VICTOIRE INGABIRE, KIONGOZI WA UPINZANI RWANDA NA MFUNGWA WA KISIASA MIAKA 15 GEREZANI
Kiongozi wa Upinzani na Mfungwa wa kisiasa nchini Rwanda, Victoire Ingabire. |
Na Malisa Godlisten
Victoire Ingabire, kiongozi wa Chama cha Upinzani cha FDU nchini Rwanda, ni mfungwa wa kisiasa ambaye anatumikia kifungo cha miaka 15 jela kwa tuhuma za uhaini.
Victoire amekuwa mwanaharakati wa kutetea haki za binadamu
na utawala bora kwa muda mrefu kabla ya kuamua kujiingiza rasmi kwenye siasa
mwaka 2009. Alizaliwa mwaka 1968 kupata
elimu ya msingi na sekondari nchini Rwanda, kabla ya kwenda nchini Uholanzi kwa
ajili ya elimu ya juu, ambapo alitunukiwa shahada ya kwanza ya Sheria za
Biashara na Uhasibu (Commercial Law &Accounting) na Shahada ya pili ya
Uchumi (Business Economics).
Baadae alifanya kazi katika taasisi kadhaa za kifedha nchini
Uholanzi kabla ya kuamua kujiingiza kwenye siasa rasmi. Victoire pia amewahi kushiriki katika
harakati mbalimbali akiwa mwanafunzi na baadae mtumishi nchini Uholanzi. Mwaka 1998 alichaguliwa kuwa Mwenyekiti wa
RDR kwa wanyarwanda waishio nchi za Ulaya.
Mwaka 2010 aliacha kazi nchini Uholanzi na kurudi Rwanda na
kujiingiza rasmi katika siasa. Mwaka
huohuo alichaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Shirikisho la Vyama vikuu vya Upinzani
nchini humo (RDR), na mgombea Urais kupitia vyama hivyo akitarajiwa kuchuana
Rais Kagame. Lakini jina lake
liliondolewa na Tume ya uchaguzi nchini humo na akafungiwa kujihusisha na
masuala ya kisiasa, kwa madai ya kufanya njama za kumpindua Kagame.
Siku chache baadae (October 14) mwaka huohuo alikamatwa na
kushtakiwa kwa makosa ya uhaini ambapo upande wa Jamhuri uliiambia mahakama
kuwa Victoire alishirikiana na baadhi ya wanajeshi katika jeshi la Rwanda na kula
njama za kupindua serikali ili kumuondoa madarakani Rais Kagame.
Katika kesi hiyo Victoire alishtakiwa pamoja na viongozi kadhaa
wa jeshi la Rwanda akiwemo Kanali Tharcisse Nditurende, Luteni Kanali Noel
Habiyaremye, Luteni Jean Marie Vianney Karuta na Meja Vital Uwumuremyi. Wote kwa pamoja walipatwa na hatia na kutupwa
gerezani ambapo Victoire alihukumiwa kifungo cha miaka nane gerezani.
Lakini alikata rufaa ya kupinga adhabu hiyo kwenye mahakama ya
juu (Supreme Court). Rufaa ya Victoire
ilikua na hoja mbili. Hoja ya kwanza ni
kwamba, makosa aliyodaiwa kuyatenda si ya kweli kwa sababu kipindi ambacho
makosa hayo yanadaiwa kutendeka alikua uhamishoni nchini Uholanzi. Kwahiyo asingeweza kupanga mbinu za kumpindua
Kagame akiwa uhamishoni.
Pili Victoire alipinga hukumu hiyo akidai kuwa sheria ilitumika
kinyume cha utaratibu. Sheria iliyompata
na hatia ilitungwa mwaka 2008 wakati anadaiwa kutenda kosa mwaka 2007. Wakili
wa Victoire aliiambia mahakama kuwa si sahihi kutumia sheria kinyumenyume (the
law should not be used retrospectively but retroactively).
Pia Luteni Kanali Michel Habimana aliyekua shahidi katika kesi
hiyo aliiambia mahakama kuwa upande wa Jamhuri ulifanya upotoshaji na
udanganyifu katika ushahidi. Alisema ushahidi
mwingi uliowasilishwa na Jamhuri ulikua umetengenezwa kwa lengo la kuwatia
hatiani Victoire na wenzie.
Alisema maafisa wengi wa jeshi waliotoa ushahidi
mahakamani walikuwa wameambiwa maneno ya kusema na walipachikwa vyeo bandia ili
ushahidi wao uwe na nguvu.
Baada ya mahakama hiyo kusikiliza hoja za pande zote mbili
ilisema kwamba, kifungo cha miaka nane gerezani aliyopewa Victoire ni kidogo
kulinganisha na makosa aliyofanya.
Kwahiyo mahakama hiyo ilimuongezea adhabu ya miaka
saba na kufanya kifungo chake kiwe miaka 15.
Luteni Kanali Habimana nae alihukumiwa kifungo japo inadaiwa kuwa baadae
aliuawa kwa siri akiwa gerezani.
Victoire Ingabire ni mke na mama wa watoto
watatu. Anategemea kumaliza kifungo
chake mwaka 2025.
VICTOIRE INGABIRE, KIONGOZI WA UPINZANI RWANDA NA MFUNGWA WA KISIASA MIAKA 15 GEREZANI
Reviewed by Unknown
on
16:42
Rating:
No comments: