HIVI NDIVYO MWELEKEZI UTALII ALIVYOPOTOSHA MATAMSHI YA MTALII

Mwelekezi Utalii, Simon Sirikwa akiwa na Mtalii katika video iliyosambaa mtandaoni.
Na Mwandishi wetu.
Wiki iliyopita Mwelekezi Utalii (Tour guide) katika mbuga ya wanyama pori ya Serengeti, Simon Sirikwa, aliwekwa chini ya ulinzi kwa amri ya Waziri wa Mali asili na Utalii, Prof. Jumanne Maghembe, kwa madai ya kusambaza video kwenye mtandao wa kijamii, ambayo anatafsiri visivyo matamshi ya mtalii.

Katika video hiyo, mtalii mwanamke aliyekuwa amemaliza kutembelea hifadhi ya Ngorongoro alisikika akisema kuwa watu wa Tanzania ni wazuri na wakarimu kupindukia lakini Mwelekezi Utalii huyo alipotosha matamshi hayo na kusema kuwa mtalii huyo alikuwa akiwaambia Watanzania waache kulalamika kwa sababu ya njaa.

Jana, Sirikwa alifikishwa mahakamani na kushitakiwa kwa mujibu ya Sheria ya Uhalifu wa Kimitandao, ambayo ilianza kutumika tangu Septemba, mwaka 2015.

Kwa mujibu wa sheria hiyo, mtu atakayepatikana na hatia ya kuchapisha habari za uongo, za kuhadaa au kupotosha kwa kutumia kompyuta anaweza kuhukumiwa kifungo cha miezi mitatu jela na kuendelea au faini isiyopungua milioni mbili.

Katika mlolongo mzima wa mazungumzo ya mtalii huyo katika video hiyo iliyosambaa zaidi katika mtandao wa facebook, Sirikwa alipotosha moja kwa moja matamshi ya mtalii huyo kama ifuatavyo:

Mtalii: Hii ziara yangu nchini Tanzania imekuwa nzuri sana.  Watu ni wazuri na wenye urafiki.  Salamu kwa kawaida ni jambo.  Nina furaha kuwa hapa, ardhi ni nzuri.

Mwelekezi Utalii: anasema Watanzania mnalia sana njaa.  Kila siku mnalia njaa wakati mna maua nyumbani, si mchemshe maua mnywe, anasema si vizuri kulia njaa.

Mtalii: Aina nyingi za wanyama na watu ni wazuri, tofauti na sehemu zingine. Ni nzuri.

Mwelekezi Utalii: Anasema mnamuomba Rais wenu awapikie chakula, kwani Rais wenu ni mpishi, hangaikeni mfanye kazi, chemsheni hata nguo mnywe.

Mtalii: Ni kitu ambacho utakikumbuka katika maisha yako yote.  Ni nzuri na ni ya kupendeza.

Mwelekezi Utalii: Anasema mhangaikeni pembezoni mwa nchi, muache Rais hawezi kutoka Ikulu akuje kuwapikia chakula, hivyo mjipikie wenyewe. 
HIVI NDIVYO MWELEKEZI UTALII ALIVYOPOTOSHA MATAMSHI YA MTALII HIVI NDIVYO MWELEKEZI UTALII ALIVYOPOTOSHA MATAMSHI YA MTALII Reviewed by Unknown on 09:25 Rating: 5

No comments:

Theme images by merrymoonmary. Powered by Blogger.