WATOTO NJITI 210,000 WANAZALIWA NCHINI HUKU 13,900 WAKIPOTEZA MAISHA KILA MWAKA
Mama akiwa amembeba mtoto njiti kwa njia ya kangaroo ili kumpatia joto. |
Na Mtapa Wilson
Taasisi
inayosaidia watoto wanaozaliwa kabla ya wakati maarufu kama ‘watoto njiti’ ya
Doris Mollel Foundation imewaomba wadau mbalimbali wa afya nchini kujitolea kwa
hali na mali katika jitihada zake za kuwasaidia watoto njiti wanaozaliwa nchini.
Ofisa
Mtendaji Mkuu wa Doris Mollel Foundation, Doris Mollel, amesema kuwa ripoti ya Shirika
linalojishughulisha na afya ya mama na mtoto la Mamaye Afrika, mwaka 2014, inaonyesha
kuwa kila mwaka watoto wanaozaliwa kabla ya wakati nchini ni 210,000, huku wanaopoteza
maisha ni 13,900, kutokana na sababu zinazoweza kuepukika kama vile ukosefu wa
vifaa tiba.
Doris amesema
pia kwa mujibu wa takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO) zinaonyesha kuwa
takribani watoto milioni 15 wanazaliwa kabla ya wakati, hali inayosababisha
kuongezeka kwa vifo vya watoto kwa asilimia 40 duniani kote.
Aidha Doris
ameongeza kuwa kutokana na changamoto ya watoto njiti, taasisi yake imekuwa
ikishirikiana na serikali kwa kusaidia watoto wanaozaliwa kabla ya wakati
katika maeneo mbalimbali nchini.
“Mwaka 2015
tulisaidia watoto wapatao 4,015 katika hospitali 17 zilizoko katika mikoa mbalimbali
19 iliyopo nchini kwa kutoa vifaa tiba. Mbali
na vifaa tiba tunavyotoa kupitia wadau wetu wa Afya,” amesema.
Akielezea
changamoto iliyopo, Doris amesema wananchi walio wengi bado hawana ufahamu juu
ya tatizo zima la watoto wanaozaliwa kabla ya wakati, hivyo taasisi yake
imekuwa na jukumu kubwa la kuwafikia wananchi walio wengi katika maeneo ya
vijijini ili kuwapatia elimu ya kukabiliana na tatizo hilo. Lakini changamoto kubwa imekuwa ni uhaba wa
fedha, ambao unasababisha kushindwa kutoa msaada kwa watoto njiti wanaozaliwa.
“Sisi kama
taasisi tumeamua kuhakikisha wananchi wanaelimika juu ya watoto wanaozaliwa
kabla ya wakati na kutoa msaada wa vifaa tiba kwa watoto hao. Ajenda ya Umoja wa Kimataifa ni kupunguza
vifo vya watoto wanaozaliwa kabla ya wakati kwa asilimia 50 ifikapo 2025. Hii ni changamoto kwetu na changamoto kubwa
zaidi ni watu wengi hawana uelewa kabisa juu ya tatizo hili. Wanawake walio wengi bado wanajifungulia
nyumbani.”
WATOTO NJITI 210,000 WANAZALIWA NCHINI HUKU 13,900 WAKIPOTEZA MAISHA KILA MWAKA
Reviewed by Unknown
on
10:38
Rating:
No comments: