ZAIDI YA 20 BILIONI ZATOLEWA KUSAIDIA UHABA WA CHAKULA DODOMA NA SINGIDA


Na Chauya Adamu.
Kufuatia uhaba wa chakula katika baadhi ya maeneo nchini, Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula  Duniani (WFP) limepokea Euro milioni 9.5  (sawa na zaidi ya bilioni 20 za kitanzania) kutoka Umoja wa Ulaya (EU) ili kuunga mkono mradi wa kusaidia kukuza usalama wa chakula na lishe katika mikoa ya Dodoma na Singida.

Fedha hizo zimetolewa ili kuimarisha usalama wa chakula na lishe kwa zaidi ya watu 40,000 kwa lengo la kupunguza utapiamlo katika wilaya za Bahi na Chamwino mkoani Dodoma na Ikungi na Singida Vijijini katika mkoa wa Singida.

Akizungumza leo jijini Dar es Salaam, baada ya kutiliana saini juu ya mkataba wa kuendelea kusaidia kuimarisha hali ya lishe katika nchi maskini kama ilivyopangwa na Umoja wa Mataifa (UN), Mkuu wa Ubalozi wa umoja wa Ulaya nchini Tanzania, Roeland Van De Geer, amesema licha ya kuimarika kwa viashiria vingi vya afya katika muongo uliopita, bado hakuna hatua kubwa katika kuimarisha hali ya lishe ya watoto na wanawake nchini hapa nchini.
Roeland ameongeza kuwa “Viwango vya juu vya kuduma, kukosa uzito wa kuridhisha na upungufu wa viinilishe nchini kunaashiria dharura ya kimyakimya. Utayari wa kisiasa katika safu ya viongozi wa juu katika kukabili lishe duni nchini Tanzania kwa mtazamo wa sekta nyingi ni mageuzi makubwa”.
Hata hivyo ameongeza kuwa kupitia mradi huu, EU pamoja na WFP ziko katika nafasi nzuri ya kubaini na kuunga mkono uhusiano kati ya kilimo, afya, usalama wa chakula na lishe, ambao hapo kabla haukuwa umeelezwa kwa kina au kufuatiliwa kikamilifu.
Mradi huu unatumia uwepo wa muda mrefu wa WFP katika mikoa ya kanda ya kati ambapo uzoefu wake katika kutoa chakula chenye lishe na mawasiliano yenye una lengo la kubadilisha tabia ya kijamii kupitia vituo vya afya.
Kwa upande wake mwakilishi wa WFP, Michael Dunford alisema “Tunashukuru kwa mchango huu kutoka Umoja wa Ulaya kwani umeiwezesha WFP kuendelea na programu hii bunifu inayolenga kukidhi mahitaji ya watu walio hatarini zaidi, hasa watoto katika kile kipindi muhimu sana cha ukuaji wao, yaani siku 1,000 za mwanzo tangu kubebwa mimba hadi kutimiza miaka miwili,”
Aliongeza kuwa Programu hiyo itatoa ushahidi ambao utatoa mwongozo kwa jitihada za baadaye, na kwamba kuna uwezekano wa kuleta mabadiliko ya kudumu nchini.
Amesema viwango vya utapiamlo sugu miongoni mwa watoto unatokana na umaskini, ukosefu wa usalama wa chakula na ukosefu wa chakula cha kutosha kwa watoto wachanga na unyonyeshaji watoto.
Hata hivyo ameongeza kuwa Shirika la kusaidia watoto duniani (Save the Children) ni mshirika wa WFP katika kuimarisha ushirikiano na uwezo wa asasi zilizojikita katika jamii ili kuhamasisha uwezeshaji wa jinsia na uhusiano wa sekta mbalimbali katika suala la lishe, pamoja na kuratibu utekelezaji wa kipengele cha kilimo katika mradi.
Mradi huo ni sehemu ya majukumu ya WFP katika kufanikisha lengo la pili katika Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs) ambalo ni kufuta njaa  ifikapo mwaka 2030, ambapo WFP inashirikiana na washirika mbalimbali kama vile serikali, sekta binafsi na asasi za kiraia.
ZAIDI YA 20 BILIONI ZATOLEWA KUSAIDIA UHABA WA CHAKULA DODOMA NA SINGIDA ZAIDI YA 20 BILIONI ZATOLEWA KUSAIDIA UHABA WA CHAKULA DODOMA NA SINGIDA Reviewed by Unknown on 19:46 Rating: 5

No comments:

Theme images by merrymoonmary. Powered by Blogger.