ALICHOSEMA TUNDU LISSU BAADA YA RAIS MAGUFULI KUHUTUBIA SIKU YA SHERIA
Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu. |
Na Tundu Lissu
Nimesikiliza
sehemu ya hotuba ya Rais Magufuli wakati wa sherehe za Siku ya Sheria leo. Nimemsikiliza aliposema wanaokamatwa na nyara
za Serikali au madawa ya kulevya wanastahili kuchukuliwa hatua bila kufuata
taratibu za kawaida za kisheria hasa pale wanapokamatwa 'red-handed’
(kithibitisho mkononi).
Amesema
na mawakili wanaowatetea nao wanastahili kukamatwa na kuwekwa rumande ili na
wao 'waisome namba' ili pengine waache kuwatetea wakosaji hawa. Wote waliokuwa wanamsikiliza Rais, akiwamo
Kaimu Jaji Mkuu na Majaji wenzake wa Rufaa na Mahakama Kuu, Mawakili na wageni
wengine waliokuwapo pale, waliangua kicheko kikubwa.
Wanafikiri
alichokisema ni cha kuchekesha. It's not
funny at all (siyo jambo la kuchekesha hata kidogo). Jeshi letu la polisi limekubuhu katika kusingizia
watu vitu vya uongo. Kwa polisi wa nchi
hii, planting evidence (kupandikiza ushahidi), kuwekea watuhumiwa nyara za
serikali au madawa au silaha ili wawakamate na kuwafungulia mashtaka mazito ili
kuwakamua watoe pesa, ni kitu cha kawaida sana.
Polisi
wetu wamekubuhu katika ‘kusachi’ watu bila kuwa na ‘search warrants’ na bila
kufuata sheria na taratibu za kufanya ‘sachi’.
Hivi ndivyo wanavyopandikiza ushahidi.
Polisi wetu wamekubuhu katika kutesa watuhumiwa ili wakiri makosa ambayo,
mara nyingi, hawakuyafanya.
Yote
haya tunayafahà mu na Mawakili, Majaji na Mahakimu wa nchi hii wanayafahamu
sana. Wanakutana nayo kila siku mahakamani. Kauli ya Rais wetu kwamba watuhumiwa hawa
washughulikiwe mara moja bila kujali taratibu za kisheria zilizopo ni baraka
kwa matendo haya machafu ya jeshi letu la polisi.
Ni
presidential blessings for state lawlessness (ni Baraka za Rais kwa nchi
kuvunja sheria) na ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu. Ndicho kitakachofuatia bila shaka
yoyote. Yamekuwa yanatokea muda wote,
sasa yataongezeka kwa sababu yana baraka za Rais.
Kilichonishangaza
mimi sio alichosema Magufuli, huyu tumeshamzoea, bali ‘reaction’ ya waliokuwa
wanamsikiliza ambao wanafahamu fika madhara ya kauli hii ya Rais. Kwingineko duniani Mawakili wangetoka nje in
protest (kwa maandamano) na Rais angeshambuliwa vikali kila mahali kwenye
vyombo vya habari, kama tunavyoona yanayomtokea Rais Donald Trump wa Marekani.
Sio
Tanzania. Kwetu kila mtu anaona ni
kichekesho. Kuhusu Mawakili kukamatwa, miezi
kadhaa iliyopita Kamanda wa Polisi Zanzibar, Ahmed Msangi, kama sikosei, alitoa
kauli ya kuwatisha Mawakili wa Zanzibar waliokuwa wanawatetea watuhumiwa wa
kesi za kisiasa walizofunguliwa dhidi ya viongozi na wanachama wa CUF huko
Zanzibar.
Kamanda
huyo alisema Mawakili wanaowatetea watuhumiwa hao nao watakamatwa na kuwekwa
ndani. Kauli hiyo ilishambuliwa vikali, na kwa usahihi kabisa, na Chama cha
Mawakili Zanzibar (ZLS) na wenzao wa Chama cha Mawakili Tanzania (TLS). Leo Magufuli ametoa kauli hiyo hiyo, na
waliokuwa wanamsikiliza wamechekelea badala ya kutoka nje ya ukumbi in protest
(kwa maandamano).
Tusubirie
tuone kama TLS watadiriki kutoa kauli ya aina waliyoitoa wakati wa sakata la
Zanzibar au wakili mwenzao alipokamatwa Loliondo. Mimi binafsi nina mashaka makubwa kama
watadiriki kufungua mdomo.
Katiba
yetu inatamka wazi kwamba kila mtuhumiwa anahesabika kuwa hana hatia mpaka
mahakama zitakapothibitisha vinginevyo.
Rais Magufuli haamini hivyo. Kwake
kila mtuhumiwa sio tu ana hatia bali pia hastahili kusikilizwa wala kupata
utetezi wa wakili mahakamani.
Anachostahili
ni adhabu tu, and the bigger the punishment the better (tena adhabu kubwa ndiyo
nzuri zaidi). Katiba yetu inasema kila
mtuhumiwa ana haki ya kusikilizwa kwa ukamilifu. Haki hii, kama ambavyo mahakama zetu za juu
zimesema mara kwa mara, inajumuisha kusikilizwa kupitia kwa wakili.
Juzi
Jumanne tumepitisha haraka haraka na kwa mbwembwe nyingi Sheria ya Msaada wa
Kisheria. Sheria hiyo inasema kila
mtuhumiwa wa kesi ya jinai ana haki ya kupatiwa wakili bila malipo yoyote kama
Jaji au hakimu akiona inafaa. Mtendaji
Mkuu wa Mahakama, mteule wa Rais, amepewa mamlaka ya kuwalipa mawakili
watakaowatetea watuhumiwa hawa.
Kwahiyo,
fedha za umma zitatumika kuwalipa mawakili watakaowatetea watuhumiwa hawa wa
makosa ya jinai. Bila shaka Muswada wa
Sheria hii ulipitia kwenye Baraza la Mawaziri kama ilivyo kawaida. Leo Rais Magufuli na Mwenyekiti wa Baraza la
Mawaziri anatamka hadharani kwamba mawakili watakaowatetea watuhumiwa
wanaokutwa na nyara za serikali au madawa ya kulevya na wao wakamatwe na kutiwa
ndani.
Waziri
ambaye juzi alikuwa anashadadia watuhumiwa hawa wapatiwe msaada wa kisheria
bila malipo anachekelea kauli ya Rais. Majaji na Mahakimu watakaoamua
watuhumiwa hawa wapatiwe msaada wa kisheria nao wanachekelea. Na Mawakili ambao wanatakiwa na sheria watoe
msaada wa kisheria na ambao watakuwa victims (wathirika) wa kauli ya Magufuli
nao wanachekelea.
I
can only imagine (sipati picha) Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya angetoa kauli ya
aina hii Mawakili, Wanasiasa, Waandishi habari na wananchi wa kawaida wa Kenya
wangemfanyaje! Lakini kwetu wanachekelea.
This happens only in Tanzania (mambo haya yanatokea Tanzania peke yake).
ALICHOSEMA TUNDU LISSU BAADA YA RAIS MAGUFULI KUHUTUBIA SIKU YA SHERIA
Reviewed by Unknown
on
12:56
Rating:
No comments: