RC MAKONDA AAGIZA CHID BENZ, WEMA SEPETU, T.I.D, RECHO KUJISALIMISHA POLISI KWA UTUMIAJI WA MADAWA YA KULEVYA

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda.
Na Mwandishi wetu

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, ameagiza baadhi ya wasanii wa muziki wa bongo fleva na filamu nchini kujisalimisha wenyewe kesho katika kituo kikuu cha polisi jijini Dar es Salaam, kutokana na tuhuma zinazowakabili za utumiaji wa madawa ya kulevya.

Wasanii waliotajwa na Mkuu huyo wa Mkoa ni Khalid Mohamed maarufu kama T.I.D, Rashid Makwilo maarufu kama Chid Benz, Winfrida Josephat maarufu kama Recho, na muigizaji nyota wa filamu nchini, Wema Sepetu.

Akizungumza leo jijini Dar es Salaam mbele ya waandishi wa habari, Makonda amesema kuwa katika oparesheni maalumu aliyoiendesha hivi karibuni kwa ajili kubaini mtandao wa wauzaji, wasambazaji na watumiaji wa madawa ya kulevya, amegundua kuwa kuna wasanii wanahusishwa moja kwa moja na utumiaji wa madawa hayo haramu, jambo ambalo ni kinyume na sheria.

“Wapo wafanyabiashara wakubwa, majina yao yako hapa mtayachukua ili mkayaandike vizuri.  Wapo wale wasambazaji lakini wapo wengine wanasemekana wanatumia.  Hakuna aliyetoa ushahidi kama kweli wanatumia ila wanasemekana wanatumia.  Ukimuhoji huyu anasema na wengine wanakuambia huyu tunatumia naye. 

Sasa hawa nao ni vyema nikakutana nao pale kituo kikuu cha polisi, wakiwamo T.I.D, Wema Sepetu, Junior Sniper.  ……..kuna watu kama Recho, Chid Benz, wote hawa ni vijana wenzangu nadhani tukionana tutaelewana vizuri,” alisema Makonda.

Aidha Mkuu huyo wa Mkoa ameagiza kukamatwa kwa baadhi ya Maofisa wa jeshi la polisi Kitengo cha Kupambana na biashara ya madawa ya kulevya katika mkoa wake, ambao wanatuhumiwa kushirikiana na mtandao wa wauza madawa hayo mpaka pale uchunguzi utakapokamilika na ikibainika kuwa wanahusika basi hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.


RC MAKONDA AAGIZA CHID BENZ, WEMA SEPETU, T.I.D, RECHO KUJISALIMISHA POLISI KWA UTUMIAJI WA MADAWA YA KULEVYA RC MAKONDA AAGIZA CHID BENZ, WEMA SEPETU, T.I.D, RECHO KUJISALIMISHA POLISI KWA UTUMIAJI WA MADAWA YA KULEVYA Reviewed by Unknown on 16:32 Rating: 5

No comments:

Theme images by merrymoonmary. Powered by Blogger.