ANGUKO SHULE ZA SERIKALI TUSITAFUTE MCHAWI KUTOKA NJE, NI SISI WENYEWE
Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi. Prof. Joyce Ndalichako. |
Na
Dotto Bulendu
Wakati huo shule za serikali kama shule za sekondari Azania,
Mwanza, Mwenge, Mzumbe, Ilboru, Kilakala, Loreza, Mazengo, shule ya wavulana
Tabora, Milambo, Rugambwa,Ihungo, Tosamaganga, shule ya ufundi Tanga (Tanga
Tech), Msalato, Jangwani, Mkwawa, zikifanya vizuri hatukuwa tunachimba madini,
tulikuwa tunalima pamba, chai, mkonge,tumbaku, lakini pia tulikuwa tunafuga tu
mifugo.
Kipindi hicho uwekezaji ulikuwa mkubwa, shule za
msingi za serikali zilikuwa wanafunzi wanagaiwa madaftari, wanakunywa uji bure,
penseli na biki zilikuwa zinagaiwa.
Waliofaulu kwenda sekondari walikuwa wanasafiri bure, chakula
bure, shuleni ilikuwa ni sehemu salama, ukikosa kuchaguliwa shule za serikali ilikuwa
ni kilio, unaweza kujifungia ndani wiki nzima ukilia kukosa nafasi ya kwenda
shule ya serikali.
Chuo Kikuu ilikuwa ni sehemu ya heshima, unakwenda
Chuo Kikuu kwa gharama ze serikali, si mkopo kama ilivyo sasa.
Vikaibuka vitoto fulani, vikaja na mawazo yao ya
utaratibu mpya wa kuendesha uchumi wa dunia, vikauita SAPs, vikauza mawazo yao
Benki ya Dunia (WB) na Shirika la Fedha Ulimwenguni (IMF), wakaletewa Waafrika
wakiwemo watanzania.
Vikasema hivi vitoto vya Chuo Kikuu kutoka Ulaya, eti
mfumo huu wa elimu ni mbovu,serikali ijitoe kabisa, iache kubeba gharama za
kuendesha elimu,vikasema si sawa serikali kugharamia elimu.
Wakubwa wetu kama walivyo, yaani wao ni kama madodoki,
hawawezi kukataa wala kuhoji, jambo likitoka Ulaya ama Marekani au Asia ni zuri
hilo, wakamuona Mwalimu Nyerere kapitwa na wakati, wakakumbatia utandawazi na
mawazo ya tuvijana tulivyobuni mradi wa SAPs, wakaanza sema ooooh, sasa shule
watu wachangie.
Mara ooh, kazi ya serikali siyo kuwahudumia watu wake,
serikali zetu zikaanza kujiondosha kugharamia elimu yetu, viongozi wetu
wakaanza kujenga shule zao binafsi na kuachana na shule wanazozisimamia.
Enzi hizo za Julius Nyerere, Idara ya ukaguzi ilikuwa
imara sana, si kila mtu alikuwa mwalimu, ilikuwa huwezi kwenda darasa la tano
bila mtihani wa darasa la nne,ilikuwa huwezi kwenda kidato cha tano bila
kufaulu kidato cha nne, ilikuwa huwezi kwenda kidato cha tatu bila kufaulu
mtihani wa taifa wa kidato cha pili, huendi Chuo Kikuu bila ‘Principle pass’
mbili na ‘subsidiary’ moja zenye wastani wa 4.5.
Haya yote yalifutwa, ikawa zigizaga, tukaanza kujenga
shule bila nyumba za walimu, tukaanza kuajiri wahitimu wa kidato cha sita wasio
na mafunzo ya ualimu eti tukaita Voda fasta, serikali ikajitoa kuendesha na
kusimamia shule zake.
Shule zikajengwa huku hazina hata kagari kadogo, enzi
hizo karibu shule zote za serikali zilikuwa na magari makubwa, leo shule hazina
hata pikipiki, walimu wanalalamika kila siku,hawana morali, wanafundisha wakiwa
na mawazo (Go slow strike).
Sasa serikalini kila mtu anachaguliwa, hakuna tena
ushindani wa kuingia shule za serikali, ushindani umehamia shule binafsi, shule
za Serikali leo hakuna mitihani ya kuchuja, kuna kipindi eti wastani wa kwenda
kidato cha tatu kutoka cha pili ulishushwa mpaka asilimia 14 kutoka asilimia
21, wakati huko shule binafsi na seminari,ili utoke hatua moja lazima upate
wastani wa asilimia si chini ya 50, wengine lazima upate asimilia 60, halafu
tunataka shule za binafsi zifanye vizuri.
Hatutakiwi kusaka mchawi kutoka nje katika hili la
kufanya vibaya kwa shule za serikali, wachawi ni sisi wenyewe, tukubali kuwa
tulikosea na tulifanya mambo ya ajabu ambayo leo yanatugharimu.
ANGUKO SHULE ZA SERIKALI TUSITAFUTE MCHAWI KUTOKA NJE, NI SISI WENYEWE
Reviewed by Unknown
on
12:09
Rating:
No comments: