TUNDU LISSU AMKOSOA MAKONDA KISHERIA, Asema hana mamlaka ya kumfukuza mtu Mkoani kwake, ataka aelimishwe kwa kushtakiwa.
Mbunge wa Singida Mashariki na Mwanasheria Mkuu wa Chadema, Tundu Lissu |
Na Tundu Lissu
Kauli
ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam,Paul Makonda, kwamba ana uwezo wa kumhamisha
mtu yeyote kutoka kwenye Mkoa wake ni mfano mwingine wa aina ya wanasiasa waliopewa
madaraka na Rais Magufuli, ambayo hata hawayaelewi na kwa sababu hiyo, hata wao
wenyewe hawajielewi.
Nafasi ya Wakuu wa
Mikoa imetambuliwa na ibara ya 61 ya Katiba yetu. Ibara ya 61(4) inafafanua kwamba kila Mkuu wa
Mkoa atatekeleza kazi na majukumu yaliyofafanuliwa na, au chini ya, sheria yoyote iliyotungwa na Bunge.
Sheria
iliyotungwa na Bunge kwa ajili ya kufafanua kazi na majukumu ya Wakuu wa Mikoa
ni Sheria ya Tawala za Mikoa ya 1997.
Sheria
hiyo ndiyo iliyowapa Wakuu wa Mikoa na Wilaya mamlaka ya kipolisi, yaani
mamlaka ya kukamata watu wanaosadikiwa kufanya makosa ya jinai mahali ambapo
hakuna askari polisi.
Mamlaka
haya ni madogo sana tofauti na Wakuu wa Mikoa au Wilaya wa aina ya Makonda
wanavyoamini au kuaminishwa.
Kwanza,
ni mamlaka ya nyongeza (supplementary powers) tu kwa mamlaka ya Jeshi la Polisi
ambalo ndilo lenye mamlaka hasa ya kukamata wahalifu.
Hii
ina maana kwamba Mkuu wa Mkoa au Wilaya hawezi kutumia mamlaka ya kipolisi pale
ambapo tayari kuna askari polisi. Polisi
wanatakiwa wafanye kazi yao bila kuamriwa na Mkuu wa Mkoa au Wilaya.
Pili,
mamlaka ya kipolisi yamewekewa masharti ya muda, yaani, mtu aliyekamatwa kwa
amri ya Mkuu wa Mkoa au Wilaya anatakiwa apelekwe mahakamani au aachiliwe huru
ndani ya muda wa saa 48.
Tatu,
Mkuu wa Mkoa au Wilaya aliyetoa amri ya kukamata mtu chini ya mamlaka yake ya
kipolisi, anatakiwa haraka iwezekanavyo kupeleka taarifa ya maandishi kwa
hakimu juu ya kukamatwa kwa mtu huyo na sababu zake.
Sheria
imeweka wazi kwamba Mkuu wa Mkoa au Wilaya asiyetekeleza masharti haya
hataruhusiwa kumkamata mtu huyo kwa kosa hilo hilo na anaweza kushtakiwa
mahakamani kwa kosa la matumizi mabaya ya madaraka yake.
Hakuna
mahali popote katika Sheria ya Tawala za Mikoa ambako Mkuu wa Mkoa au Wilaya
amepewa mamlaka ya kumwondoa mtu yeyote kwenye Mkoa au Wilaya yake.
Mamlaka
ya kuondoa watu kwenye maeneo yao, yaani deportation, yalikuwa sehemu ya
mamlaka ya Rais kwa mujibu wa Sheria ya Kuondoa Watu (Deportation Ordinance).
Sheria
hii ya kikoloni ilitangazwa kuwa kinyume na Katiba, na kwa hiyo batili, na Jaji
James Mwalusanya wa Mahakama Kuu katika kesi maarufu ya Chumchua Marwa na
Wenzake ya mwaka 1987.
Ni
wazi Mkuu wa Mkoa wa aina ya Paul Makonda, hawezi kufahamu mambo makubwa kama
haya. Kwake yeye na kwa Wakuu wa Mikoa
au Wilaya wa aina yake, kuwa Mkuu wa Wilaya au Mkoa ni sawa na kuwa Rais wa
Mkoa au Wilaya aliyokabidhiwa.
Wakuu
wa aina hii wanahitaji kuelimishwa kwamba wao hawana mamlaka ya kifalme aliyonayo
Magufuli.
Na
namna bora kabisa ya kuwaelimisha ni kuwashtaki kwa madai mahakamani pale
wanapoenda nje ya masharti ya madaraka yao.
Tutaanza na Paul Makonda.
TUNDU LISSU AMKOSOA MAKONDA KISHERIA, Asema hana mamlaka ya kumfukuza mtu Mkoani kwake, ataka aelimishwe kwa kushtakiwa.
Reviewed by Unknown
on
07:51
Rating:
No comments: