RAIS MUGABE ASIFIA MISIMAMO YA TRUMP

Rais wa Zimbabwe, Robert Mugabe.
Zimbabwe
Rais wa Zimbabwe, Robert Mugabe amesema anakubaliana na sera ya Rais wa Marekani Donald Trump, kwamba "Marekani iwe ya Wamarekani".
Rais Mugabe, ambaye ndiye mara ya kwanza anazungumzia utawala wa Rais Trump, amesema alishangazwa na ushindi wa kiongozi huyo wa Republican.
Hata hivyo, amesema hakutaka pia "Madam Clinton ashinde", akirejelea mgombea wa chama cha Democratic aliyeshindwa uchaguzi wa Novemba mwaka jana Hillary Clinton.
"Lakini vilevile, ukija kwa Donald Trump ambapo anazungumzia uzalendo... Marekani iwe ya Wamarekani - katika hilo, nakubaliana naye. Zimbabwe iwe ya Wazimbabwe," Rais Mugabe amesema, kwenye dondoo ambazo zimechapishwa katika gazeti rasmi la serikali la Herald.
Ameongeza kwamba Rais Trump anafaa kupewa muda wa kudhihirisha uwezo wake.
"Sijui. Mpeni muda. Rais Trump huenda hata labda ataangalia upya vikwazo vilivyowekewa Zimbabwe," Rais Mugabe amesema.
Mahojiano kamili ya Rais Mugabe yanatarajiwa kupeperushwa rasmi kesho jioni kwenda sambamba na maadhimisho ya kusherehekea kiongozi huyo kutimiza miaka 93 tangu kuzaliwa kwake.
Rais Mugabe pia amesema anafaa kuendelea kuongoza, kwani watu wengi nchini mwake wanahisi kwamba hakuna mtu anayetosha kuchukua pahala pake.
Kiongozi huyo tayari ameteuliwa na chama tawala cha Zanu-PF kuwa mgombea wake wa urais katika uchaguzi mkuu wa mwaka ujao.
Rais Mugabe ameongoza Zimbabwe tangu ilipopata uhuru wake mwaka 1980.
CHANZO: BBC
RAIS MUGABE ASIFIA MISIMAMO YA TRUMP RAIS MUGABE ASIFIA MISIMAMO YA TRUMP Reviewed by Unknown on 16:32 Rating: 5

No comments:

Theme images by merrymoonmary. Powered by Blogger.