'FEZA BOYS' YATOA MSHINDI TUZO DSTV EUTELSAT AFRIKA
Na Mtapa Wilson
Davids
Bwana, ambaye ni mwanafunzi wa shule ya wavulana Feza nchini Tanzania amekuwa
mshindi wa pili barani Afrika katika shindano la kuwania tuzo ya nyota wa DSTV
Eutelsat, ambalo lilifanyika nchini Nigeria na washindi wake kutangazwa
Februari 7, mwaka huu.
Tuzo ya
nyota wa DSTV Eutelsat hushirikisha zaidi wanafunzi wa ngazi ya elimu ya
sekondari, ambapo hutakiwa kuwasilisha kazi zao kwa njia ya kuandika insha au
kuandaa bango kuhusu elimu ya anga hususani satelaiti kwa lengo la kukuza
vipaji vya kiakili kwa wanafunzi ili kuleta mageuzi endelevu na yenye tija
katika ulimwengu wa sayansi na teknolojia.
Tuzo ya
nyota wa DSTV Eutelsat huandaliwa na kampuni ya Multichoice Afrika kwa kushirikiana
na Shirika la anga la Eutelsat la nchini Ufaransa.
Ni mara ya
sita kufanyika kwa tuzo hii barani Afrika na mwaka huu imeshirikisha shule
takribani 1,000 na nchi 20 barani Afrika, ambapo mwanafunzi kutoka nchini
Ethiopia, Leoul Mesfin, aliongoza katika uandishi wa insha juu ya elimu ya
satelaiti akifuatiwa na mtanzania, Davids Bwana, jambo lililofanya kuwa mtu wa
kwanza kushika nafasi ya juu zaidi katika shindano hilo kutoka ukanda wa Afrika
Mashariki.
Wakati
katika upande wa kuandaa bango juu ya masuala ya satelaiti, nafasi ya kwanza
ilichukuliwa na mwanafunzi kutoka nchini Nigeria, Emmanuel Ochenje, kisha
nafasi ya pili kuchukuliwa na mwanafunzi kutoka nchini Botswana, Aobakwe Letamo.
Akizungumza
na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam, Bwana amesema kuwa amepata
nafasi hiyo kutokana na jitihada kubwa alizoziweka pamoja na walimu wake katika
kuandaa insha yake.
Amesema
ilikuwa ni changamoto kubwa kwake kushiriki shindano hilo ambalo lilikuwa
linahitaji kila mshiriki abuni satelaiti yake mwenyewe na kuielezea jinsi
itakavyofanya kazi na kusaidia kuboresha hali ya kiuchumi na kijamii, jambo
ambalo litasaidia kuharakisha maendeleo barani Afrika.
“kwa kifupi
mimi binafsi, familia yangu na wazazi wangu, na pia wanafunzi wenzangu wote kwa
ujumla tumefurahishwa sana na ushindi huu.
Bila shaka itakuwa changamoto kwa wanafunzi wenzangu kote nchini
kushiriki kwa wingi katika tuzo hizi mwakani ili ikiwezekana tufanye vizuri
zaidi na kuchukua nafasi zote za juu,” amesema.
Aidha Mkuu
wa Kitengo ya Uhusiano wa Umma wa kampuni ya Multichoice Tanzania, Johnson
Mshana, amesema kuwa nafasi aliyoipata Bwana katika shindano hilo ni
uthibitisho tosha kuwa watanzania wana uwezo mkubwa wa kushindana katika anga
za kimataifa.
“kitendo cha
kijana huyu kuibuka miongoni mwa washindi katika shindano linaloshirikisha kazi
bora kabisa kutoka mataifa 20 kote Afrika ni heshima kubwa sana kwetu. Hii itawatia sana moyo wanafunzi wa Tanzania
na hivyo kuongeza jitihada. Bila shaka
kabisa mwakani washindi wa kwanza pande zote watatoka Tanzania,” amesema.
Mkurugenzi
wa shule za Feza nchini, Ibrahim Yunus Rashid, amesema kuwa ushindi wa
mwanafunzi wao umewapa furaha kubwa sana kwa pamoja walimu, wanafunzi na
wafanyakazi wote kwa ujumla.
“Tumetiwa
moyo sana na tunaamini wanafunzi wetu na wafanyakazi wetu watakuwa na ari zaidi
katika kusoma na kufanya kazi ili kushiriki mashindano mbalimbali ya kitaifa na
kimataifa na bila shaka shule yetu itaendelea kufanya kazi vizuri,” amesema.
Naye mama mzazi
wa Davids Bwana, Dk. Mbutolwe Esther Mwakitalu, alipongeza sana jitihada binafsi
za mwanaye, walimu na wanafunzi wenzie, ambapo pia alitoa wito kwa wazazi
wenzake kuwa karibu na watoto wao na kuwasaidia kwa hali na mali katika ukuaji
wao wa kitaaluma kwakuwa elimu ndio urithi mzuri kwao na kwa vizazi vyao
vijavyo.
Kutokana na
ushindi alioupata Bwana, sasa atapata fursa ya kwenda Afrika ya Kusini
kutembelea Ofisi za Multichoice Afrika pamoja na Shirika la Anga la Afrika
Kusini akiwa kama mgeni maalum wa Multichoice Afrika.
'FEZA BOYS' YATOA MSHINDI TUZO DSTV EUTELSAT AFRIKA
Reviewed by Unknown
on
20:42
Rating:
No comments: