazi wangu watambue kwamba haya ni mapito na yatapita. Niwashukuru wanafunzi wenzangu wa UDSM, niseme neno moja tu kwaherini!

Niwashukuru wanasheria, ndugu na marafiki zangu walioshikamana na mimi katika wakati huu mgumu.  

Nachotaka niseme kwao ni kwamba, hatma ya maisha ya mwanadamu ipo mikononi mwa Mwenyezi Mungu.
ALPHONCE LUSAKO, MWANAFUNZI ALIYEFUKUZWA UDSM 'AFUNGUKA' ALPHONCE LUSAKO, MWANAFUNZI ALIYEFUKUZWA UDSM  'AFUNGUKA' Reviewed by Unknown on 21:09 Rating: 5

No comments:

Theme images by merrymoonmary. Powered by Blogger.