MAKONDA AITWA BUNGENI KUJIELEZA, Atuhumiwa kulewa madaraka, Akiuka Sheria ya Dawa za kulevya

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda.
Na Mwandishi wetu

Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mbele ya Mwenyekiti wake, Andrew Chenge, limepitisha maazimio manne ikiwamo kuwaita na kuwahoji Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda na Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, Alexander Mnyeti, kwa tuhuma za matumizi mabaya ya madaraka.

Hoja hiyo ya kumuita Makonda na mwezake Mnyeti, ili wahojiwe na Kamati ya Bunge ilitolewa na Mbunge wa Ukonga, Mwita Waitara na baadaye kuungwa mkono kwa kauli moja na Bunge zima.

Makonda na Mnyeti wanadaiwa kutokidhi matakwa ya sheria ya utumishi wa umma na kutumia madaraka yao vibaya.

Mnyeti anatuhumiwa kuwanyanyasa waandishi wa habari, ambapo kwa nyakati tofauti amewasweka rumande waandishi wa kituo cha televisheni cha ITV na kituo cha Radio Five cha jijini Arusha.

Aidha Makonda anadaiwa kuvunja sheria nyingi ikiwemo ya maadili ya utumishi wa umma na sheria ya kudhibiti madawa ya kulevya, ambapo kwa mujibu wa sheria hiyo Mkuu wa Mkoa hana mamlaka yoyote ya kutuhumu wala kutaja washukiwa wa madawa ya kulevya.

Kwa mujibu wa sheria hiyo, vyombo vinavyopaswa kushughulikia tuhuma za madawa ya kulevya ni Ofisi ya Waziri Mkuu, Mawaziri wenye dhamana, Mwanasheria Mkuu (AG), Mwendesha Mashitaka wa Serikali (DPP), Jeshi la Polisi na Idara ya Usalama wa Taifa (TISS).

Mwenyekiti wa Bunge, Andrew Chenge, aliruhusu hoja ya Waitara kujadiliwa na baada ya majadiliano Bunge lilipitisha maazimio manne ambayo ni kama ifuatav; Makonda na Mnyeti waitwe Bungeni ili kuhojiwa na Kamati, Waziri wa TAMISEMI apeleke mwongozo kwa Wakuu wa Mikoa na Wilaya kuwa wasiuchezee mhimili wa Bunge, Mamlaka ya Uteuzi wa Makonda na Mnyeti, zichukue uamuzi haraka wa kuwavua madaraka na Wabunge wasikamatwe bila kufuata utaratibu wa kibunge.
MAKONDA AITWA BUNGENI KUJIELEZA, Atuhumiwa kulewa madaraka, Akiuka Sheria ya Dawa za kulevya MAKONDA AITWA BUNGENI KUJIELEZA, Atuhumiwa kulewa madaraka, Akiuka Sheria ya Dawa za kulevya Reviewed by Unknown on 05:36 Rating: 5

1 comment:

Theme images by merrymoonmary. Powered by Blogger.