TUNDU LISSU AMSHUKIA DK. MWAKYEMBE KUFUTA CHAMA CHA WANASHERIA TANZANIA
Waziri wa Katiba na Sheria, Dk. Harrison Mwakyembe. |
Na Tundu Lissu
Mawakili
wenzangu. Mimi binafsi sijashangazwa na kauli ya Dk. Mwakyembe, kwamba
atakifuta Chama cha wanasheria Tanzania (TLS) kama kitajiingiza katika harakati
za kisiasa.
Hii sio mara ya
kwanza kwa viongozi wa serikali ya Tanzania kutoa vitisho vya kuifuta TLS. Waziri Mkuu zamani hayati Edward Sokoine aliwahi
kutishia hivyo katika kilele cha vita dhidi ya wahujumu uchumi mwanzoni mwa miaka
ya 1980.
Hata
kabla ya hapo katika miaka ya 1960 na 1970 watangulizi wa Sokoine walijaribu kufanya
hivyo hivyo. Sababu ya kuanzishwa kwa Shirika
la Sheria Tanzania (Tanzania Legal Corporation) kipindi hicho kulichagizwa na
jitihada za kuondoa mawakili wa kujitegemea au mawakili wasiokuwa wa serikali.
Vitisho
dhidi ya TLS vilirudi miaka ya 1990 wakati wa Augustino Lyatonga Mrema. Kitu kimoja kiko common katika vitisho hivyo
vyote. Vitisho hivi vimetolewa kila
wakati kwa TLS na mawakili wa kujitegemea wanapotumia uhuru wao kutetea utawala
wa sheria na kupinga uvunjifu wa sheria katika nchi na matumizi mabaya ya
madaraka miongoni mwa watawala.
Mawakili
wakiwa kimya na TLS ikiwa mfukoni mwa serikali na wasipohoji matumizi mabaya ya
madaraka basi wanakuwa ni watu wanaojipendekeza kwa serikali.
Kuna
kitu kingine ambacho siku zote huwa kinatokea kwamba vitisho hivi havijawahi
kufanikiwa na havitafanikiwa. Rais wa
kwanza wa Zanzibar, Sheikh Abeid Amani Karume alipiga marufuku uwepo wa taasisi
binafsi za kisheria mara baada ya Mapinduzi ya Zanzibar ya 1964. Tanzania ya leo sio Zanzibar ya miaka ya 1960
na 1970, hatutakubali udikteta wa aina ya Karume au wa aina nyingine yoyote
kwenye Tanzania ya leo.
Inaelekea Dk.
Mwakyembe hafahamu au anajisahaulisha jinsi ambavyo TLS na mawakili binafsi
walivyo ambatanishwa kwenye mfumo wetu wa kikatiba na kisheria. Kwa lugha nyepesi, ukifuta TLS maana yake ni
kwamba hakuna wakili binafsi hata mmoja nchi nzima.
Mfumo
mzima wa kimahakama unategemea uwepo wa mawakili na kwa hiyo uwepo wa TLS. Mahakama karibu zote zitashindwa kufanya kazi
kusipokuwa na mawakili binafsi. Vivyo
hivyo itakuwa katika taasisi zingine za kisheria na kimahakama.
Aidha,
kuna taasisi nyingi zilizoundwa na Katiba yetu - kama vile Tume ya Huduma za
Mahakama (Judicial Service Commission) na Tume ya Mabadiliko ya Sheria (Law
Reform Commission), ambazo zinakuwa zinaundwa kukiwa na uwakilishi wa TLS.
Kuna
taasisi nyingine nyingi ambazo zimeanzishwa na sheria za kawaida ambazo uundwaji
wake unakamilika kukiwa na uwakilishi wa TLS. Hilo agizo la kisheria, kikatiba
na kisiasa litakalofanya kufutwa kwa TLS, ni kitu ambacho hakijawahi kutokea na
wala haifikiliwi kuwa kitatokea kwa mtu mwenye akili timamu.
Dk. Mwakyembe ana
akili timamu. Anaweza kuwa
anatania. Hawezi kufuta TLS. Anachotaka kufanya ni kuwatisha mawakili ili
wachague watu wale wale wa miaka yote kuongoza TLS. Anatutisha ili tuendelee na sura ile ile
katika uongozi wa TLS.
Hataki
tufanye mabadiliko yanayohitajika ili TLS yetu isichukue nafasi yake stahiki
katika kuamua mustakbali wa nchi yetu na wa taaluma yetu. Nawataka viongozi na wanachama wa TLS
wamkemee Dk. Mwakyembe kwa nguvu kubwa zaidi.
Nawataka wagombea
wenzangu wa nafasi mbali mbali za uongozi katika TLS wajitokeze hadharani na
kulaani kauli ya Dk. Mwakyembe bila kujali tofauti. Wakinyamaza tutawajua wako
upande wa nani? Sura ile ile ya uongozi wa TLS au mabadiliko. Na nitawaomba nyote
mpige kura kulingana na hali hiyo.
TUNDU LISSU AMSHUKIA DK. MWAKYEMBE KUFUTA CHAMA CHA WANASHERIA TANZANIA
Reviewed by Unknown
on
09:44
Rating:
No comments: