UN WOMEN: SHERIA ZINAZOKANDAMIZA WANAWAKE NA WASICHANA ZIBADILISHWE

Mkurugenzi Mtendaji wa UN Women, Phumzile Mlambo-Ngcuka akizungumza katika mkutano wa kimataifa uliofanyika katika ukumbi wa makao makuu ya Umoja wa Mataifa (UN) na kujadili Ajenda ya Mpango wa Maendeleo ya Usawa wa Kijinsia ifikapo mwaka 2030. (Picha na UN Women/Ryan Brown)

Na Mtapa Wilson

Upitiaji upya wa sheria, mabadiliko ya sheria na utekelezaji wake ni lazima uzingatie haki za binadamu kama vile usawa wa kijinsia ili kufikia Malengo Endelevu (SDG’s) ya Umoja wa Mataifa ikifikapo mwaka 2030.

Hayo yamesemwa katika mkutano wa ushirikiano mpya unaolenga kuleta mabadiliko ya sheria za ukandamizaji wa kijinsia na kuanzisha mpango wa maendeleo ya usawa wa kijinsia duniani.

Mkutano huo umeandaliwa kwa pamoja na Shirika la Umoja wa Mataifa linalojihusisha na masuala ya Wanawake la UN Women, Jumuiya ya Kimataifa ya Muungano wa Mabunge (IPU) na Shirika la Usawa Sasa (Equality Now).

Licha ya baadhi ya maendeleo katika miaka michache iliyopita, inakadiriwa kwamba asilimia 90 ya nchi zote duniani zina sheria angalau moja ya ukandamizaji wa kijinsia katika mifumo yake ya kisheria.

Kuna baadhi ya sheria ambazo zinazuia mwanandoa kushitaki endapo atakuwa amebakwa na wakati mwingine hakuna utekelezaji wa sheria za kupiga marufuku ndoa za utotoni au ukeketaji.

Aidha kuna sheria zinazoshindwa kukabiliana na unyanyasaji dhidi ya wanawake kutokana na utekelezaji wake kusuasua na pengine kukosekana kwa usiri na ulinzi kwa wanawake waathirika wa vitendo vya kikatili, ambao hutafuta usaidizi wa kisheria dhidi ya unyanyasaji unaowakumba.

Vilevile bado kuna utekelezaji hafifu wa sheria zinazotoa fursa ya ushiriki sawa wa wanawake katika shughuli za kisiasa.  Mfano; sheria ya nafasi za upendeleo katika uwakilishi wa wanawake bungeni.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mtendaji wa UN Women, Phumzile Mlambo-Ngcuka amesema kuwa sheria inatakiwa kushughulikia ukandamizaji wa kijinsia katika maeneo ya umma, ikiwa ni pamoja na maeneo ya mitaani au maeneo ya usaifiri wa umma; kuhakikisha kuwa wanawake wanapata fursa sawa ya ajira na wanaume na kwamba wanalipwa ujira wao sawa na wanaume kwa kazi moja wanayofanya.

Pia sheria inatakiwa kuwawezesha watoto kupata utaifa si tu kutoka kwa baba zao, lakini pia hata kwa mama zao.

"Mara nyingi sheria za ukandamizaji wa kijinsia hutokana na mila kandamizi katika jamii, ambazo hubaki na kuenea na mara nyingi ni vigumu kuzibadilisha ndiyo maana UN Women inashirikiana na vyama vya kiraia na wanaharakati ngazi ya chini, ambao ni muhimu katika kubadilisha mitazamo miongoni mwa watunga sheria na jamii kwa ujumla."

"Sheria zinazowakandamiza wanawake na wasichana hazipaswi kuwepo ili kuweka usawa wa kijinsia.  Tunahitaji kufanya mabadiliko ambayo yataondoa kasumba ya ukandamizaji wa wanawake.  Hayo ndiyo yatakuwa maendeleo tumefanya kwa ajili ya vizazi vijavyo," amesema Mkurugenzi Mtendaji huyo.

Mpango wa UN Women katika maendeleo ya usawa wa kijinsia umelenga zaidi kuharakisha jamii siyo tu katika kurekebisha sheria bali pia kutekeleza kwa vitendo sheria mpya.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Equality Now, Yasmeen Hassan amesema kuwa “usawa chini ya sheria ni muhimu sana kwa ajili ya maendeleo ya usawa wa kijinsia, kwa sababu sheria huwapa nafasi wanawake kuchagua cha kufanya katika maisha.  Miaka 20 iliyopita tumeona maendeleo kadhaa.  Lakini hata hivyo tuna wasiwasi kuhusu kasi ya mabadiliko hasa juu ya sheria za kifamilia,”

Nae Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kimataifa ya Muungano wa Mabunge (IPU), Martin Chungong, ameongeza kuwa "Wanawake wote wanaendelea kukabiliwa na ukandamizaji bila kujali chimbuko lao.  Jumuiya ya kimataifa inahitaji kuunganisha nguvu ya pamoja kama tunataka kuwa na ufanisi katika kubadilisha mahusiano haya mabaya ya kijamii. IPU ina nia ya kuhamasisha mabunge na kutumia sheria kuziba mahala penye mianya ya ukandamizaji "

Mpango wa usawa wa kijinsia uliozinduliwa na Shirika la UN Women umejikita zaidi katika Malengo ya Maendeleo Endelevu, hasa lengo la tano juu ya usawa wa kijinsia, ambalo linatoa wito kwa kukomesha aina zote za ukandamizaji dhidi ya wanawake na wasichana kila mahali ifikapo mwaka 2030.
UN WOMEN: SHERIA ZINAZOKANDAMIZA WANAWAKE NA WASICHANA ZIBADILISHWE UN WOMEN: SHERIA ZINAZOKANDAMIZA WANAWAKE NA WASICHANA ZIBADILISHWE Reviewed by Unknown on 15:04 Rating: 5

No comments:

Theme images by merrymoonmary. Powered by Blogger.