MAKAMU WA RAIS ATAJWA DAWA ZA KULEVYA
Rais wa Venezuela, Nicholas Maduro (kulia) akiwa na Makamu wake, Tareck El Aissami. (Picha na AFP) |
Venezuela
Marekani imetangaza vikwazo dhidi ya Makamu wa Rais
wa Venezuela, Tareck El Aissami, kwa tuhuma za kuhusika na ulanguzi wa
kimataifa wa mihadarati. El Aissami
ameongezwa kwenye orodha ya walanguzi wakuu wanaosakwa na Marekani.
Aidha tajiri maarufu wa Venezuela, Samark Lopez, amewekewa
vikwazo kwa kutuhumiwa kama mshirika mkuu wa El Aissami. Tareck El Aissami, aliteuliwa kama Makamu wa
Rais na Rais Nicolas Maduro mwezi uliopita.
El
Aissami amekanusha madai ya kuhusika na visa vyovyote ya jinai. Lakini Lopez hajajibu hatua hizi za
Marekani. Vikwazo hivi vinamaanisha
kwamba mali yote ya Makamu wa Rais iliyoko Marekani inashikiliwa huku akizuiwa
kuingia nchini humo.
Wizara
ya Fedha ya Marekani imesema kwamba, El Aissami alisimamia kuvukishwa kwa tani
nyingi za mihadarati ndani ya Marekani kwa kutumia ndege au meli.
Kadhalika imeongeza kuwa alikua kwenye orodha ya
waliopokea mulungula kutoka kwa mlanguzi mkuu wa mihadarati wa Venezuela
aliyeko korokoroni, Walid Makled, ili kumkinga wakati akiendelea na biashara
haramu.
El Aissami aliwahi kuwa Gavana wa jimbo la Aragua na
pia akawa waziri wa Mambo ya Ndani na Sheria nchini Venezuela kati ya mwaka
2008 na 2012. Taarifa zilizonadiwa na
mashirika ya habari ya nchini Marekani, zinasema kuwa El Aissami alikua
akichunguzwa na Marekani kwa kushirikiana na kundi la wapiganaji la Hezbollah
nchini Lebanon.
Wakati
akiwa Waziri wa Mambo ya Ndani, imedaiwa kuwa hati kadhaa za kusafiria za Venezuela
zilipatikana zikitumiwa na wapiganaji wa Hezbollah. Mapema mwezi huu wabunge 34 wa Baraza la
Congress Marekani walimuandikia waraka Rais Donald Trump, wakimtaka kuweka
vikwazo kwa baadhi ya Maofisa wa serikali ya Venezuela.
Walimtaja
hasa Tereck Al Aissami, wakisema ana nafasi kubwa ya kuongoza nchi kama Makamu
wa Rais na alistahili kuchukuliwa hatua kutokana na tuhuma zake kuhusika na
ulanguzi wa mihadarati pamoja na kuwa mshirika wa kundi ambalo Marekani
imeliorodhesha kama la kundi la kigaidi.
CHANZO: BBC
MAKAMU WA RAIS ATAJWA DAWA ZA KULEVYA
Reviewed by Unknown
on
10:22
Rating:
No comments: