MANJI APIGILIWA MSUMARI MWINGINE, Adaiwa kuajiri raia wa kigeni bila vibali, Uhamiaji yataka ajisalimishe mwenyewe.

Mwenyekiti wa Kampuni ya Quality Group, Yusuf Manji
Na Mtapa Wilson
Idara ya Uhamiaji Mkoa wa Dar es Salaam, imekamata hati za kusafiria zipatazo 126, ambapo imebaini kuwa hati 25 zilikuwa zinamilikiwa na raia wa kigeni wenye asili ya Asia, ambao walikuwa wakifanya kazi katika kampuni ya Quality Group, bila kuwa na kibali cha kufanya kazi nchini (work permit), jambo ambalo ni kinyume cha sheria.

Kampuni ya Quality group inamilikiwa na mfanyabishara maarufu nchini, Yusuf Manji, ambaye hivi karibuni amekuwa akituhumiwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, kuwa anajihusisha na biashara pamoja na matumizi ya dawa za kulevya.

Akizungumza na waandishi wa habari, leo jijini Dar es Salaam, Ofisa Uhamiaji wa Mkoa wa Dar es Salaam, John Msumule, amesema idara yake imeshafanya uchambuzi wa kina na inajiandaa kuwafungulia mashitaka raia wote hao wa kigeni pamoja na mmiliki wa kampuni hiyo, Yusuf Manji.

“Wote hawa, hatua zitachukuliwa na watapelekwa mahakamani.  Lakini labda niseme ukweli, hawa hawatapelekwa peke yao mahakamani.  Lazima Yusuf Manji, ambaye ndiye mwajiri wa watu hawa na mmiliki wa kampuni hii, naye afikishwe mahakamani ili kujibu mashitaka,” amesema.

Msumule amesema Idara yake ilitaka kumkamata Manji, jana ili alale mahabusu na leo afikishwe mahakamani lakini kwa bahati mbaya walipokea taarifa kuwa Manji amelazwa hospitalini mpaka sasa.

Msumule ameendelea kusisitiza kuwa pindi Manji atakaporuhusiwa kutoka hospitalini anatakiwa kujisalimisha mwenye kwenye Ofisi za Idara ya Uhamiaji Mkoa ili aunganishwe moja kwa moja katika tuhuma hizo zinazomkabili.
MANJI APIGILIWA MSUMARI MWINGINE, Adaiwa kuajiri raia wa kigeni bila vibali, Uhamiaji yataka ajisalimishe mwenyewe. MANJI APIGILIWA MSUMARI MWINGINE, Adaiwa kuajiri raia wa kigeni bila vibali, Uhamiaji yataka ajisalimishe mwenyewe. Reviewed by Unknown on 14:51 Rating: 5

No comments:

Theme images by merrymoonmary. Powered by Blogger.